Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ameyataka mashirika na taasisi za Serikali kutoa gawio kulingana na fedha zilizokusanywa na matakwa ya sheria, badala ya kujikamua ilimradi zionekane zimechangia.
Vilevile, ameeleza umuhimu wa taasisi hizo kutoa gawio, akisema ndiyo msingi wa nchi kuendesha mambo yake bila kutegemea mikopo, suala ambalo litalifanya nchi ijenge heshima duniani.
Akisisitiza hilo, amesimualia jinsi Benki ya Dunia (WB) ilivyoweka vikwazo kuikopesha Tanzania kwa ajili ya kuendeleza bandari, lakini baadaye ikajitokeza kutaka kuikopesha baada ya kuona maendeleo yaliyofanyika kwa uwezo wa ndani.
Ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam leo, Juni 10, 2025 baada ya kupokea gawio la Sh1.028 trilioni, ikiwa ni ongezeko la asilimia 68 kutoka Sh767 bilioni zilizopatikana mwaka jana.
Gawio hilo ni kutoka taasisi ambazo Serikali ina hisa chache na mashirika yanayochangia asilimia 15 ya mapato yake ghafi.
Licha ya ongezeko hilo, Rais Samia amewataka wakuu wa mashirika na taasisi hizo, wasijikamue ili waonekane wametoa gawio, badala yake wachangie kwa mujibu wa sheria na faida waliyoitengeneza.
“Usione aibu hata ukichangia Sh1 bilioni au mbili, changia kwa faida uliyoitengeneza na siku hii hapa unavyoona wenzio wanachangia, ikupe chachu kwamba na wewe ukaongeze gawio lako ili nawe ukasomeke hapa,” amesema.
Amesema anatarajia mwakani kutakuwa na ongezeko zaidi na ili kufanikisha hilo, amemtaka Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu ahakikishe anaziwekea mazingira taasisi na mashirika ya umma ili zizalishe na Serikali ikusanye zaidi.
“Ukimkamua ng’ombe kiwele hakikujaa, hawezi kukupa maziwa mengi, lakini tukiwasaidia kiwele kikijaa wataenda kutoa kikubwa zaidi,” amesema.
Amesema lengo lake ni kuona angalau mashirika yanachangia asilimia 10 ya mapato yasiyo ya kikodi kwa Serikali, ingawa sheria inasema yatoe asilimia 15.
Amemtaka Mchechu aweke malengo na kuyasimamia kwa mashirika ili yachangie vizuri.
Hata hivyo, amesema katika gawio la mwaka huu ameshuhudia taasisi ambazo Serikali ina hisa chache zimeongoza katika uchangiaji, ukilinganisha na zile zinazotoa asilimia 15 ya mapato yake ghafi.
“Hii ni ishara muhimu ya manufaa ya ushirikiano wa kimkakati baina ya sekta ya umma na binafsi katika kuongeza tija na kuleta matokeo chanya katika utendaji wa taasisi zetu,” amesema.
Rais Samia amesema lazima ikubalike kuwa sekta binafsi ni kiungo muhimu katika safari ya mageuzi ya sekta ya umma na popote itakapoonekana haja ya ushirikiano watashirikiana nayo.
Akijenga hoja kuhusu umuhimu wa kutumia fedha za ndani, Rais Samia amesema mwaka juzi Serikali iliomba mkopo WB kwa ajili ya kuendeleza bandari, lakini taasisi hiyo ya fedha ilikuja na masharti lukuki ikionyesha kwa nini haitaweza kuikopesha Tanzania kwa shughuli hiyo.
Baada ya kuona Serikali imeanza kuiboresha bandari na inakusanya fedha kutokana na sekta hiyo, benki hiyo ikajitokeza yenyewe bila kufuatwa, ikitaka kuikopesha Tanzania Dola za Marekani 500 milioni (zaidi ya Sh1.302 trilioni).
“Mbossa (Plasduce, Mkurugenzi Mkuu wa TPA), akaja mbio kwangu, mama… nikamwambia mh! tulia kwanza usiharakishe. Hawa wameshaona kitu hawa, kaa nao zungumza nao ujue, wana kitu gani haswa, wasione kwamba tunaendelea, sasa hii 500 ikaja ikatutokea puani.
“Nikamwambia una fedha za kutosha kufanya uendelezaji, anza mwenyewe. Ukikwama tutaangalia, tunakwenda huko au tunakwenda wapi,” amesema.
Rais Samia amesema nchi ina fahari ya kufanikisha mambo yake yenyewe bila utegemezi na kwamba hata wakopeshaji wanakufuata, badala ya kuweka masharti lukuki.
Amefafanua kuwa kwa kadri inavyopandisha gawio kwa taasisi ndivyo ulimwengu utaiheshimu nchi kwa kuwa itaeleweka kuwa Taifa limeyajua mapungufu yake, limeyarekebisha na sasa linaanza kujitegemea.
“Na ile mkono wa nigawie nigawie, utakuwa unarudi kidogo kidogo, mfano mzuri ni kwa TPA baada ya kuwezeshwa na kuifanya bandari moja ya Dar es Salaam na Tanga sasa hivi zinafanya vizuri, zimeondoa mzigo mkubwa wa gharama kwa sekta binafsi tuliyoiweka pale,” amesema.
Amesema TPA kwa sasa haiwajibiki kugharimia ununuzi wa mitambo ya kushushia mizigo, badala yake inajikita na uendeshaji na kuipatia huduma stahiki sekta binafsi iliyopo.
“Kwa sababu wameondoa mzigo wa gharama za kuendeleza bandari, wao sasa watajielekeza kwenye kuweka miundombinu ya kuongeza bandari yetu ili wawezekezaji waje na mizigo zaidi iingie,” amesema.

Rais Samia Suluhu Hassan akihutubia viongozi pamoja na wageni mbalimbali kwenye hafla ya kupokea gawio la Serikali katika hafla iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam leo Juni 10, 2025.
Amesema mageuzi ni hatua na kulikofikiwa sasa ni tofauti na zamani.
“Lengo letu ni kuyafanya mashirika yakope kwa uwezo wake wa kifedha ili tupunguze mzigo wa mkopo kwa Hazina, tupunguze mzigo wa deni la Taifa.
“Mashirika kama TPA, TPDC yanaweza kukopa kwa hali zao za kifedha na mkopo ukawa wa kwao na si deni la Taifa na wakafanya maendeleo makubwa tu ndani ya nchi. Huko ndiko tunakoelekea,” amesema.
Akizungumza baada ya kutoa gawio, Mbosa amesema mabadiliko yaliyofanyika katika uendeshaji wa bandari ndiyo siri ya mafanikio.
Amesema yamesaidia kupunguza gharama za uendeshaji zilizokuwa zikitumika awali kwa asilimia 46.
Amesema kabla ya kuingia kwa wawekezaji matumizi ya kawaida, ikiwemo kununua mitambo, vifaa zaidi Sh1.1 trilioni zilikuwa zikitumika lakini sasa zimeshuka hadi Sh537 bilioni.
“Huu ni upungufu wa zaidi ya asilimia 46 na hiyo ni kwa sababu eneo kubwa ambalo linaendeshwa na wawekezaji sasa wao ndiyi wanabeba gharama zote na hii ndiyo sababu tulikuwa tukiwaambia wananchi wawekezaji hawa wana mtaji kwa sababu wao wanaweza kubeba gharama ambazo tulikuwa tukizibeba awali,” amesema.
Amesema fedha ambayo zilikiwa ikitumika awali sasa zinapelekwa katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali, ikiwemo kupanua bandari iliyopo Mtwara, ujenzi wa matenki ya mafuta kwa zaidi ya Sh600 bilioni, Bandari ya Mbambabay zaidi ya Sh70 bilioni sambamba na Kemondo ya Bukoba na huduma nyingine.
“Sasa na si gawio tu na kodi kubwa tunatoa na hili linatokana na mabadiliko tuliyofanya. Siri ya kuendelea kuchangia gawio hili ni mabadiliko ya kiutendaji ambayo tumefanya na tunayoendekea kufanya,” amesema Mbossa.
Amesema fedha zilizotolewa zitakwenda kuifaa nchi kwenye mambo kadhaa na kwamba imepunguza utegemezi uliokuwepo katika miaka ya nyuma.
“Tukiendelea hivyo kila mwaka tunapunguza utegemezi na tunaenda kwenye kujitegemea,” amesema akisisitiza dhamira ya Serikali ni kuhakikisha mashirika yanajitegemea badala ya utegemezi kwa Serikali kuu.
Katika kipindi hicho, amesema tayari Stamico na TPDC zimeshajitoa kwenye ruzuku za Serikali na zinajiendesha zenyewe kwa mishahara na uendeshaji.
Amesema mashirika 11 kati ya 13 yaliyokuwa na mtaji hasi yametoka kwenye makundi hayo na sasa yana mtaji chanya na mengine manane kati ya 13 yaliyokuwa yanapata hasara mfululizo, yametoka kwenye kundi la hasara na sasa yanapata faida.
Amemtaka Mchechu aendelee kufanya tathmini na kuchukua hatua zaidi kwa sababu ana uhakika mashirika hayo yanaweza kufanya kazi zaidi.
Amesema kazi ya uandaaji wa dashibodi ya mashirika ya umma imekamilika na kuanzia sasa kutakuwa na uwazi, kwani kila taasisi itaona ukuaji na kuporomoka kwake.
“Itarahisisha kufanyika kwa uamuzi wa kiutendaji na kimkakati katika ngazi zote, kwa ujumla uwekezaji uliofanywa na Serikali katika mashirika ni mkubwa na bila shaka ufuatiliaji nao unapaswa kuendana na ukubwa huo,” amesema.
Ameyataka mashirika kuongeza ubunifu ili kukuza ufanisi wa utendaji na kutatua changamoto zinazowakabili, ikiwemo upatikanaji wa mitaji.
Katika hilo, amesema Serikali imeongeza uwekezaji lakini bado mahitaji makubwa.
“Sasa mageuzi haya ni pamoja na kuwa wabunifu, tusisubiri Serikali itatue kila kitu. Tutumie fursa mbalimbali zinazotuzunguka katika kutatua changamoto hizo, ikiwemo kuingia kwenye soko la mitaji na kuongeza ushiriki wa wananchi,” amesema.
Amemtaka Mchechu kufanya utafiti ili kujua na kubainisha taasisi zenye mwelekeo na viwango vya kuingia kwenye soko la mitaji, ili zikavune mitaji, badala ya kutegemea serikalini pekee.
Pia ameyataka kuimarisha matumizi ya Tehama kwa kuwa yametoa uhakika kuwa makusanyo yataongezeka zaidi iwapo itatumika.
Ili kufikia mafanikio hayo, amemtaka Profesa Mkumbo kusimamia ukamilishaji wa sheria ya uwekezaji wa umma, ili kuhakikisha azma ya kuimarisha usimamizi na kuwa na mfuko wa uwekezaji inafikiwa.
“Kwa jina lolote mtakaloita itakuwa sawa, mfuko wa uwekezaji sijui, jina lolote ambalo halitaleta utata kisheria ndani ya nchi yetu. Kwa sababu najua kipengele kimoja kinachochelewesha sheria hiyo ni mfuko huo,” amesema.
Taasisi, mashirika yaliyofanya vizuri
Amezitaja taasisi na mashirika yaliyofanya vizuri kuwa ni Twiga Minerals iliyotoa gawio la Sh93.6 bilioni, ikifuatiwa na Airtel Tanzania na Airtel Money iliyotoa Sh73.9 bilioni.
Mengine ni NMB (Sh68.1 bilioni), Puma Energy Tanzania (Sh13.5 bilioni), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (Sh11.7 bilioni) na NBC Sh10.5 bilioni.
Kwa upande wa mashirika yanayotoa asilimia 15 ya mapato yake ghafi, iliyoongoza ni Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) iliyotoa gawio la Sh181.5 bilioni ikifuatiwa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) iliyotoa Sh38.8 bilioni.
Mengine Wakala wa huduma za Misitu Tanzania (Sh29.8 bilioni), Wakala wa Usajili wa Biasahara la Leseni (Sh20.4 bilioni), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (Sh19.2 bilioni), Shirika la Uwakala wa Meli (Sh16.3 bilioni) na Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (Osha) iliyochangia Sh10.4 bilioni.