Chadema kukutana kujadili uamuzi wa Mahakama

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeitisha kikao cha dharura kujadili uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo kushiriki kwa namna yoyote shughuli zote za kisiasa kwa muda na kutoka na uamuzi wa nini watafanya.

Uamuzi huo wa Mahakama umetolewa leo Jumanne Juni 10, 2025 na Jaji Hamidu Mwanga kufuatia kesi iliyofunguliwa na wanachama wa Chadema akiwemo aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti- Zanzibar, Said Issa Mohamed.

Kesi ya msingi kuhusu mgawanyo wa rasilimali za chama hicho imepangwa kuanza kusikilizwa Juni 24, 2025. Kilichofanyika leo ni uamuzi mdogo wa mapingamizi ya Mohamed na wenzake ya kuomba zuio la shughuli za kisiasa za Chadema hadi kesi ya msingi isikilizwe.

Usiku wa leo Jumanne, Chadema imetoa taarifa kwa umma juu ya kilichotokea. Taarifa imetolewa na Mkurugenzi wake wa Mawasiliano na Uenezi, Brenda Rupia ikidai kwa mtazamo wao, uamuzi huo umechochewa zaidi na shinikizo la kisiasa badala ya msingi wa kisheria au haki huku ukizingatia halo ya kisiasa ilivyo nchini.

“Chadema inachukulia hatua hizi kama ishara hatari ya kuporomoka kwa demokrasia nchini. Viongozi wa chama watafanya mkutano wa dharura kutathmini hali hii na kuamua msimamo rasmi wa chama kuhusu hatua za kuchukua,” amesema Brenda na kuongeza:

“Tunatoa wito kwa viongozi, wanachama, wafuasi wetu, na Watanzania wote wanaoamini katika misingi ya uhuru, haki, na demokrasia, kuwa tayari kupokea maelekezo kutoka kwa viongozi wakuu wa chama. Hatutarudi nyuma katika kudai Tanzania yenye mfumo wa haki, uhuru, na utawala wa sheria.”

Endelea kutufuatilia Mwananchi.

Related Posts