NIKWAMBIE MAMA: Wanaodhaminiwa kuongoza wakumbushwe historia

Napenda kulipongeza Jeshi kwa ujumla wake kwa mkakati wao wa kurudisha uzalendo kwa Watanzania.

Kipindi cha nyuma kujiunga na Jeshi la kujenga Taifa ilikuwa si hiyari. Mtu yeyote aliyekuwa tayari kulihudumia Taifa alilazimika kupitia hapo ili kufundishwa uzalendo na jinsi ya kujilinda mwenyewe na Taifa lake. Ubinafsi ni neno lililotakiwa kufutika kabisa kwenye kamusi yake ya ubongoni.

Mafunzo haya ni muhimu sana hasa kwenye kizazi cha sasa ambacho kinalelewa au kujilea katika utandawazi.

Yanawakumbusha vijana kuwa na maadili mema katika jamii na uwezo wa kujitegemea hata kwenye wakati mgumu.

Pia vijana wanapata fursa ya kujifunza ujasiliamali, kupitia mafunzo ya Kilimo, Ufugaji na Biashara. Ni fursa ya kipekee kwani karibu kila kijana aliyehitimu Elimu ya Msingi ana nafasi ya kujumuika nayo.

Lakini hii pia ni nafasi adhimu kwa viongozi wetu watarajiwa. Fujo tunazoziona zikipamba moto siku baada ya siku zinatokana na watu wetu kutoelewa historia yao wenyewe.

Wagombea viti huko Majimboni wamefikia kujenga uhasama na kutengenezeana ubaguzi kwa wananchi kama watu wanaotoka kwenye sayari tofauti.

Naamini wangekuwa tayari hata kurushiana magruneti kama wangekuwa nayo. Wengi wao hawakijui au wamekisahau kile Chuo muhimu cha Mwalimu Nyerere Memorial Academy (MNMA). Kilianza kama Kivukoni College mwaka 1961 na kinatambulika kwa nafasi yake kubwa katika siasa na mafunzo ya viongozi wa Tanzania.

Kilianzishwa na mama mmoja wa Kiingereza lakini mzalendo wa Kitanzania, Joan Wickens aliyefariki mwaka 2005 huko kwao Uingereza baada ya kuitumikia Tanzania karibu maisha yake yote.

Huyu ndiye aliyekuwa akimsaidia Waziri Mkuu wa Kwanza wa Tanganyika baadaye Rais wa kwanza wa Tanzania, Julius Nyerere kuhimili kuiongoza Tanganyika huru.

Alianza kufanya kazi na Nyerere kabla ya Tanganyika kupata Uhuru na kubakia kuwa msaidizi wake hadi kufariki kwa Rais huyo mstaafu mwaka 1999.

Joan Wickens alizunguka sehemu mbalimbali za Tanzania kukusanya fedha za kusaidia kufadhili ujenzi wa Chuo cha Chama Kivukoni.

Sote tunajua kisa cha wanafunzi kuvaa sare ni kufanana. Pamoja na sababu zingine za utambulisho, lakini sare zinaenda mbali zaidi kwa kuweka uzani sawa baina ya wanafunzi. Zinasawazisha tofauti za malezi ya wanafunzi huko majumbani mwao na kuwaweka katika daraja moja.

Asijulikane aliyetokea familia ya matajiri aliyelelewa kama yupo Amsterdam, wala yule mwenye wazazi makapuku aliyeishi maisha ya paka wa jalalani.

Kwa namna iliyofanana na hiyo, Chuo cha Chama Kivukoni kiliwanyosha viongozi watarajiwa kuwa wazalendo bila kujali utajiri wao, ukabila, udini, uchifu na kadhalika.

Uzalendo ndio kilikuwa kitu cha kwanza ambapo viongozi waliwachukulia Watanzania kama ndugu. Nakumbuka Mwalimu Nyerere aliwazoesha watu wake kuitana “Ndugu Waziri” badala ya “Mheshimiwa Waziri.”

Matokeo mazuri yalionekana japo mengine si moja kwa moja, lakini ari ya viongozi kuepuka rushwa na ufisadi ilikuwa juu.

Kwenye vituo vya afya na Jeshi la Polisi rushwa ilikuwa ni kitu cha ajabu kabisa. Hata mashuleni watoto waliujua wimbo wa “Rushwa ni adui wa haki, sitatoa wala kupokea rushwa”. Haya ni sehemu ya mafanikio ya mafunzo yaliyotolewa na Chuo cha Chama Kivukoni.

Hivi sasa watu wanatia nia ya kugombea uongozi kwa sababu tu wanataka kuvaa kofia hizo, au wameshawishika na kukubalika kwao ndani ya jamii.

Vyama vinaliona hilo, lakini kwa sababu vina uhakika na kukubalika kwa mtia nia havisiti kumpa dhamana kutimiza lengo lake. Kila chama kinalenga kupata viti vingi kwenye Bunge na Baraza la Madiwani, hivo ni rahisi kuyaweka mambo mengine kando ilimradi maisha yaendelee.

Suala la weledi wa kazi linakuja baadaye. Ni sawa na wanaume wanaosema “Mwanamke sura, tabia tutafunzana ndani.”

Inawezekana wapo sawa, lakini ni kweli wanafunzana au wanapigana? Waswahili husema “samaki hukunjwa angali mbichi”, na tuliona viongozi waliopitia Chipukizi, Skauti, Umoja wa Vijana na JKT walivyoiva kiasi cha kutokutetereka hata pale mambo yalipokuwa magumu.

Athari za kuondoka kwa mifumo ile adhimu zinaanza kuonekana tangu kwenye kampeni. Mgombea wa chama kimoja humuona mpinzani wake kama kunguru aliyeingia kwenye tundu lake la njiwa.

Atawahamasisha wapiga kura kulifukuza joka hilo” kama waumini wanavyohamasishwa kumkataa shetani.

Ubaguzi unapandishwa na kauli mbiu ya “Watanzania wote ni ndugu” inashushwa.

Pindi mgombea asiye mzalendo anapofanikiwa kulitwaa jimbo, upande uliokuwa kinyume naye unageuka haramu.

Makundi yanachukua nafasi na jimbo linagawanyika. Lakini kwa kuwa wananchi ndio nyenzo ya kwanza ya maendeleo, jimbo linakosa ushirikiano wa wananchi na kuanza kupoteza nuru yake.

Kiongozi atakuwa akirudi kila baada ya miaka mitano kuomba kuaminiwa katika vipindi vingine bila kujua kuwa sumu aliyoimwaga jimboni ingali ikifanya kazi.

Ni muhimu kwa vyama kujiridhisha na wagombea wao. Muasisi wa Taifa, Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kuwa mnaweza kumpenda mtu hadi msile wala kunywa bila yeye kuwepo.

Lakini hicho si kigezo cha kumpa uongozi kwani uongozi ni wito. Ni lazima awe na kiwango cha juu cha uzalendo, kujitoa kwa ajili ya watu.

Related Posts