Katika kufanya utafiti wangu usio rasmi, nimegundua mambo ya ajabu. Naweza kujiita mgunduzi wa karne hii kwenye sayansi ya jamii. Nianze na niliyogundua.
Mosi, nimegundua kuwa fyatu anaweza kwenda shule asielimike. Kifyatu, hii inaitwa education for ignorance. Fyatu anaweza kuoga lakini akabaki mchafu achia mbali kutakata.
Pili, Fyatu anaweza kula kwa miguu na mikono lakini akaishia kuwa na njaa asishibe. Kuna wagonjwa wanaoonekana wazima na wazima wanaoonekana wagonjwa.
Kuna wajinga wanaoitwa wasomi na wasomi wanaoitwa wajinga. Usomi na ujinga vinapokosa tofauti, nini faida ya kusoma? Wapo walioelimika bila kusoma kama shehe Karume na waliosoma wasielimike kama maprofesa waliogeuka marais wakaangamiza kaya zao. Kwani hawapo?
Tatu, wajinga wanapogeuzwa wasomi na wasomi wajinga, kuna tatizo. Waadilifu wanapochukiwa wakapendwa wabadhilifu, uje kuna tatizo.
Maadili yanapogeuzwa madili, jua kuna balaa. Haramu inapogeuzwa halali, unategemea nini? Dini zinapogeuzwa maduka na zana za kutajirika haraka, unategemea nini? Unategemea nini makaburi ya watakatifu yanapotunzwa na walevi na wazinzi?
Nne, mafyatu wanapoacha kufikiri na kuchapa kazi wakashikilia kuomba na kungoja miujiza, ni nini kama si ajabu la maajabu?
Kwani hayapo? Hakuna muujiza kama kuchuuzwa kwa neno la Mungu tena kufanywako na matapeli wa kawaida kwa kutumia ujinga na si weledi.
Ni ujinga kiasi gani samaki kufa kwa kiu mtoni? Fyatu zwazwa anakwenda kwa mganga wa kienyeji maskini na mpumbavu kutafuta utajiri. Lo! Kweli nguruwe anaweza kumfunza tausi usafi au mbwa kumfunza mbwa mwitu uhuru? Je nune anaweza kujua siri ya unene japo yu anenepa kwa kuishi kwenye kinyesi? Je kuku anaweza kumfunza uhuru kanga?
Nyangumi, pamoja na ukubwa na umwamba wake huuawa na pomboo. Simba pamoja na ukali wake hawatishi nyuki.
Ni heri kuwa nyuki mbele ya simba kuliko kuwa kondoo mbele ya mchinjaji. Nyoka, pamoja na sumu yake, huwagwaya vicheche.
Nyuki, pamoja na ukali wao, hawafui dafu mbele ya nyegere. Je siri ya haya yote ni nini? Ni kujiamini, kujitambua, na umoja. Hii ndiyo injili yangu kwa mafyatu.
Unaweza kutajirika lakini ukabaki maskini. Unashangaa! Jiulize. Kwanini wapigaji wengi wa mali za mafyatu ni matajiri lakini wasioacha kupiga? Kama siyo umaskini nini kuiba na kusababishia wengine mateso hata vifo kana kwamba hutokufa?
Kama unashangaa bado, basi angalia bara la Afrika. Linasifika kwa kuwa na maliasili zenye thamani zinazohitajika na kutegemewa sana duniani. Ajabu, bado ni maskini wa kunuka! Afrika inafyatuliwa ndani na nje huku mafyatu wakiendelea kufyatuliwa na kusota bila sababu yoyote ya msingi isipokuwa kukataa kufyatuka na kuufyata.
Mafyatu wamegoma kufyatuka na kuuliza maswali ya kifyatu. Mfano, inakuwaje mkurugenzi anayesafiria ndinga la nusu bilioni, kila mwaka, anaripoti hasara?
Je hapa mchawi ni biashara kugoma au israfu ya wakuu wa kampuni au shirika kama hili? Tumenunua mapipa, tena mapya, kutoka kila kona. Ajabu ya maajabu, mafyatu wachache tuliowakabithi mashirika kama Eya Danganyika, Shirika la Relwe na mengine mengi yanayosifika kuingiza hasara si faida.
Je njuluku inakwenda wapi? Je hii siyo biashara kichaa? Haiwezekani isiwe wakati ni kichaka cha upigaji. Ajabu, wakati haya yakiendelea, tunasifiana kudumisha amani! Amani gani ya imani? Kuna amani gani katikati ya dhuluma, jinai, wizi, uchawa, kujipendekeza, uzembe, ubabaishaji, na mazabe mengine ya kizwazwa? Hamjaambwa kuwa mjenga na mbomoa kaya ni mwanakaya mwenyewe?
Wakati haya yakiendelea, utayasikia mabambataa mabingwa wa kwaya wakisifu hata uchafu.
Mengine yamepiga book hadi uprofesa uliogeuka uprofedheha kama si fedheha. Kama kuku, tunazalisha tusichokula na kula tusichozalisha halafu tukiitwa kuku tunaamba twatukanwa! Ebo! Sasa mnataka muitwe nini wakati mfanyacho ni ukuku? Juzi nilimsikia profedheha mmoja chawa na bingwa wa kujikomba akisema eti sisi tunaongoza kwa demokrasia duniani! Dunia gani au ile ya ndoto na mapambio?
Tunaongoza vipi wakati fyatu mdogo aliyeteuliwa si kuchaguliwa anaweza kuzuia wapingaji kufanya mikutano yao ya kikatiba? Tunaongoza nini wakati wizi wa kura kwenye uchakachuaji ni sehemu ya maisha?
Tunaongoza vipi wakati bado tuna walaji wanaokula mafyatu kwa sababu ya surnames zao? Tunaongoza nini wakati tunajitahidi hata kufunga uhuru wa kufikiri mbali na kuhabarishana?
Tuna sharia ngapi za hovyo za kukandamiza vyombo vya umbea? Je hii nayo ni demokrasia au kadhia? Demokrasia gani katika uchakachuaji na ukandamizaji?
Mwisho, demokrasia ni pamoja na haki na uhuru vya mafyatu. Penye ubangaizaji, usanii, uzembe, upigaji, na ufujaji wa njuluku za mafyatu hapawezi kuwa na demokrasia wala haki. Demokrasia ni kula na kushiba na siyo kumeza mate wakati wachache wakifakamia na kupwakia kwa mikono na miguu.
Hii ndiyo injili ya leo kama ilivyoandikwa na mwenye dhambi Daktari, Profesa, Muadhama, Shehe Fyatu Mfyatuzi. Hivi nitaruhusiwa lini toka hospitali ya vichaa?