Morogoro. Watu tisa wamefariki dunia papo hapo na wengine 44 kujeruhiwa baada ya basi la Kampuni ya Hai kugongana uso kwa uso na lori lililokuwa limebeba shehena ya sukari katika eneo la Lugono Melala, barabara kuu ya Morogoro–Iringa.
Ajali hiyo imetokea wakati magari hayo mawili yalipogongana kwa nguvu, na kusababisha maafa hayo makubwa.
Kwa mujibu wa Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, Dk Daniel Nkungu, ajali hiyo imetokea alfajiri ya leo Alhamisi Juni 12, 2025 na hospitali imepokea miili ya marehemu tisa.
Ameeleza kuwa kati ya miili hiyo, mitano ni ya wanaume na minne ni ya wanawake.
Aidha, Dk Nkungu amesema hospitali hiyo imepokea majeruhi 44, ambapo kati yao watu wazima ni 37 na watoto ni saba.
Dk Nkungu amebainisha kuwa majeruhi wengi wamepata mivunjiko na wanaendelea kupatiwa matibabu ya haraka chini ya uangalizi wa karibu wa wataalamu wa afya.
Amesema kuwa miili minne kati ya tisa tayari imetambuliwa na ndugu wa marehemu, ambapo utambuzi huo umewezekana kupitia vitambulisho walivyokuwa navyo marehemu hao.
Dk Nkungu amesema miili mingine bado haijatambuliwa na imehifadhiwa katika chumba cha maiti Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, ikisubiri utambuzi na taratibu zaidi kutoka kwa familia husika.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amesema kwamba atatoa taarifa rasmi kwa vyombo vya habari muda si mrefu, kuhusu chanzo cha ajali hiyo na hatua zinazochukuliwa.