Unguja. Bajeti ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kwa mwaka wa fedha 2025/2026 imependekeza kuongeza viwango vya ushuru katika bidhaa mbalimbali, zikiwemo dizeli, petroli, pombe kali, mvinyo na shisha, hatua inayotarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha Sh38.27 bilioni.
Mbali na mapendekezo hayo ya nyongeza ya ushuru, bajeti hiyo pia imejumuisha ongezeko la mishahara kwa madiwani na masheha, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuboresha masilahi ya viongozi wa ngazi za msingi na kuimarisha ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Hotuba ya bajeti ya SMZ imewasilishwa leo, Alhamisi Juni 12, 2025, na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Fedha na Mipango), Dk Saada Mkuya Salum, akiomba Baraza la Wawakilishi kuidhinisha jumla ya Sh6.9 trilioni kwa ajili ya mwaka wa fedha 2025/2026.
Maombi hayo yamelenga kuongeza mapato ya ndani, kulinda afya ya jamii kwa kudhibiti matumizi ya shisha na vileo vingine vyenye madhara, kuwalinda vijana dhidi ya athari za ulevi, pamoja na kuimarisha viwanda vya ndani na kukuza ajira kwa wananchi.
Kwa mujibu wa Dk Mkuya, SMZ imetenga kiasi cha Sh3.2 bilioni kwa mwaka wa fedha 2025/26 kwa ajili ya kuongeza mishahara ya madiwani na masheha.
Kwa mujibu wa Dk Mkuya amesema katika mwaka wa fedha 2025/26, Serikali inapendekeza kufanya marekebisho ya viwango vya tozo ya leseni ya barabara na tozo ya kuendeleza barabara kwa kuongeza tozo ya leseni ya barabara kutoka Sh38 hadi Sh100 kwa uingizaji wa lita moja ya mafuta ya dizeli na petroli.
“Na kuongeza tozo ya kuendeleza barabara kutoka Sh100 hadi Sh200 kwa uingizaji wa lita moja ya mafuta ya dizeli na petroli.
Hatua hizi zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa Sh35.75 bilioni fedha zake zitatumika katika kuboresha miundombinu ya barabara,” amesema.
Pia, amesema Serikali inapendekeza kuongeza kiwango cha ushuru wa bidhaa kwa uingizaji wa mvinyo na vinywaji vikali kupitia marekebisho ya sheria ya ushuru wa bidhaa namba nane ya mwaka 2017.
Dk Mkuya amesema kwa mwaka wa fedha 2025/26, Serikali inapendekeza kuongeza kiwango cha ushuru wa bidhaa kwa uingizaji wa vinywaji vikali kwa kutoza ushuru wa bidhaa kwa uingizaji wa vinywaji vikali kutoka Sh4,386 hadi Sh6,000 kwa lita na kutoza ushuru wa bidhaa kwa uingizaji wa mvinyo (wine) kutoka Sh4,386.06 hadi Sh6,000 kwa lita.
“Hatua hizo zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa Sh1.25 bilioni ambapo fedha zake zitatumika kwa ajili ya kuimarisha mfuko wa afya,” amesema.
Dk Mkuya amesema kwa mwaka wa fedha uliopita 2024/25, Serikali ilitoza ushuru wa bidhaa kwa kiwango cha asilimia 120 kwa uingizaji wa shisha ili kuwalinda vijana ambao ndio nguvu kazi kwa Taifa.
Hata hivyo, amesema bado kumekuwa na wimbi kubwa la ongezeko na matumizi ya bidhaa hizo nchini, hali iliyosababisha matumizi ya bidhaa hiyo kuongezeka kwa vijana.
“Hivyo, inapendekezwa kutoza kiwango maalumu cha ushuru wa bidhaa cha Sh28, 232 kwa uingizaji wa kilo moja ya ladha ya shisha ili kupunguza matumizi ya bidhaa hiyo kwa vijana. Natarajia kukusanya Sh1.27 bilioni na fedha zake zitatumika kwa ajili ya kuimarisha Mfuko wa Afya,” amesema.
Kuimarisha uzalishaji viwandani
Dk Mkuya amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2024/25, Baraza la Wawakilishi lilipitisha utozaji wa ushuru wa Sh300 kwa kila kilo moja ya kuku au samaki zinazoingizwa Zanzibar.
Lengo la hatua hiyo lilikuwa kuimarisha uzalishaji wa ndani, kuhakikisha ushindani wa haki sokoni, na kuongeza ajira kwa wananchi wengi.
Hata hivyo, bado kuna ongezeko kubwa la uingizaji wa bidhaa hizo, jambo ambalo limeathiri uzalishaji wa ndani na kupunguza ajira kutokana na kushindanishwa kwa bidhaa za nje.
Kwa mujibu wa DK Mkuya kutokana na hali hiyo, Serikali imependekeza ongezeko la ushuru kutoka Sh300 hadi Sh1,000 kwa kilo moja ya kuku au samaki.
Hatua inayolenga kuendeleza viwanda vya ndani, kuhakikisha ushindani halali katika soko la ndani na kukuza ajira zaidi kwa wananchi.
Dk Mkuya amebainisha kuwa ongezeko hili la ushuru linatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa Sh7.25 bilioni.
Makusanyo na deni la Taifa
Kwa mwaka wa fedha 2024/25, Serikali ilipanga kukusanya jumla ya Sh5.182 trilioni kutoka vyanzo vyote vya ndani na nje. Hadi kufikia Machi 31, 2025, kiasi cha Sh2.204 trilioni kilishakamilika kukusanywa.
Dk Mkuya amesema kuwa deni linalodhaminiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar limefikia Sh1.334 trilioni hadi Machi 2025.
“Kati ya deni hilo, la ndani linakadiriwa kuwa Sh1.319 trilioni, linalojumuisha asilimia 99 ya jumla ya deni, wakati deni la nje likiwa ni Sh15.20 bilioni, sawa na asilimia moja tu ya deni lote,” amesema.
Kwa mujibu wa Dk Mkuya deni hilo limeongezeka kwa kiasi cha Sh400.6 bilioni ikilinganishwa na deni lililoripotiwa Machi 2024, lililokuwa Sh934 bilioni.
Ameeleza kuwa kati ya deni la ndani, Sh557.5 bilioni linatokana na hati fungani za muda mrefu kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), huku Sh761.9 bilioni likitokana na mikopo kutoka taasisi za kifedha mbalimbali.
Dk Mkuya amesema kwa upande wa mwenendo wa makusanyo ya mapato, Serikali inatarajia kukusanya kiasi cha Sh4.057 trilioni ifikapo Juni 2025, sawa na asilimia 78 ya makadirio ya jumla ya Sh5.182 trilioni kwa mwaka mzima wa fedha.
Kuongeza uthaminishaji wa bidhaa
Kwa sasa uthaminishaji wa bidhaa zinazoingizwa nchini hutozwa kodi kwa wastani wa asilimia 20 hadi asilimia 50 ambapo amesema viwango hivi, vimepitwa na wakati na haviendani na hali halisi ya uchumi wa Zanzibar.
Hivyo, amesema Serikali inapendekezwa kuongeza uthaminishaji wa bidhaa kwa kiwango cha asilimia 25 ya kiwango cha sasa.
“Miongoni mwa bidhaa zinazopendekezwa kuongezwa uthaminishaji ni nondo, saruji, misumari, marumaru, vinywaji vikali, mvinyo na magari, mpango huu unatarajia kukusanya Sh12.75 bilioni,” amesema Dk Saada
Kutoa unafuu ushuru wa bidhaa
Amesema taasisi za fedha zikiwemo benki zimekuwa zikitozwa ushuru wa bidhaa wakati wa ununuzi wa huduma kutoka nje ya nchi. Hali hiyo imepelekea kuongezeka kwa gharama za utoaji wa huduma.
Hivyo, Serikali inapendekeza kutoa unafuu wa ushuru wa bidhaa kwa taasisi za fedha wakati wanaponunua huduma kutoka nje ya nchi ili kuimarisha miundombinu ya huduma za kifedha pamoja na kuongeza wigo wa huduma jumuishi za kifedha.
Amesema hatua hiyo inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa Sh37.27 bilioni.
Kuimarisha huduma ya elimu
Amesema miongoni mwa vipaumbele vya Serikali ni kuimarisha sekta ya elimu nchini ili kujenga Taifa lenye wasomi, ambao wataitumikia nchi hapo baadaye.
Hivyo, inapendekeza kutenga asilimia moja ya Corporate Social Responsibility (CSR) na Marketing kuchangia katika mfuko wa elimu.
Dk Mkuya amesema Serikali pia inapanga kufanya mageuzi katika taasisi za ukusanyaji mapato kwa kuipa Mamlaka ya Mapato Zanzibar jukumu la kusimamia mapato yote ya wizara.
“Serikali itaanzisha Taasisi ya Uchumi Halali (Zanzibar Halal Bureau) kwa ajili ya kuthibitisha uhalali wa bidhaa na huduma, hasa kwa masoko ya Mashariki ya Kati.
“Serikali pia imepanga kufanya mapitio ya sheria za kodi na misamaha ili kuboresha usimamizi wa mapato, huku ikisisitiza matumizi ya mifumo ya kielektroniki katika kufanya malipo na kupunguza utegemezi wa fedha taslimu,” amesema.
Dk Mkuya amesema fedha zimetengwa pia kwa ajili ya shughuli za uchaguzi mkuu, kuanzisha Soko la Mitaji Zanzibar, na kukuza sekta ya kilimo kupitia teknolojia ya ‘greenhouse’.
Pia, ametangaza Sh3.2 bilioni zimetengwa kwa ajili ya nyongeza ya mishahara ya madiwani na masheha, pamoja na posho za walimu na makatibu wa mikoa.