Matarajio bajeti ya Zanzibar 2025/2026, ikiwasilishwa Baraza la Wawakilishi

Unguja. Wakati Bajeti ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kwa mwaka wa fedha 2025/2026 yenye makadirio yanayofikia Sh6.8 trilioni ikisomwa kesho, wananchi na wataalamu mbalimbali wameendelea kutoa maoni tofauti kuhusu vipaumbele vinavyopaswa kuzingatiwa.

Bajeti hiyo ni ongezeko la asilimia 31 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka wa fedha uliopita wa 2024/2025 ya Sh5.182 trilioni, ambayo  ilionyesha mwelekeo wa kimkakati katika kukuza uchumi wa buluu, kuimarisha miundombinu na kuhimiza ushirikiano na sekta binafsi.

Kwa mujibu wa taarifa, bajeti ya mwaka wa fedha uliopita wa 2024/2025, ukuaji wa uchumi ulikadiriwa kuwa asilimia 7.2, huku sekta ya utalii ikitarajiwa kuongezeka kwa asilimia 30 kwa wageni wa kimataifa na asilimia 64.5 kwa watalii wa ndani.

Vipaumbele vilijumuisha ujenzi wa miundombinu ya afya, elimu, maji safi, na usafiri pamoja na kutoa ajira mpya 21,808.

Bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026 inayotarajiwa kusomwa kesho Juni 12,2025 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Dk Saada Mkuya Salum, inakadiriwa kufikia Sh6.8 trilioni, ikiwa ni ongezeko la asilimia 31 kutoka mwaka 2024/2025.

Hatua ya kusomwa kwa bajeti hiyo inakuja baada ya kukamilika kwa mjadala na upitishaji wa bajeti za wizara mbalimbali katika Baraza la 10 la Wawakilishi, Mkutano wa 19, ambao ndio mkutano wa mwisho kabla ya baraza hilo kufungwa rasmi katika ngwe ya mwisho ya kipindi cha miaka mitano (2020–2025).

Matarajio ya wananchi, wachumi

Wadau wa uchumi na wananchi wametaja matarajio yao kuelekea bajeti kuu ya SMZ kwa mwaka wa fedha 2025/2026, wakisisitiza umuhimu wa kuboresha mazingira ya biashara, mfumo wa kodi na kuinua uchumi wa mtu mmojammoja.

Mtaalamu wa uchumi na mshauri wa sera, Dk Twahir Mohamed Khalfan amesema bado kuna kazi kubwa ya kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji na kuondoa kodi zinazobana biashara.

“Ili uchumi ukue, lazima kuwe na mifumo bora ya kodi itakayoongeza mapato bila kuwaumiza wananchi au wawekezaji,” amesema.

Amesema Zanzibar ina viwango vya juu vya kodi ikilinganishwa na nchi jirani, hivyo bajeti inapaswa kuelekea kwenye kupanua wigo wa kodi badala ya kuongeza viwango, ili Serikali iweze kuwekeza kwenye sekta kama elimu, afya na barabara.

Aidha, amependekeza sekta binafsi, hususan ya wazawa ishirikishwe kikamilifu katika ujenzi wa uchumi wa nchi.

Amesema makato kama michango ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF)  ya asilimia 21 na bima ya afya asilimia 6, ambayo jumla yake ni asilimia 27 ni mzigo mkubwa kwa sekta binafsi na yanapunguza ari ya kuajiri.

“Sekta binafsi inapaswa kuchangia, lakini asilimia hizi ni kubwa mno tunahitaji mabadiliko,” amesema.

Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (Suza), Faida Abdulla Ali amesema anatarajia bajeti ijikite kwenye mifumo ya kisasa ya ukusanyaji kodi kwa njia ya kidijitali.

“Ni lazima mfumo uwe rafiki kwa mtumiaji ili kuchochea ukusanyaji wa mapato bila kuwa kikwazo kwa walipa kodi,” amesema.

Wote kwa pamoja wanasisitiza kuwa hakuna uchumi unaoweza kustawi kwa kutegemea misaada, hivyo Zanzibar inapaswa kujenga uchumi wake kwa kushirikisha wananchi, sekta binafsi na kuweka mifumo wezeshi ya kodi.

Baadhi ya wataalamu na wananchi wanapendekeza bajeti ijayo izingatie misamaha ya kodi kwa wafanyabiashara wadogo badala ya kuendelea kuwanufaisha wakubwa pekee.

Dk Twahir Khalfan amesema vijana wengi wanaojiajiri hukumbana na changamoto kubwa za kodi na adhabu zisizoendana na uhalisia wa biashara changa.

Mtaalamu wa kodi, Haji Ali Omar amesisitiza kuwa ni muhimu misamaha ilenge bidhaa za vyakula ili kudhibiti mfumuko wa bei, ambao huathiri zaidi wananchi wa kipato cha chini.

“Mfanyabiashara hufidia gharama kwa kupandisha bei, lakini mwananchi wa kawaida ndiye anaumia,” amesema.

Kwa upande wake Mohamed Khamis amesema licha ya kuambiwa uchumi unakua, hali ya maisha haionyeshi mabadiliko kwa mtu mmojammoja, huku Ashura Abubakar Haji akitaka bajeti izingatie usawa wa kijinsia.

Wamependekeza pia kuwepo kwa usawa kati ya Unguja na Pemba, wakisisitiza kuwa bado iko nyuma katika maendeleo.

“Bajeti hii itazame watu wa kawaida, sio tu miradi mikubwa,” amesema Mohamed.

Wawakilishi wa Baraza la Wawakilishi wamependekeza bajeti ya SMZ ijayo izingatie huduma bora kwa wananchi, hususan sekta ya afya, elimu na ajira.

Aza Januar Joseph (nafasi za wanawake) amesema uhaba wa madaktari bado ni changamoto kubwa licha ya uwekezaji kwenye miundombinu ya hospitali, hali inayowalazimu wananchi kukaa foleni muda mrefu.

Mwakilishi wa Pandani, Profesa Omar Fakih Hamad amesisitiza kuwa malaria bado ni tatizo na linahitaji mkakati mpya wa pamoja, si kuachiwa wizara ya afya pekee, huku mwakilishi (nafasi za wanawake), Rukia Omar Ramadhan amependekeza bajeti ya afya iongezwe, hasa kwa huduma za mama na mtoto.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Chumbuni, Miraji Khamis Mussa amehimiza kuboresha masilahi ya walimu, huku mwakilishi wa Mtoni, Hussein Makungu akitaka wajengewe nyumba za gharama nafuu.

Dk Mohamed Ali Suleiman (Mtambwe) ameshauri Serikali iangalie ajira za vijana kwa kujenga viwanda badala ya kutegemea fursa kutoka nje.

Suleiman Makame Ali, mwakilishi wa Ziwani,  amesisitiza umuhimu wa kuwa na mkakati wa maendeleo unaodumu bila kuathiriwa na mabadiliko ya uongozi.

Related Posts