Dar es Salaam. Wakati pato halisi la Taifa lilifikia Sh156.6 trilioni mwaka 2024 kutoka Sh148.5 trilioni mwaka uliotangulia, sekta tatu pekee zimetajwa kuchangia takribani nusu ya pato hilo.
Sekta hizo ni kilimo kilichochangia asilimia 26.3, ujenzi asilimia 12.8 na uchimbaji wa madini na mawe asilimia 10.1.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango Na Uwekezaji, Profose Kitila Alexander amesema hayo leo Juni 12, 2025 wakati akiwasilisha bungeni taarifa ya hali ya uchumi kwa mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2025/26.
Profesa Mkumbo amesema ukuaji huo wa pato la Taifa ulichangiwa na jitihada mbalimbali za Serikali, sekta binafsi na wadau wengine wa maendeleo.
“Jitihada hizo ni pamoja kuanza kwa uzalishaji wa umeme katika Bwawa la Julius Nyerere na utekelezaji endelevu wa miradi ya kimkakati na ya kielelezo inayohusisha miundombinu ya nishati na usafirishaji,” amesema Profesa Mkumbo.
Sababu nyingine za ukuaji huo ni kuongezeka kwa mikopo ya sekta binafsi, usimamizi madhubuti wa sera za fedha, kuimarika kwa uzalishaji wa mazao ya kilimo na uwekezaji wa Serikali katika huduma za jamii hususan elimu, afya, maji na hifadhi ya jamii.
Katika mwaka 2024, sekta tano ziliongoza kwa ukuaji ambazo ni sanaa na burudani kwa asilimia 17.1; uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme asilimia 14.4; habari na mawasiliano asilimia 14.3; fedha na bima asilimia 13.8 na afya asilimia 10.1.
Wakati hali hiyo ikishuhudiwa, taarifa ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ya Aprili 2025 inaonyesha kasi ya ukuaji wa uchumi wa dunia imeendelea kupungua hadi kufikia asilimia 3.3 mwaka 2024 ikilinganishwa na asilimia 3.5 mwaka 2023.
Upungufu huo ulitokana na sababu mbalimbali ikiwemo athari za utekelezaji wa sera za fedha za mataifa mbalimbali, kupunguza ukwasi na kuongeza riba ili kukabiliana na mfumuko wa bei pamoja na migogoro ya kisiasa, hususan Ulaya Mashariki na Mashariki ya Kati.
“Pia taarifa ya IMF inaonyesha kuwa ukuaji wa uchumi wa dunia unatarajiwa kuendelea kupungua na kufikia asilimia 2.8 kwa mwaka 2025,” amesema.
Pia kwa mujibu wa ripoti ya IMF ya Aprili 2025, kiwango cha ukuaji wa pato la Taifa kwa nchi za ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kilikuwa asilimia 1.5 na asilimia 3.1 mwaka 2024, ikilinganishwa na wastani wa ukuaji wa asilimia 5.2 na asilimia 3.9 mwaka 2023, mtawalia.
Kupungua kwa ukuaji wa uchumi kwa nchi wanachama wa EAC na SADC kulitokana na migogoro ya kisiasa ikiwemo migogoro inayoendelea nchini DRC na Sudan Kusini ambapo kumekuwa na ukuaji hasi wa asilimia 27.6 kwa Sudan Kusini.
“Pia athari za mabadiliko ya tabianchi zimepunguza ukuaji wa uchumi kwenye baadhi ya nchi za jumuiya hizo ikiwemo Malawi, Msumbiji na Sudan Kusini kufuatia hali ya ukame na mafuriko, ulioleta athari kubwa katika sekta za kilimo, miundombinu na maisha ya watu. Aidha, kiwango cha ukuaji wa uchumi kwa jumuiya hizo kinatarajiwa kufikia asilimia 2.7 kwa EAC na asilimia 3.5 kwa SADC kwa mwaka 2025,” amesema Profesa Mkumbo.
Wakati pato la Taifa likikua, mfumuko wa bei nchini ulipungua na kufikia asilimia 3.1 mwaka 2024, ikilinganishwa na asilimia 3.8 mwaka 2023.
Mfumuko wa bei ulipungua kutokana na usimamizi madhubuti wa sera za fedha na bajeti, kutengemaa kwa bei za mafuta katika soko la dunia na kuimarika kwa upatikanaji wa chakula katika masoko ya ndani.
“Kiwango hiki cha mfumuko wa bei kipo ndani ya wigo wa lengo la EAC na SADC ya kutokuzidi asilimia 8.0 na kuwa kati ya asilimia 3.0 hadi 7.0,” amesema Profesa Mkumbo.
Taarifa ya IMF ya Aprili 2025 inaonyesha kuwa mfumuko wa bei duniani ulipungua na kufikia wastani wa asilimia 5.8 mwaka 2024 kutoka asilimia 6.7 mwaka 2023.
Kupungua huko kulitokana na utekelezaji wa sera za fedha za kupunguza ukwasi na kushuka kwa bei za bidhaa muhimu, hususan mafuta na mbolea katika soko la dunia.
“Mfumuko huu unatarajiwa kuendelea kupungua na kufikia asilimia 4.3 mwaka 2025 na asilimia 2.2 mwaka 2026. Kwa upande wa nchi za EAC, mfumuko wa bei uliongezeka na kufikia wastani wa asilimia 23.45 mwaka 2024 kutoka asilimia 15.5 mwaka 2023,” amesema Profesa Mkunbo.
Amesema ongezeko hilo lilitokana na kupungua kwa uzalishaji wa chakula kulikosababishwa na mabadiliko ya tabianchi na ongezeko la gharama za usafirishaji.
Aidha, mfumuko wa bei kwa nchi za ukanda wa SADC ulikuwa wastani wa asilimia 62.3 mwaka 2024 ikilinganishwa na asilimia 52.4 mwaka 2023.