Bujumbura. Chama tawala cha muda mrefu nchini Burundi, National Council for the Defense of Democracy–Forces for the Defense of Democracy (CNDD-FDD), kimeibuka mshindi wa viti vyote vya Bunge.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (CENI) ilitangaza matokeo hayo jana Jumatano, Juni 11, 2025, ambapo mwenyekiti wa tume hiyo, Prosper Ntahorwamiye, alisema kuwa CNDD-FDD ilijinyakulia asilimia 96.51 ya kura zote kitaifa.
“Hakuna chama kingine kilichofikia kiwango cha chini cha asilimia 2 kinachohitajika kikatiba kuingia Bungeni, hivyo viti vyote 100 vinakwenda kwa CNDD-FDD,” amesema Ntahorwamiye katika matangazo ya moja kwa moja kupitia runinga.
Kwa ushindi huo, CNDD-FDD kinazidi kuimarisha uthabiti wake wa kisiasa katika taifa hilo la Afrika Mashariki, ambapo kimekuwa madarakani tangu mwaka 2005.

Hata hivyo, hali ni tofauti kwa upande wa vyama vya upinzani ambapo Chama kikuu cha upinzani nchini humo, National Congress for Liberty (CNL), hakikushiriki uchaguzi huo baada ya kupigwa marufuku kushiriki kwa madai mbalimbali yaliyotolewa na mamlaka.
CNL ilishindwa kushiriki uchaguzi kwa sababu mbalimbali ikiwemo kusimamishwa, mgogoro wa ndani ambao ulisababisha uongozi wake kubadilishwa, na baadhi ya wagombea waliopendekezwa hawakuruhusiwa na Tume ya Uchaguzi kwa sababu ya kukosa idhini ya kisera.
Anicet Niyonkuru, mgombea wa ubunge na kiongozi wa chama cha Council of Patriots, alidai kuwa watu waliweka kura zilizokwisha jazwa kwenye masanduku ya kura, na kuuita ‘udanganyifu mkubwa ulioonekana kila mahali.
Kwa upande wake, Olivier Nkurunziza, kiongozi wa chama cha upinzani cha Uprona kilichopata asilimia 1.38 ya kura, amesema uchaguzi huo umechakachuliwa.
“Tumesambaratisha demokrasia,” amesema Nkurunziza akiongeza kuwa katika baadhi ya majimbo, CNDD-FDD ilitangazwa kupata kura zote, bila hata kura batili, za watu kutofika au kukataa kupiga kura, licha ya Uprona kuwa na wagombea zaidi ya 50 katika kila jimbo.
Ripoti kutoka kwa waandishi wa habari na wapigakura waliokataa kutajwa kwa sababu za kiusalama pia zimedokeza kuwepo kwa ukiukwaji mkubwa wa taratibu za uchaguzi.
Itakumbukwa Juni 2023, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Burundi ilisitisha shughuli zote za CNL ikisema kulikuwa na dosari katika mikutano yake ya ndani hatua iliyochukuliwa kama kusitisha shughuli za chama hicho taifa zima.
Imeandikwa na Evagrey Vitalis kwa msaada wa Mashirika