Polisi yaomba radhi kwa kudanganya taarifa za kifo cha mwanablogu

Nairobi. Mkuu wa Polisi nchini Kenya (IGP), Douglas Kanja amewaomba radhi wananchi wa Kenya kwa taarifa ya uongo iliyotolewa na Idara ya Kitalfa ya Polisi nchini humo (NPS) kuhusu kifo cha mwalimu na mwanablogu, Albert Ojwang.

Ojwang alifariki akiwa katika kituo cha polisi jijini Nairobi nchini humo.
Awali ripoti hiyo ya NPS ilisema Ojwang alijiua. Tayari Rais William Ruto ameviagiza vyombo vya usalama nchini humo kufanya uchunguzi wa kina wa mkasa huo.
Taifa Leo imeripoti leo Jumatano Juni 11, 2025, kuwa tukio hili la kusikitisha limeacha simanzi kubwa na kuzua mjadala mkubwa katika majukwaa nchini humo.
Mapema wiki hii, IG Kanja alidai kuwa Ojwang alifariki kwa kujitoa uhai baada ya kujigonga kichwa kwenye kuta za mahabusu ya polisi alimokuwa, madai ambayo yalizua taharuki kwa umma, ambao uliishutumu polisi kwa kujaribu kuficha ukweli wa chanzo kifo cha Ojwang.

Katika kikao cha Baraza la Seneti leo, Kanja amesisitiza kwamba asingeweza kutoa tamko lolote hadi Mamlaka Huru ya Kusimamia Polisi (IPOA) ikamilishe uchunguzi huo.

Pia ameapa kuwachukulia hatua maofisa waliompatia ripoti hiyo akisema taratibu za kinidhamu zitaambatana na taratibu za kawaida za uendeshaji wa mashauri ya aina hiyo.

“Ikiwa katika uchunguzi unaoendelea na IPOA, tutajua ukweli, maofisa waliotoa ripoti ya awali watachukuliwa hatua za kinidhamu,” amesema Kanja.

“Kutokana na kile tulichosikia hapa, tutaendelea na kuchukua hatua zinazohitajika dhidi ya ofisa aliyetupa taarifa siku hiyo.”

Hata hivyo maseneta hao walipinga matamshi ya Kanja na kudokeza kuwa IPOA imefutilia mbali kujiua kufuatia kutolewa kwa matokeo ya uchunguzi wa mwili wa  mwanablogu huyo na daktari aliyemfanyia uchunguzi na ilibainika kuwa alifariki kutokana na majeraha makubwa aliyoyapata.

Huku akibananishwa na wabunge kwa maswali magumu Kanja ameomba msamaha kwa umma huku akieleza kusikitishwa na ripoti ya awali.

“Ninaomba msamaha kwa niaba ya Huduma ya polisi ya kitaifa NPS kwa sababu ya habari hiyo,” Kanja amesema huku akishangiliwa na maseneta.

Kundi la haki za binadamu limewasilisha ombi mahakamani likitaka kuanzisha kesi ya kibinafsi dhidi ya Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi, Eliud Kipkoech Lagat kuhusu kifo cha mwanablogu huyo.

Kulingana na ombi hilo, mazingira yanayozunguka kifo cha mwanablogu huyo kinachodaiwa kutokea baada ya kukamatwa, kuzuiliwa na kuteswa ni mabaya kuweza kushughulikiwa tu kupitia taratibu za ndani za kinidhamu.

Walalamikaji hao ambao ni Julius Ogogoh, Khalef Khalef, Francis Auma, na Peter Agor wanahoji kuwa mamlaka za uchunguzi na uendeshaji wa mashtaka zimeshindwa kuchukua hatua ifaayo katika suala hilo.

Kanja ambaye alikuwa bungeni leo amesema naibu wake (DIG), Lagat ndiye anayelalamikiwa kuhusika na kukamatwa kwa Ojwang’, kwani alidai kuwa marehemu alikuwa ametoa matamshi ya kashfa dhidi yake kwenye jukwaa lake la X.

Kanja amewaambia Maseneta  kwamba uchunguzi ulianza wakati machapisho ya mtandaoni yalipodai naibu wake (Lagat) alihusika katika ufisadi ndani ya Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS).

“Chapisho hilo lilidai kuwa alihusika katika ufisadi ndani ya NPS. Hasa, habari iliyochapishwa ilidai kuwa Lagat amewaweka kimkakati maofisa wake wa kuaminiwa kusimamia dawati la vitabu vya mamlaka ya upelelezi ya (DCI) na mabadiliko ya trafiki ili kudhibiti njia zote mbili za mapato na ujasusi,” Kanja amelieleza bunge hilo.

Lagat yuko kwenye hatihati ya kushikiliwa muda wowote na kuchukuliwa hatua za kisheria huku uchunguzi wa kina kuhusu kesi hiyo ukianzishwa wakati huu ambao wanaharakati wa haki za kiraia na Wakenya wanashinikiza ajiuzulu, kwa madai kwamba alihusika na kifo cha Ojwang.

Related Posts