Taifa limetekwa na mkumbo wa kauli mbiu (slogan). Upande mmoja ulianza kuchafua mitandao ya kijamii kwa kuandika maoni kwenye kila posti ya mtu maarufu; No Reforms, No Election. Kwamba bila mabadiliko ya sheria hakutakuwa na uchaguzi.
No Reforms, No Election ni kauli mbiu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), msingi wake ni kusukuma presha kwa dola na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), kwamba bila kufanyika mabadiliko ya Katiba na sheria za uchaguzi, mwaka huu (2025) hakutakuwa na uchaguzi mkuu.
Mwanamuziki anaposti wimbo wake mtandaoni. Msululu wa watu unainuka na maoni, “No Reforms, No Election.”
Tena hawaandiki kwa usahihi, wao wanatupia “No Reform, No Election”. Herufi “s” kwenye Reforms hawaiweki. Ni kipimo kuwa wamedaka slogan juu kwa juu na kuisambaza bila kuielewa vema.
Unaandika taarifa ya msiba, wanakutana na “No Reforms, No Election.” Kuna viongozi wakafunga uwanja wa maoni. Wasanii na watu wengi mashuhuri wameshindwa kuvumilia na kuamua kuzuia maoni kwenye posti zao za mitandaoni.
Niliona kejeli kutoka timu ya No Reforms, No Election, ikihoji, CCM wanajinasibu kuwa na wanachama 13 milioni, ambao iliwatangaza kwenye Mkutano Mkuu Mei 29, 2025, mbona sasa hawaonekani kupambana na No Reforms, No Election?
Kejeli ile ilichokoza nyuki. Yaliibuka mafuriko ya maoni ya “Oktoba Tunatiki.” Posti yoyote ya mtu maarufu au kiongozi, unakutana na mashindano ya maoni ya “No Reforms, No Election” dhidi ya “Oktoba Tunatiki.”
Katika sayansi ya siasa, mchuano wa No Reforms, No Election na Oktoba Tunatiki unaitwa vita ya kisiasa (political war). Na mbinu za political war ni mbili; propaganda na presha ya kisaikolojia (psychological operations “PsyOps”).
Mashambulizi ya No Reforms, No Election, kwenye maoni ya posti za viongozi na watu maarufu, bila shaka lengo lilikuwa kuonesha mamlaka za nchi kwamba mitaa haitaki chochote zaidi ya No Reforms, No Election. Hiyo ni propaganda, vilevile PsyOps.
Ukifuatilia maoni ya No Reforms, No Election, zinatumika zaidi akaunti bandia. Unakuta No Reforms, No Election nyingi, kila ukifuatilia waweka maoni hayo, si watu halisi. Akaunti hazijawahi kuposti chochote.
Ilikuwa rahisi kutambua kwamba kuna watu wamefungiwa mahali, au wamewekwa vituo tofauti, wanaendesha akaunti bandia, kazi yao ni kuvamia posti za viongozi na watu maarufu ili kufikisha ujumbe kwamba taifa limesimama katika No Reforms, No Election.
Upande fulani waliweza kutengeneza mkumbo wa kisiasa. Hata baadhi ya watu halisi, wakitumia akaunti zao halali, walianza kushambulia kwa maoni, No Reforms, No Election. Wakiamini ndiyo fasheni ya kuwa mwanaharakati.

Kisha sasa, Oktoba Tunatiki wakajibu mapigo. Oktoba Tunatiki ni kauli mbiu au kampeni ya CCM kuwa ikifika Oktoba 2025, siku ya Uchaguzi Mkuu 2025, itakuwa kutiki (kumchagua), mgombea wao wa kiti cha Urais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
Ni vita ya “hakuna uchaguzi bila mabadiliko” dhidi “uchaguzi upo na Oktoba tunamchagua Rais Samia.”
Kila upande unatumia janja ya kisiasa kuonesha unakubalika. No Reforms, No Election, wanataka ifahamike wapo wengi nyuma ya agenda hiyo.
Oktoba Tunatiki, nao wanafikisha ujumbe kwamba namba kubwa ipo kwao na hakuna wa kuzuia uchaguzi. Njia ni zilezile za akaunti nyingi bandia na chache halisi.
Mashambulizi ya No Reforms, No Election na Oktoba Tunatiki, jumlisha matokeo ya kuibuka wafuata mkumbo, halafu wachukue waliofungia maoni. Jawabu la pamoja unapata ugonjwa unaoitwa mashaka ya kisiasa.
Dalili za mashaka ya kisiasa ni wasiwasi usiokoma kuhusu matukio ya kisiasa. Ipo wazi, mfumuko wa maoni ya No Reforms, No Election, ni matokeo ya wasiwasi kwamba mwenendo ulivyo, wanaweza kuendelea kupuuzwa na uchaguzi utafanyika. Kisha, watakuwa wamepoteza kila kitu.
Kadhalika, Oktoba Tunatiki ni matokeo ya wasiwasi kuwa maoni ya No Reforms, No Election, yakiachwa yatawale, yanaweza kusababisha uharibifu mkubwa wa kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Dalili ya pili kuwa nchi inaumwa mashaka ya kisiasa ni jinsi watu wanavyoshindwa kujikita kwenye mambo mengine ya kila siku, badala yake, No Reforms, No Election, vilevile Oktoba Tunatiki, ndiyo zinashika hatamu.
Mtu anaposti biashara yake apate wateja, auze apate fedha za kuendesha maisha yake na watu wanaomtegemea, wateja wanashindwa kuuliza hata bei, wanahofia wimbi la No Reforms, No Election pamoja na Oktoba Tunatiki.
Mawazo ya siasa yanatuama kwenye vichwa muda wote. Watu wametekwa na taarifa za mitandaoni, wakifuatilia kwa ukaribu, kila kinachoendelea kuhusu mchuano wa No Reforms, No Election dhidi ya Oktoba Tunatiki. Ni matokeo ya Mashaka ya kisiasa.
Dalili nyingine ya ugonjwa huo ni watu kuchokozeka kirahisi kisiasa, kupoteza matumaini au hata kukata tamaa.
Kitendo cha kukimbilia kufunga maoni, ni pointi kwamba unachokozeka kwa urahisi. Kiongozi wa kisiasa hapaswi kuchokozeka kirahisi, tena uchokozi wenyewe ukiwa ni siasa.
Mashambulizi ya No Reforms, No Election mitandaoni ni ishara ya kupoteza matumaini ya kufanikiwa kwa njia sahihi. Hivyo, wakaamua kubuni mpango wa kuchafua mitandao kwa imani kuwa presha ikiwa kubwa, wanaweza kueleweka.
Mwisho kabisa, No Reforms, No Election na Oktoba Tunatiki ni matokeo ya kupaniki kisiasa. Hiyo ni sehemu ya mashaka ya kisiasa (Political Anxiety.)
Walioanzisha walipaniki, ndiyo maana walichagua kufanya fujo mitandaoni badala ya kujenga hoja.
Waliojibu nao walipaniki, wakatembea kwenye mdundo uleule ulioanzishwa na waliopaniki.
Hayo yanatokea kwa sababu vyama vya siasa na wanasiasa, wamechagua kufanya siasa bila misingi. Madhara ya kijamii ni makubwa sana. Watu makini, wenye misingi, hawawezi kuibua taharuki za kimtandao ambazo hazijengi.