Songwe. Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo amewataka wakuu wa idara na vitengo wa Halmashauri za mkoa huo, kusimamia fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo hata baada ya mabaraza ya madiwani kuvunjwa.
Chongolo ametoa wito huo wakati wa kikao cha baraza la madiwani katika halmashauri ya Ileje lililofanyika kwa ajili ya kujadili hoja za Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG).
Kikao hicho kilichofanyika leo Jumatano Juni 11, 2025, kimehudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, kamati za ulinzi na usalama za mkoa na halmashauri, wataalamu wa halmashauri, pamoja na madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje.
Chongolo amewataka wataalamu wanaobakia kutekeleza majukumu ya kitaalamu kutotumia mwanya wa kuvunjwa kwa mabaraza ya madiwani kufanya mambo kiholela.
“Hakikisheni fedha zinalindwa zaidi, kila mkuu wa idara anatakiwa ajibadilishe kuwa diwani kulinda fedha za Serikali na kuziba mianya ya ufujaji wa fedha hizi,” amesema Chongolo.

Madiwani wa halmashauri ya Ileje wakiwa kwenye kikao cha kujadili hoja za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG). Picha na Denis Sinkonde
Amevitaka pia vyombo vinavyosimamia utendaji wa halmashauri navyo vijibadili kuwa kama wajumbe wa baraza la madiwani sambamba na kuwa jicho la kuangalia kila taratibu zinazofanyika kwenye halmashauri zao.
Mkuu huyo wa mkoa amesema vyombo vyote vya usalama vimeunganishwa na vina jukumu la kufuatilia kwa karibu matumizi ya fedha za Serikali.
Ametaja vyombo hivyo kuwa ni pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mkuu wa Wilaya ambaye ni msimamizi mkuu wa shughuli zote za Serikali ngazi ya wilaya, pamoja na Katibu Tawala wa Wilaya ambaye pia ni mjumbe wa baraza la madiwani na vikao vya Wakuu wa Idara (CMT) wa halmashauri.
“Macho yote yanapaswa kuelekezwa kwenye vikao vya halmashauri ili kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa,” amesema Chongolo.
Aidha, amewataka maofisa tarafa kuwajibika kwa nafasi zao kwa kuwa ni wawakilishi wa Serikali Kuu katika ngazi ya serikali za mitaa. Amesisitiza kuwa katika kipindi hiki ambacho mabaraza ya madiwani yanakaribia kuvunjwa, maofisa hao wanapaswa kusimama imara na kuhakikisha masilahi ya Taifa yanalindwa katika kila hatua.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje, Ubatizo Songa amewasihi wakuu wa idara na vitengo ndani ya halmashauri hiyo kushirikiana kwa karibu katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.
Amesema hiyo itasaidia kuhakikisha usimamizi thabiti wa fedha za miradi na kuepusha hoja kutoka kwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
“Kutokuwepo kwa baraza la madiwani katika kipindi hiki cha uchaguzi huchangia kuibuka kwa hoja nyingi kutoka kwa CAG, hasa pale ambapo baadhi ya watumishi hawasimamii ipasavyo matumizi ya fedha za umma. Hivyo, kila chombo kinapaswa kutimiza wajibu wake kama alivyoelekeza Mkuu wa Mkoa,” amesema Songa.
Akihitimisha hotuba yake, Chongolo ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Ileje kwa kupata hati safi kutoka kwa CAG.
Amesema mafanikio hayo ni ishara ya usimamizi mzuri wa rasilimali za umma, uwajibikaji, uwazi na uadilifu katika utendaji kazi wa serikali za mitaa.