Dodoma. Serikali kufanya ukaguzi maalumu katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kuangalia changamoto ya utumikishaji wa watoto nchini.
Kwa mujibu wa Utafiti Jumuishi wa Nguvu Kazi uliofanywa na Serikali, takwimu zinaonesha kuwa utumikishaji huo umepungua kutoka asilimia 29 mwaka 2014 hadi asilimia 24.9 mwaka 2021.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Patrobas Katambi amesema hayo leo Juni 12,2025 katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Utumikishwaji wa Watoto.
Katambi amesema bado kuna kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha watoto wote nchini wanalelewa katika mazingira salama na huru dhidi ya ajira haramu.
Amesema ukaguzi huo utafanyika kwenye migodi, mashamba, viwanda na maeneo mengine yote ambayo kazi zinafanyika.
Amesema kuwa changamoto ya ajira kwa watoto bado ipo kwenye sekta za kilimo, migodi, kazi za nyumbani na ajira zisizo rasmi mijini, ambapo wengi hujikuta wakitumikishwa kwa masilahi ya kiuchumi ya familia au waajiri.
Amesema Serikali imeanzisha mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na Mpango Kazi wa Taifa wa Kupinga Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWA II, 2024/25–2028/29) na Mkakati wa Taifa wa Kutokomeza Utumikishwaji wa Watoto.
Amesema lengo la mikakati hiyo ni kuunganisha nguvu za wadau wote wa maendeleo na mashirika ya kiraia na jamii kwa ujumla.
“Ni marufuku kutumikisha watoto, nitoe wito kwa waajiri wote nchini kuhakikisha hawajihusishi na ajira za watoto. Kaguzi zinaendelea kufanyika na wale watakaobainika, sheria itachukua mkondo wake bila ajizi,” amesema.
Amesema Serikali itaendelea kutoa elimu kwa umma, kushirikiana na wadau na kuhakikisha utekelezaji wa sheria kama Sheria ya Mtoto Sura ya 13 na Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini, Sura 366 unafanyika kwa ukamilifu.
Naye, Mratibu wa miradi kitaifa wa Shirika la Kazi Duniani (ILO), Glory Blasio ameipongeza Tanzania kwa hatua kubwa ya kukabiliana na utumikishaji huo huku akidai kwa kiasi kikubwa utumikishaji bado upo kwa watoto wa kike.
Kamishna wa Kazi, Suzan Mkangwa amesema katika kuadhimisha siku hiyo watafanya kaguzi na kutoa elimu kwa wazazi kujiepusha na utumikishaji watoto kwa kuwa unakiuka sheria na miongozo ya nchi.