Matarajio Zanzibar bajeti ya Serikali leo

Wananchi na wataalamu mbalimbali visiwani humu wamekuwa na maoni tofauti kuhusu bajeti ya Serikali inayotarajiwa wakitaka ijikite katika kuinua uchumi wa mwananchi mmojammoja, kugusia msamaha wa kodi wa biashara changa na ushirikishwaji wa sekta binafsi..

Mtaalamu wa masuala ya uchumi na mshauri binafsi katika sera na uchumi, Dk Twahir Mohamed Khalfan amesema bado kuna kazi ya kufanya kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na kuondoa kodi ambazo zinaonekana kuwa mwiba.

Amesema ili Zanzibar ifike katika uchumi wa kati unaoendelea lazima kipato cha wananchi mmojammoja kikue na ili kipato kikue lazima biashara na uchumi ukue na ili uchumi ukue lazima kuwepo na mifumo Rafiki na wezeshi ya kulipa kodi.

“Ili kufika huko mapato ya kodi lazima yaongezeke na Zanzibar katika Nchi za Afrika za Afrika Mashariki mapato ya kodi yapo juu ikilinganishwa na nchi zingine,” amesema

Amesema anatamani bajeti ije na mipango ya kupanua wigo wa kodi ili Serikali ipate kodi nyingi zaidi na iweze kuwekeza katika sekta za kijamii kama elimu na barabara na hili ni jambo la msingi na muhimu sana.

Khalfan anasema hakuna nchi inajengwa kwa uchumi tegemezi, hivyo Zanzibar kama nchi lazima ipanue mipango yake katika kulipa kodi na kupunguza utegemezi kwa wafadhili.

Amesema kodi ya Zanzibar sio kubwa lakini haipo sawa, halafu inapofanyika tathmini lazima ieleweke vyema isipoeleweka inaleta changamoto kubwa kwa uwekezaji

Amesema kuna makato ambayo yanakuwa makubwa na yanaleta changamoto hivyo inatatiza biashara.

Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (Suza) shule ya biashara Faida Abdulla Ali amesema wanatarajia kuona kuna mipango ya makusanyo ya kodi kwa njia ya kidijitali badala ya kutumia karatasi.

“Ingawa tayari tupo kwenye mifumo lakini inaturejesha nyuma, hivyo mimi binafsi natarajia kuona ni bajeti ambayo imejikita kwenye mifumo imara ili kuwa na uchumi bora maana kupitia mifumo hiyo tunapata makusanyo,” amesema

Hata hivyo amesema lazima mifumo hiyo iwe rahisi ili wananchi wanaoitumia waone kuwa ni Rafiki kwao badala ya kugeuka kuwa changamoto na kikwazo.

Aidha mtaalamu huyo amesema kumekuwapo na misamaha ya kodi kwa biashara kubwa lakini ifike wakati sasa misamaha ya kodi iwalenge wafanyabiashara wadogo pia kwani kila siku inasema wajiajri.

“Kuna vijana wengi wanatoka kwenye vyuo wengine wapo mtaani, Serikali inasema inabidi tujiajiri kukuza uchumi wetu maana haiwezi kuajiri wote lakini bado hakujawa na urafiki wa kodi, hivyo tunataka tuone misamaha ikiwagusa wafanyabiashara wadogo kabisa,” amesema

Mtaalamu mwingine katika masuala ya kodi Haji Ali Omar anasema wanategemea kuweka nafuu katika kudhibiti mfumko wa bei maana unaongeza gharama za maisha kwa wananchi

Naye amezungumzia misamaha ya kodi akisema wanatarajia kuona ikijikita katika bidhaa za vyakula ili kupunguza bidhaa hizo kupanda maana zinapopanda anayeumia ni mwananchi wa kawaida.

“Kwa kawaida mfanyabiashara hana hasara kwa sababu yeye anachokifanya anafidishia gharama zake kwa kuongeza bei hivyo anayekwenda kuumia ni mwananchi wa kawaida,” amesema

Naye Mohamed Khamis alisema wanatamani kuona bajeti hii ikijielekeza namna ambavyo mzunguko wa fedha utakuwa kwa watu kwani licha ya kuambiwa uchumi unakuwa lakini bado maisha yanaendelea kuwa magumu.

“Tumeshuhudia miradi mingi imeshatekelezwa kwa kiwango cha kutosha hivyo nadhani hii bajeti sasa ijikite kuinua maisha ya watu, hali ya uchumi kwa mwananchi mmojamoja bado ni ngumu sana,” amesema Mohamed ambaye ni mkazi wa Zanzibar.

Amesema hata mikopo inayotajwa kutolewa kwa wananchi lakini haijawafikia wananchi wengi hivyo hata uwezeshaji wa wananchi unakuwa mdogo katika kukwamua.

Kadhalika, amesema katika kipindi hiki ni vyema Pemba ikaangaliwa kwa jicho la kipekee maana bado kuna tofauti kubwa kati ya Unguja na Pemba hivyo ifike wakati sasa visiwa hivyo viwe na sura inayofanana.

Mwananchi mwingine Ashura Abubakar Haji yeye anasema anatamani kuona bajeti ikizingatia usawa wa kijinsia ili kuwapa nguvu wanawake kwani wamekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo lakini katika vipaumbele bado hawajazingatiwa. “Tunataka kuona masuala ya jinsia yanatawala katika bajeti hii, hatua hii itawahamasisha wanawake wengi kushiriki katika shughuli za maendeleo,” amesema.

Mbali na mtazamo huo amesema inabidi kuwaangalia wananchi wa hali ya chini kwani bado maisha yameendelea kuwa magumu pamoja kuambiwa kuwa uchumi umekua.

Related Posts