Arusha. Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete amesisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kutumia takwimu sahihi na teknolojia za kisasa, hususan katika sekta ya kilimo, ili kuwezesha uundaji wa sera madhubuti za kupambana na umaskini.
Akizungumza leo Alhamisi, Juni 12, 2025, wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kimataifa unaojadili mbinu shirikishi za kutokomeza umaskini duniani, Kikwete amesema umaskini si tatizo la kudumu, bali ni changamoto inayoweza kushughulikiwa kwa jitihada za pamoja kati ya Serikali, sekta binafsi, asasi za kiraia na mashirika ya kimataifa.
Mkutano huo unahusisha wadau na wataalamu kutoka nchi mbalimbali zikiwamo Australia, Bangladesh, Canada, Ethiopia, India, Kenya, Tanzania, Poland na Pakistan.
“Haiwezekani tuendelee kuishi katika dunia yenye utajiri mkubwa huku mamilioni ya watu wakikosa huduma za msingi kama chakula, elimu na afya. Nchi za Afrika zinapaswa kuwekeza zaidi katika utafiti wa kilimo ili kuwawezesha wananchi kukabiliana na njaa na kuinuka kiuchumi kupitia sekta hii muhimu,” amesema Kikwete.
Amesema umaskini si hatima bali ni changamoto inayohitaji juhudi, uvumbuzi na mshikamano wa kitaifa na kimataifa.
Hivyo, amesisitiza kuwa takwimu sahihi zinapaswa kuwa msingi wa utungaji sera ili kusaidia kugawa rasilimali kwa ufanisi na kupima mafanikio ya hatua zinazochukuliwa.
“Takwimu za kuaminika hutuwezesha kutambua mwenendo wa matatizo, kupima ufanisi wa sera na kuimarisha ugawaji wa rasilimali. Majadiliano, tafiti na mbinu bunifu zinazojadiliwa hapa, zitasaidia kuunda mikakati imara kwa miaka ijayo,” amesema Kikwete na kuongeza;
“Leo hatuko hapa kuzungumzia matatizo tu, bali kutafuta suluhisho. Mkutano huu uwe wito wa kuchukua hatua na uthibitisho kuwa hatutakubali umaskini kama hali ya kudumu. Tushirikiane na kutumia maarifa kuhakikisha watu wetu wanapata uwezo wa kujenga maisha yenye heshima na matumaini.”
Akizungumzia juhudi za Tanzania, Kikwete amesema kwa miaka mingi nchi imekuwa ikitekeleza mageuzi ya kiuchumi na kijamii ili kuimarisha usalama wa chakula, kuongeza upatikanaji wa elimu, kupanua huduma za afya na kuanzisha fursa za ajira endelevu.
Amekumbusha kuwa wakati wa uongozi wake, Serikali ilibaini ukuaji wa uchumi pekee haukuwa wa kutosha, hivyo ilianzisha mpango wa Kilimo Kwanza ili kuinua sekta ya kilimo inayotoa ajira kwa Watanzania wengi.
“Pia tuliuimarisha Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) kwa kuwafikia kaya maskini moja kwa moja na tukaanzisha elimu bila malipo ambayo imewapa watoto wengi fursa ya kupata elimu. Hatua hizi zote zililenga kufanikisha lengo la kwanza la Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa la kutokomeza umaskini ifikapo mwaka 2030,” amesema.
Ameongeza kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika kupunguza umaskini kupitia uwekezaji kwenye sekta za afya, miundombinu, na nishati, hali iliyosaidia kubadilisha maisha ya wananchi, hasa wa vijijini.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Dk Ismail Seif Salim ametoa pongezi kwa viongozi wa kitaifa kwa juhudi zao za kuimarisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.
“Serikali zote mbili zimejikita kwenye sekta muhimu kama afya, elimu, miundombinu na kilimo, kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha tunafikia malengo ya kupunguza na kuondoa kabisa umaskini,” amesema Dk Salim.
Naye Mkurugenzi wa Usimamizi wa Sera kutoka Shirika la Oxford Tanzania, Dk Charles Sokile amesema wanashirikiana na Serikali kwa zaidi ya miaka 10 katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya kutokomeza umaskini.