Dodoma. Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha marekebisho ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Februari 2023, likilenga kuboresha uwajibikaji na kuongeza ufanisi wa shughuli za kibunge.
Miongoni mwa marekebisho hayo ni kuwalazimu mawaziri kuwasilisha taarifa za utekelezaji wa maazimio ya Bunge yanayotokana na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mbele ya Kamati za PAC na LAAC.
Aidha, utaratibu wa kutambulisha wageni binafsi bungeni umeondolewa ili kuokoa muda wa vikao, huku kanuni mpya zikianzisha mchakato wa wabunge kuapa uadilifu, kurekodi kura za “abstain” na kutambua rasmi muda na utaratibu wa kusoma Bajeti Kuu ya Serikali.
Mapendekezo hayo yamewasilishwa na mwenyekiti Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kanuni, Mussa Zungu leo Juni 11, 2025.

Mbunge wa Viti Maalumu Halima Mdee.
Zungu amesema kuanzia Bunge lijalo, wabunge watakuwa wanatoa ahadi ya uadilifu katika kila kikao cha kwanza cha mkutano wa Bunge, ambapo kila mbunge ataahidi kuwa mtiifu na mwaminifu kwa nchi yake na kufanya kazi zake kwa uadilifu.
Kwa upande wa upigaji kura, wakati wa kupitisha Bajeti ya Serikali, marekebisho hayo yatawezesha kutambua utaratibu wa kuweka kumbukumbu ya kura za wabunge wasiokuwa na upande, wanaotumia neno abstain kupiga kura zao.
Vilevile, chini ya marekebisho hayo kanuni inatambua saa 10.00 jioni kama muda rasmi wa kusoma Bajeti ya Serikali, ambayo imekuwa ikisomwa muda huo bila kuwemo kwenye kanuni.
Marekebisho hayo pia yameweka kwenye kanuni mkutano unaoitishwa na Spika kujadiliana na wabunge kuhusu masuala ya kibunge.
Na kurasimisha taarifa za kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa na Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuwasilishwa katika mkutano wa Oktoba-Novemba.
Kuhusu utambulisho wa wageni bungeni, kamati imependekeza na Bunge likaridhia kufanya marekebisho ya kanuni ya 161 kwa lengo la kuokoa muda kwa kutambulisha wageni mahususi wa kitaifa na kimataifa waliopo katika ukumbi wa Bunge pamoja na wale tu waliotoa mchango wa kitaifa unaohitaji kuenziwa.
Vilevile, Zungu amesema kamati imebaini kuwepo kwa changamoto ya matumizi yasiyo sahihi ya bendera ya Bunge yanayosababisha kushusha hadhi na heshima ya mbunge.
Hivyo, kanuni imeweka masharti ya kusimamia upeperushaji wa bendera katika gari la mbunge.
“Mapendekezo hayo ni ya kumzuia mbunge kupeperusha bendera akiwa anaendesha gari lake, mbunge kutopeperusha bendera zaidi ya moja kwa wakati mmoja na vilevile kuelekeza kuwa mbunge anapaswa kupeperusha bendera akiwa ameketi upande wa kushoto wa gari lake likiwa linaendeshwa na mtu mwingine,” amesema.
Pia imewekwa kanuni mahsusi inayoeleza utaratibu wa Bunge kuthibitisha uteuzi wa makamu wa Rais pale inapotokea ameteuliwa baada ya kipindi cha uchaguzi kupitia Ibara ya 50(4) ya Katiba. Utaratibu huo umetokana na uzoefu wa Bunge kuendesha mchakato kama huo.
Kanuni pia zimegusa mavazi bungeni, kwa kuongeza kilemba cha kadri au mtandio kuwa sehemu ya vazi rasmi kwa katibu au katibu msaidizi mwanamke, ambaye masharti ya imani yanamtaka kuvaa vazi hilo.
Amesema katika kusimamia mavazi rasmi ya wabunge, imebainika kuwa baadhi ya wanaoingia maeneo ya Bunge huvaa sare zinazoshiria au kuzoeleka kuvaliwa na wafuasi au mashabiki wa vyama vya siasa kwa alama, nembo au maandishi ambavyo hutafsiriwa kwa jina, alama, msemo au nembo ya chama.
“Inapendekeza kuweka Kanuni inayokataza mavazi hayo ili kudumisha dhana ya Bunge kuendesha shughuli zake kwa uhuru na umoja bila kujali itikadi za kisiasa. Aidha, kanuni kuhusu mavazi imeboreshwa ili kuweka usimamizi madhubuti wa mavazi bungeni,” amesema Zungu.
Baada ya mjadala wa kanuni hizo, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson ameeleza kupokea mapendekezo ya nyongeza ya kanuni yanayoilazimu Serikali kupeleka utekelezaji wa maazimio ya Bunge yatakayotokana na taarifa zilizowasilishwa na Bunge kwenye Bunge la Januari na Februari na Kamati mbili.
Kamati hizo ni ya Hesabu za Serikali (PAC) na Serikali za Mitaa (LAAC) ambazo nazo zitawasilisha taarifa zake bungeni kila mkutano wa Bunge.

Mbunge wa Nzega Vijijini, Hamisi Kigwangalla
“Isipokuwa katika kila mkutano wa Bunge, kamati hizo mbili zitapewa nafasi ya kutoa taarifa juu ya utekelezaji wa maazimio ya Bunge,” amesema.
Akichangia mjadala huo, Mbunge wa Iramba Mashariki (CCM) Francis Mtinga amesema suala la kutambulisha wageni ni nafasi nzuri ambayo Bunge limekuwa likiitumia na kuwa wao pia wamelikuta.
“Wananchi wanapokuja hapa Mheshimiwa Spika halafu wasitambuliwe na wenzao kule kwenye majimbo yetu wakawaona kwamba kweli wamefika bungeni na kuwapelekea salamu?” amesema.
Ameomba Dk Tulia yeye pamoja na kamati yake warudi kuliangalia upya na suala la wageni libaki kama lilivyokuwa kwa sababu ni suala zuri katika kuwafanya wabunge na wananchi waweze kushirikiana katika bunge hili.
Hata hivyo, Mbunge wa Viti Maalumu, Anatropia Theonest ameungana na kamati hiyo kuwa suala la kutambulisha wageni limekuwa likia muda kwa kiwango kikubwa.
“Kwa hiyo mimi nilikuwa nashauri mheshimiwa spika utaratibu ambao umependekezwa unafaa kabisa, watu kutambuliwa kwa kusoma kwamba kuna wageni fulani basi. Watu tumejifunza, muda mwingine anatamani kuja kuonyesha kwamba ‘mimi ninatoka kampuni fulani’,” amesema.
Amesema hatua hiyo inaonyesha kama promosheni na hivyo akapendekeza kuwa utambulisho ufanyike kwa kundi lenye kwenda bungeni kwa ajili ya shughuli maalumu.
Kwa upande wake, Mbunge wa Makete (CCM), Festo Sanga amesema anatamani ndani ya ukumbi Bunge kuwe na mpangilio wa ukaaji ambapo mawaziri wakae upande mmoja ilio wakati wabunge wanachangia waangalie kama Serikali yao ipo au haipo ndani.
“Ilikuwa wakati mwingine wanachangamana hapa wabunge na Serikali kunakuwa na shida. Kwa hiyo Sitting arrangement ndani wabunge tungekuwa na upande wetu na hawa wenzetu wa Serikali wabaki hapa, ili nao wajue umuhimu au kukaa bungeni,” amesema.
Mbunge wa Sumve (CCM) Kasalali Mageni amesema mavazi rasmi bungeni mara nyingi yamekuwa ni ya kimagharibi, hasa kwa upande wa wanaume – akimaanisha suti.
“Mimi binafsi ungeniuliza hivi nilivyojipiga na tai napata taabu sana, lakini ni humu tumeambiwa mavazi rasmi na amiri. Mheshimiwa spika mavazi nadhifu tunayo masharti yetu ya Kiafrika mazuri, tunaweza kuvaa,” amesema.
Mageni amesema kuna makabila yanaheshimika kama wa Wamasai wana mavazi yao ya heshima, yanaweza kuvaa lakini anaona kama kuna ukoloni Fulani kwenye suala hilo.
“Ili twende pia na Bunge la Kitanzania, Bunge la Kiafrika na Uafrika wetu ni muhimu sana na sisi pia tunatakiwa tuuze mavazi yetu. Ifike wakati hata huko Ulaya na wao watamani kuvaa nadhifu kama tunavyovaa sisi katika makabila yetu na tamaduni zetu,” amesema.
Mbunge wa Viti Maalumu Halima Mdee amesema kwa sasa wanaamini kwa ajili ya kutengeneza uwajibikaji ni muhimu kukawa na kanuni za kuwabana mawaziri kwenye utekelezaji wa maazimio ya Bunge.
“Ili kutoa wajibu kwa Serikali au kila baada ya miezi mitatu au kila baada ya miezi sita baada ya taarifa kusomwa ya maazimio ya Bunge juu ya utekelezaji wa taarifa za CAG watuambie wametekeleza nini?”amesema.
Amesema kwa taarifa za CAG kuna mapendekezo tokea mwaka 2019 hajatekelezwa, 2020 hayajatekelezwa lakini kwa sababu watu wanajua kwamba hawana kipindi ambacho wanatakiwa walieleze Bunge utekelezaji, wanasababisha changamoto hiyo.
“Kila ambacho tumewaambia wakafanyie marekebisho na wamefanyia kiasi gani hatufahamu, sasa tukitengeneza hii ratiba maanake waziri aliyepewa dhamana kuwasimamia atutumia nguvu kuhakikisha yamefanyiwa kazi,” amesema.
“Hakuna kuwajibishana, sasa mimi nilidhani lile ni kosa kubwa sana…Kama waziri umekuwa na dhamana unashindwa kusimamia watu wako tule kichwa, kama mkurugenzi ameshindwa kusimamia naye aliwe kichwa,” amesema.
Kwa upande wake Mbunge wa Kinondoni (CCM) Abbas Tarimba ameshauri wabunge wapewe namba maalumu za magari kwa kuwa kuna maeneo mengine wabunge hawawezi kupeperusha bendera za Bunge.
“Sasa inatokea wakati kuna misafara ya kitaifa, hata misafara ya kimkoa ambapo tunatakiwa tufike maeneo fulani kwa uharaka au saa nyingine tutakuwepo katika ile misafara lakini magari yetu kwa kuwa hayana utambulisho wowote ule yanaleta changamoto,” amesema.
Ametoa mfano wabunge wanaotoka Dar es Salaam magari yao hayana utambulisho wa aina yoyote na wanapojikuta katika msafara gari lake liko nyuma anashindwa kwenda na ratiba ya ziara.
“Ukiitwa mbunge njoo utoe salaam ndio kwanza unatafuta sehemu ya kuegesha, sasa nilikuwa nafikiria kama kanuni ya kupeperusha bendera inaweza ikaendelea,”amesema.
“Nikafikiria kwamba labda tunaweza tukawa na namba plates (za magari) kwamba mfano mtu unachagua gari lako moja ambalo litatumika kwenye shughuli zako za kikazi likawa na namba plate ambayo inaashiria kwamba gari hili ni la mbunge,” amesema.
Amesema kwa kufanya hivyo kutamwezesha kumsaidia pale mahali ambapo anatakiwa afike haraka na barabarani anapokutana na trafiki kutambulika badala ya kujieleza.
Mbunge wa Geita Vijijini (CCM) Joseph Musukuma ameshauri kanuni imtambue mwenza wa mbunge kama mtu mashuhuri kwa sababu sasa mbunge anapewa hadhi tofauti na mwenza wake wanapofika katika maeneo yenye hadhi hiyo.
“Mheshimiwa Spika, sisi tumepewa heshima ya kupita VIP (vyumba vya watu mashuhuri) lakini nataka kujiuliza ukienda pale VIP ukishuka kwenye gari kama huna hela inabidi mtawanyike, mwanamke apite huku na wewe upite huku,”amesema.
“Na sisi ili upate kura lazima kuwa na mume nyuma au kuna mke nyuma yake, sasa sioni kama wenzetu walitengeneza utaratibu mzuri na sijui kwa nini, nashauri ile heshima ya VIP hasa kwenye hizi sehemu ni mbaya sana kumtenganisha mtu na mwenza wake,” amesema.
Amesema wawili hao wanaambiwa kuwa wamekuwa mwili mmoja lakini wakifika VIP wanakuwa miili miwili.