Chaumma yakazia sera ya kuwaongoza walioshiba

Tabora. Chama Cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), kimesema kikiingia madarakani kitaboresha sera ya kilimo ili wananchi wafanye shughuli hizo kwa tija na wapate chakula cha kutosheleza milo mitatu kwa siku.

Hatua hiyo inakwenda Sambamba na sera ya ubwabwa ya chama hicho ya kuwa na Taifa lenye watu walioshiba ambao wataweza kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Mwenyekiti wa Chaumma, Hashimu Rungwe, maarufu Mzee wa Ubwabwa mara kadhaa amenukuliwa akisema mtu mwenye shibe hawezi kudanganywa na anaweza kufanya mambo kwa ufanisi na kuchangia maendeleo ya jamii na Taifa.

Akihutubia mkutano wa hadhara mjini Tabora leo Jumatano, Juni 11, 2025, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Chaumma, John Mrema amesema uhakika wa chakula siyo tu utajenga jamii yenye uwezo wa kufanya kazi na kuzalisha, bali pia utamaliza tatizo la utapiamlo kwa watoto.

Amesema Tanzania imejaaliwa kuwa na ardhi yenye rutuba, misimu miwili ya mvua na idadi ya watu, hivyo inafaa kuongoza mataifa yote ya ukanda wa Afrika Mashariki na kati kwa uzalishaji wa chakula kwa kuboresha sera ya kilimo kuwezesha wananchi kulima kwa tija.

Mrema amesema nchi imejaliwa kuwa na mabonde yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji yenye kuwezesha kilimo cha mpunga kuwezesha Taifa kuzalisha mchele wa kutosha.

“Ukosefu wa chakula husababisha utapiamlo, watoto wenye utapiamlo hawawezi kukua vizuri, na hata wakikua hawataweza kufikiri wala kufanya kazi sawasawa,” amesema.

“Chaumma ikiingia madarakani itafuta kodi zote za VAT za asilimia 18 kwenye bidhaa za chakula ili bei ishuke kuwezesha wananchi kununua chakula na mafuta,” amesema.

Mrema amefafanua Taifa lenye watu wasiomudu kupata milo angalau mitatu kwa siku huzalisha jamii yenye udumavu na isiyoweza kuzalisha.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa chama hicho, Salum Mwalimu amesema yupo tayari kuitwa majina yote iwe msaliti lakini hawezi kurudi nyuma katika kupigania haki za Watanzania hadi aingie kaburini.

“Kikubwa wananchi tunawaomba kipokeeni chama cha Chaumma, tuna dhamira ya kweli katika kuwapigania wananchi, tutasimamisha wagombea katika nafasi zote za udiwani, ubunge na urais,” amesema.

“Wakati wote tumekuwa tukipeana moyo, hatuwezi kusaliti mapambano kwani itakuwa changamoto kubwa na kuwasaliti waliopata vilema na waliofilisika kwa kupigania mageuzi,” amesema.

Amesema kwa miaka zaidi ya 30 wamekuwa wakiwashauri wananchi kuachana na msimamo wa sera ya CCM kwa kuwa hawajasaidia wananchi kwa kipindi chote walichokuwa madarakani.

“Utofauti wa mtazamo ni sababu ya kuongezeka kwa vyama vya upinzani,” amesema.

Amesema safari ya mabadiliko haijawahi kuwa nyepesi na kazi hiyo haipaswi kukoma wala kutegemea hisani kutoka chama fulani.

“Chaumma tunaamini katika safari hii, Watanzania twendeni kwenye uchaguzi kama kufa tukafe wote ili tusiwasaliti waliopata vilema au waliofilisika kwa sababu ya kudai mageuzi,” amesema.

Amesema miaka mitano ya kuiacha CCM peke yake bungeni kuna madhara makubwa na maisha magumu wanayopitia Watanzania yanasababishwa na kukosa usemaji.

Related Posts