Uchunguzi waibua mapya mwanablogu aliyefariki kituo cha polisi

Nairobi. Uchunguzi wa mwili umebaini kuwa Mwalimu na Mwanablogu wa Kenya, Albert Ojwang aliyefariki akiwa mikononi mwa polisi alipigwa kichwani na kifo chake huenda kilisababishwa na kupigwa.

Daily Nation imeripoti kuwa ripoti hiyo inapingana na madai ya polisi kuwa mwanablogu huyo alijeruhiwa kichwani baada ya kujigonga ukutani akiwa mahabusu.

Kifo chake kimezua ghadhabu kubwa nchini Kenya, huku mashirika ya haki za binadamu yakitaka maofisa wa jeshi la polisi wawajibishwe. Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja awali alisema kuwa maofisa kadhaa waliokuwa kazini wakati wa kifo cha Ojwang “wamesimamishwa kazi.”

Ojwang alikamatwa kufuatia malalamiko yaliyotolewa na Naibu Mkuu wa polisi, aliyemtuhumu kwa kumchafua kwenye mitandao ya kijamii.

“Sababu ya kifo iko wazi kabisa; jeraha la kichwa, kukandamizwa kwa shingo, na majeraha mengine mwilini yanayoashiria kupigwa,” amesema Daktari wa Serikali anayesimamia uchunguzi wa maiti, Bernard Midia.

Polisi bado hawajatoa tamko kuhusu matokeo hayo.

Ojwang, mtayarishaji wa maudhui ya kidijitali aliyekuwa akiandika kwenye mtandao wa X na Facebook kuhusu masuala ya kisiasa na kijamii, alikamatwa mjini Homa Bay, magharibi mwa Kenya, siku ya Ijumaa.

Mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 31, alikamatwa kwa kuchapisha ujumbe kwenye X uliodaiwa kumkosoa Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi, Eliud Lagat.

Baadaye alihamishiwa umbali wa zaidi ya kilomita 350 hadi jijini, Nairobi, na kuwekwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Juni 7, mwaka huu.

Polisi walidai kuwa baadaye alikutwa akiwa amepoteza fahamu kwenye selo, akiwa na majeraha aliyojijeruhi mwenyewe.

Lakini uchunguzi wa maiti uliofanywa na wataalamu wa uchunguzi wa vifo watano na kutoa ripoti ya pamoja, ulionyesha kwamba Ojwang alipata majeraha makubwa kichwa, kukandamizwa kwa shingo na majeraha mengi ya tishu laini mwilini

Dk Midia, aliyeongoza timu ya madaktari hao, amesema kuwa Ojwang hakujigonga ukutani kama polisi walivyodai katika taarifa yao ya Jumapili.

Alisema kama angejigonga mwenyewe, mpangilio wa majeraha ungekuwa tofauti, na damu ingetoka mbele ya kichwa.

“Lakini damu tuliyokuta kwenye ngozi ya kichwa ilikuwa imeenea maeneo tofauti – usoni, sehemu ya kichwa na nyuma ya kichwa,” Dk Midia alieleza kwenye mkutano na waandishi wa habari.

“Pia kulikuwa na majeraha mengi ya tishu laini mwilini kote, kichwa, shingo, mikono ya juu, kiwiliwili na miguu… haya yalikuwa majeraha yaliyosababishwa kutoka nje,” ameongeza.

Majeraha hayo yalioana na ya mtu aliyepigwa kutoka nje, na pia kulikuwa na dalili za mapambano.

Mamlaka Huru ya Usimamizi wa Polisi (IPOA) ya Kenya pia imetoa taarifa na kusema kuwa taarifa za kuwa Ojwang alijiua hazina ukweli wowote.

Shirika hilo limesema matokeo ya awali yanaonyesha kuwa mifumo ya CCTV katika Kituo Kikuu cha Polisi ilivurugwa.

Baba yake Ojwang, Meshack Ojwang, amemuomba Rais William Ruto amsaidie kupata haki kutokana na kifo cha mtoto wake.

“Nisaidie kama mlipa kodi. Maafisa waliomchukua mwanangu waliona nyumba yetu ni ya kawaida na wakaamua sisi hatuna umuhimu,” amesema baba huyo.

Katika taarifa yake, Ruto ameamuru uchunguzi wa haraka, wa wazi, na wa kuaminika ufanyike kuhusiana na tukio hilo.

Hata hivyo, aliwahimiza wananchi kuepuka “hukumu za mapema au hitimisho ambalo linaweza kuhujumu mchakato na matokeo yake.”

Chama cha Watayarishaji wa Maudhui ya Kidijitali cha Kenya kimetuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Ojwang, kwa kuandika:

“Albert hakuwa tu mtayarishaji wa maudhui – alikuwa sauti ya vijana, ishara ya uvumilivu, na mfano wa ndoto na matumaini ya kizazi kinachotumia majukwaa ya kidijitali kuleta mabadiliko. Urithi wake hautanyamazishwa.”

Rais wa Chama cha Wanasheria wa Kenya (LSK), Faith Odhiambo amesema ripoti ya uchunguzi wa maiti meonyesha wazi kuwa Ojwang  huenda aliteswa na “kuuawa kikatil akiwa mikononi mwa polisi.

“Tutaendelea kuweka presha hadi kila afisa aliyehusika awajibishwe kibinafsi. Hatutakubali visingizio zaidi,” alisema Odhiambo.

Kiongozi mkongwe wa upinzani Raila Odinga amelaani kifo cha kutisha cha Ojwang, akisema kuwa kinaongezwa kwenye orodha ndefu ya “Wakenya vijana na wasio na hatia ambao maisha yao yamekatishwa mapema mno, kwa hali za kikatili na zisizo na maana, mikononi mwa polisi.”

Msemaji wa Polisi, Michael Muchiri ameieleza BBC kuwa hii inamaanisha maofisa hao hawawezi kutekeleza majukumu yao na watapokea nusu ya mshahara, wakisubiri matokeo ya uchunguzi.

ashirika ya haki za binadamu yanataka hatua zaidi zichukuliwe, yakisema kuwa kifo cha mwanablogu huyo huenda ni jaribio la kuwanyamazisha watumiaji wa mitandao kupitia vitisho na hofu.

Related Posts