Heche: Tabora inafaa kuwa mji wa viwanda vya mbao, tumbaku

Tabora. Makamu Mwenyekiti wa Chadema, John Heche  amesema mji wa Tabora unapaswa wa kitovu cha viwanda vya kuchakata mazao ya misitu na zao la tumbaku.

Akihutubia mkutano wa hadhara mjini Tabora leo Juni 10, 2025, Heche amesema uwepo wa viwanda utaongeza siyo tu thamani ya mazao ya misitu na tumbaku, bali pia pato na uchumi wa wakazi wa mkoa huo na Taifa kwa ujumla.

“Kujenga viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya misitu ikiwemo mbao ngumu inayopatikana kwa wingi mkoani Tabora kutawezesha Taifa kuokoa fedha za kigeni zinazotumika kuagiza bidhaa za mbao ikiwemo samani kutoka nje ya nchi,” amesema Heche

Huku akionyesha msisitizo, Heche amesema; “Licha ya kuwa na misitu inayozalisha mbao kwa wingi, Tanzania ikiwemo taasisi za umma bado inaagiza samani za ofisi na majumbani kutoka nchi za nje. Tanzania tunapaswa kuvuna mbao, kuzichakata na kutengeneza samani kwa mahitaji ya ndani na kuuza ziada nje ya nchi,”

Akizungumzia zao la tumbaku, kiongozi huyo wa Chadema amesema kuna haja ya kuugeuza mji wa Tabora kuwa kitovu cha viwanda vya kuchakata na kuongeza thamani, badala ya kuuza tumbaku ghafi katika soko la nje.

Makamu Mwenyekiti wa Chadema, John Heche akipokea michango ya Tone Tone kutoka kwa wananchi waliohudhuria mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Uyui mjini Tabora.

“Kiwanda cha tumbaku kinapaswa kujengwa Tabora kutokana na wingi wa uzalishaji wa zao hilo katika wilaya za Mkoa wa Tabora. Lakini kwa miaka 63 ya uhuru, hakuna kiwanda cha kuongeza thamani ya tumbaku kimejengwa Tabora,” amesema Heche.

Kwa mujibu wa makadirio ya takwimu za uzalishaji kutoka Bodi ya Tumbaku, Kanda ya Tumbaku ya Tabora inayojumuisha wilaya nane inatarajiwa kuzalisha zaidi ya tani 136.2 milioni za tumbaku kwa mwaka 2024/25 kulinganisha na zaidi ya tani 60 milioni zilizozalishwa msimu wa kilimo wa 2023/24.

Zao la tumbaku linalimwa katika wilaya 21 ambapo zaidi ya asilimia 95 ya zao hilo huuzwa kwenye masoko ya nje ya nchi na mauzo yake yameongezeka kutoka Dola za Marekani 106,278,461 mwaka 2020/2021, hadi kufikia Dola za Marekani 389,556,750 mwaka 2023/2024.

Kilimo cha zao hilo kinatoa ajira kwa zaidi ya kaya ya 100,000 wanaolima kati ya ekari moja hadi tano huku mnyororo wake wa  thamani ukinufaisha zaidi ya kaya 400,000.

Kuna aina tatu za tumbaku zinazolimwa hapa nchini ambazo ni  ya kukausha kwa moshi, inayokaushwa kwa mvuke na tumbaku ya kukaushwa kwa jua huku aina ya tumbaku inayolimwa kwa wingi nchini ni ile ya kukaushwa kwa mvuke na kwa moshi.

Zao la tumbaku linalimwa kwa wingi  katika wilaya za Tabora, Kagera, Kigoma, Shinyanga, Iringa, Mbeya, Singida na Rukwa

Wilaya nyingine inayolimwa tumbaku ni Urambo, Kahama, Chunya, Kasulu, Ushetu, Manyoni, Nzega, Namtumbo, Songea, Kaliua, Sikonge, Uyui na Serengeti.

Related Posts