Chaumma yawaweka kati CCM, Chadema

Nyasa/Same. Viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na wale wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ‘wamevutana’ juu ya baadhi ya makada wa Chadema kutimkia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma).

Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira amedai mgogoro uliopo ndani ya Chadema na wanachama wake ndiyo uliosababisha wenzao kutimkia Chaumma. Makamu Mwenyekiti wa Chadema- Bara, John Heche na Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika wamejibu hoja hizo.

Heche alipotafutwa na Mwananchi kuzungumzia kauli ya Wasira, alimkataa kiaina akisema:“Hana muda kumjibu Wasira.”

“Kaka sina muda wa kumjibu Wasira,” amesema Heche kwa ufupi alipotafutwa na Mwananchi kwa simu.

Naye Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika amemjibu Wasira akidai:”Suala la Chaumma ni mkakati wa mfumo wa Serikali ya CCM ulioratibiwa kwa usaliti wa wachache.”

“No Reforms No Election sio msimamo uliotokana na viongozi wabinafsi kama anavyodai bali ni msimamo uliotokana na matakwa ya umma na ukapitishwa na vikao vya juu vya chama ikiwemo mkutano mkuu.

“Hili ni kutokana na hali halisi ya hujuma za CCM na Serikali kwenye uchaguzi kutokana na kutokuwepo na mifumo huru ya kikatiba, kisheria na kiutendaji katika nchi,” amejibu Mnyika.

Wasira ameitoa kauli yake hiyo leo Jumatano, Juni 11, 2025, wakati akizungumza na wananchi na wanachama wa CCM Wilaya ya Nyasa, mkoani Ruvuma, kupitia mkutano wa ndani wa chama hicho.

Wasira yupo mkoani Ruvuma kwa ziara ya siku nne na aliwasili mjini Songea Juni 9, na atahitimisha ziara yake mkoani hapa Juni 13.

Wasira amesema Chadema haipaswi kutafuta mchawi, bali yenyewe ndiyo mchawi kutokana na kunyima wanachama wake fursa ya kugombea uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu.

Akichambua kauli yake, Wasira amesema Chadema imekuwa na kaulimbiu nyingi ikiwemo No reforms, no election (Hakuna mabadiliko, hakuna uchaguzi) na No hate, No fear (Hakuna chuki, Hakuna hofu) lakini walipofanya uchaguzi ulionekana kujawa na chuki.

“Walipofanya mikutano yao ilijawa na chuki na walipomaliza chama kikasambaratika, kila mtu akachukua virago vyake. Freeman Mbowe, Tundu Lissu, Mwenyekiti wa sasa, akachukua virago vyake, sasa hawapo pamoja na ndiyo wamesababisha kupatikana kwa chama kinaitwa Chaumma (chama cha ubwabwa),” ameongeza.

Tangu kumalizika kwa uchaguzi wa Chadema Januari 21, 2025 kwa Lissu kuwa mwenyekiti akihitimisha uongozi wa Mbowe wa miaka 21, chama hicho kimekuwa katika msuguano wa chini kwa chini wa wenyewe kwa wenyewe.

Wasira amesema Chaumma sasa kinaongozwa na waliokuwa wanachama wa Chadema na Mwenyekiti wa Chaumma Taifa, Hashim Rungwe, anafurahia hali ya chama hicho.

“Wanachama wao wanawaambia mturuhusu tukagombee ubunge, wao wanasema mna uchu wa madaraka na wanaosema mna uchu wa madaraka ni vijana wadogowadogo, Tundu Lissu ameshakuwa mbunge miaka 10.

“Pia Godbless Lema amekuwa mbunge miaka 10 wakati wao wanagombea hawakuwa na uchu wa madaraka, hawa watu ni wabinafsi na ndiyo wameifanya chama kimesambaratika, kwa hiyo watafute mganga wa kugangua chama chao,” amesema.

Chaumma ilianzishwa na Rungwe na wenzake mwaka 2012 na ikapata usajili wa kudumu mwaka 2013. Imekuwa ikiendesha siasa zake kwa kusuasua hadi sasa ambapo waliokuwa viongozi na wanachama wa Chadema walipoamua kujiunga na Chaumma.

Kwa sasa, Chaumma inaendelea na mikutano ya operesheni ya C4C mkoani Tabora ikitokea Mwanza na Kigoma.

Mbali na kauli hiyo, Wasira amewananga wanaosema Rais Samia Suluhu Hassan ni dikteta, akihoji dikteta anawezaje kuruhusu mikutano ya hadhara.

“Sasa wanasema Rais Samia ni dikteta. Sasa dikteta anaweza kuruhusu watu kuandamana na Polisi kuwalinda? Labda kama hujui maana ya udikteta, tukutafutie maana yake ni nini ukajifunze,” amesema.

Hatuna furaha mgogoro wa Chadema

Kwa upande wake, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla, akihutubia mkutano wa hadhara Kata ya Ndungu, Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, amesema CCM haina furaha na mgogoro wa ndani ya Chadema, akikiitaka chama hicho kumaliza haraka mzozo ili kuwe na utulivu wa kisiasa nchini.

Makalla amesema hali inayoendelea Chadema inadhihirisha udhaifu mkubwa wa uongozi wa chama hicho, akitoa wito kwa viongozi wa chama hicho kusuluhisha tofauti zao kwa njia ya ndani bila kuhusisha dola au kuhujumiana.

“Wamepelekana mahakamani wao kwa wao, hakuna Serikali, hakuna CCM, hata sisi hatufurahishwi na mgogoro huo ushauri wetu ni wakae wayamalize wenyewe,” amesema Makalla.

Kauli hiyo imekuja kufuatia uamuzi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, kuzuia Chadema kujihusisha na shughuli za kisiasa kwa muda wa hadi kesi ya msingi iliyofunguliwa na baadhi ya viongozi wake itakaposikilizwa, walalamikaji ni Said Issa Mohamed, Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chadema Zanzibar.

Makalla aliwataka viongozi wa Chadema kuacha kuilaumu Serikali au Mahakama, akisisitiza kuwa kesi hiyo imefunguliwa na wanachama wao wenyewe.

“Tungependa ushindani wa kisiasa, lakini hali ya Chadema sasa ni dhaifu sana waache visingizio, tuheshimu mihimili ya dola,” ameongeza.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni, akizungumzia miradi ya maendeleo, amesema wilaya hiyo imepokea zaidi ya Sh444.4 bilioni katika miaka minne kwa ajili ya miradi ya barabara, afya, elimu na nishati.

“Tuna vituo vinne vya afya kutoka kituo kimoja, mradi wa kupooza umeme unaogharimu Sh3.5 bilioni  unaendelea na utamaliza tatizo la umeme wilayani hapa,” amesema Mgeni.

Katika hatua nyingine, Wasira amesema chama hicho kinaendelea kuimarisha umoja wa wananchi na hakitakubali kamwe chokochoko zinazolenga kuibua mgawanyiko wa watu.

Amesema umoja wa Tanzania ndio chachu ya amani, wapo watu wanatamani wananchi wafarakane jambo ambalo haliwezi kutokea.

Amesema hayo katika mkutano wake wa ndani na  wananchi na wanachama wa CCM Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma.

“Kuna watu wanaopenda tufarakane, tugombane na wenye mawazo hayo wengine wapo nje ya nchi, wenyewe sio Watanzania,  ili wafanikiwe wanawatumia Watanzania kama vibaraka wao, nimekuja kuwambia amani ni tunu ya Taifa.

Amani na umoja wetu ni tunu za Taifa, Watanzania wajihadhari na wenye nia mbaya, wanataka kutugawa na kupenda kutuona tukigombana wenyewe kwa wenyewe,” amesema.

Kuhusu uhuru uliopo nchini, Wasira  amesema ndio umesababisha watu kutoa maoni, uwepo wa vyama vya siasa akisisitiza uhuru unaendana na sheria.

Amesema Tanzania ina watu wengi na haiwezekani kila mtu kujifanyia jambo lake.

Related Posts