Bajeti ya kimkakati | Mwananchi

Dar es Salaam. Serikali imewasilisha bajeti ya kimkakati kwa mwaka wa fedha 2025/26, ikilenga kuiweka nchi katika nafasi imara ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Katika mkakati huo, imeelekeza vipaumbele vyake kwenye maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, maandalizi ya michuano Mataifa ya Afrika (Afcon) 2027 na utekelezaji wa miradi ya mikubwa ya maendeleo.

Bajeti hiyo, iliyowasilishwa leo Alhamisi Juni 12, 2025 na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba bungeni jijini Dodoma, inaangazia pia kuimarisha sekta za uzalishaji, rasilimali watu na mazingira ya biashara, kwa lengo la kuchochea uchumi jumuishi unaoshirikisha sekta binafsi na kukuza ajira.

Kupitia bajeti hiyo, Serikali imesisitiza dhamira yake ya kugharimia Uchaguzi Mkuu kwa kutumia fedha za ndani, kuendeleza miundombinu ya michezo kwa ajili ya Afcon na kuimarisha usimamizi wa fedha za umma kupitia mifumo ya kidijitali, uwajibikaji na ufuatiliaji wa karibu wa miradi ya kimkakati.

Aidha, bajeti hiyo inakwenda kulipa mishahara mipya ya watumishi wa umma nyenye nyongeza inayoanza Julai mosi pamoja na ongezeko la pensheni kwa wastaafu wa kima cha chini wanaolipwa na Hazina.

Waziri Nchemba amesema Serikali pia imeweka kipaumbele cha ugharamiaji wa deni la Serikali, mishahara na stahiki za watumishi wa umma, ujenzi na ukarabati wa viwanja vya michezo kwa ajili ya maandalizi ya Afcon 2027.

“Nipende kuwafahamisha Watanzania kuwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 tutaugharamia kwa fedha zetu za ndani,” amesema Dk Nchemba.

Katika eneo la kuboresha mazingira ya biashara, Dk Nchemba amesema wanalenga kuvutia ushiriki wa sekta binafsi katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Vilevile, amesema Serikali inakwenda kukamilisha utekelezaji wa miradi, programu za maendeleo na afua zinazochangia maeneo makuu ya vipaumbele vya Mpango wa tatu wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano.

Waziri huyo amezungumzia pia lengo la kuimarisha usimamizi wa bajeti husika na kuimarisha matumizi sahihi ya mifumo ya Tehama katika utekelezaji wa shughuli za Serikali.

“Tutaimarisha uwajibikaji na udhibiti katika matumizi ya fedha za umma kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo ili kuziba mianya ya ubadhirifu kwa lengo la kupata thamani ya fedha katika matumizi ya Serikali,” amesema.

Pia, amesema Serikali itaimarisha ufuatiliaji na tathmini katika utekelezaji wa miradi ili kuhakikisha inafanywa kwa ufanisi na kuokoa gharama za ziada zinazoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji.

Asilimia 71 ya bajeti yote ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2025/26 inatarajiwa kugharamiwa kwa mapato ya ndani, huku kiwango kilichobakia kikitegemewa kutoka kwenye mikopo na misaada.

Wakati hali ikiwa hivyo kwenye vyanzo vya bajeti hiyo, asilimia 29.4 ya bajeti yote imeelekezwa katika Mfuko Mkuu, huku asilimia 24.8 ikielekezwa kwenye kulipia madeni.

Katika mwaka huo wa fedha, Serikali imepanga kukusanya na kutumia jumla ya Sh56.49 trilioni, kama ilivyowasilishwa leo Alhamisi Juni 12, 2025 na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba bungeni jijini Dodoma.

Dk Nchemba amesema kati ya kiasi hicho, Sh40.46 trilioni zinatarajiwa kutoka kwenye mapato ya ndani, huku kiasi kilichobaki kikitarajiwa kupatikana kupitia mikopo na misaada.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, misaada na mikopo inatarajiwa kuchangia Sh1.74 trilioni ya bajeti hiyo, huku misaada ya mikopo ya miradi ikichangia Sh5.18 trilioni.

Pia, amesema kutakuwa na misaada ya mikopo ya kisekta itakayochangia Sh189.73 bilioni, huku mikopo ya ndani ikifikia Sh3.32 trilioni, ile mikopo ya nje Sh2.95 trilioni na mikopo ya kibiashara Sh2.62 trilioni.

Kwa upande wa matumizi, Serikali inatarajia kutoa Sh1.3 trilioni kila mwezi kwa ajili ya Mfuko Mkuu, ambapo kati yake Sh1.18 trilioni zitakuwa kwa ajili ya kulipa deni la Taifa.

Aidha, kila mwezi Serikali itatumia Sh1.09 trilioni kwa ajili ya kulipa mishahara ya watumishi wa umma katika mwaka huo wa fedha.

Katika matumizi mengine, Dk Nchemba amesema jumla ya Sh9.18 trilioni zinatarajiwa kutumika, ambapo fedha za halmashauri zitakuwa Sh1.09 trilioni na matumizi mengine ni Sh8.1 trilioni.

Kuhusu matumizi ya maendeleo, Dk Nchemba amesema Sh17.49 trilioni zinatarajiwa kutumika, kati ya hizo, Sh12.11 trilioni zitakuwa ni fedha za ndani, huku Sh5.37 trilioni zikiwa fedha za nje.

Mgawanyo wa bajeti kisekta

Katika mgawanyo wa bajeti, sekta iliyoongoza kwa kutengewa fedha nyingi ni huduma za utawala, ikibeba Sh24.5 trilioni, kati ya hizo deni la Taifa likibeba Sh14.2 trilioni, huku mihimili ya utawala, usimamizi wa mapato na matumizi, mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki ukitarajiwa kutumia Sh10.3 trilioni.

Kiwango kilichotengwa kwa ajili ya deni la Taifa ni takriban asilimia 25 ya bajeti yote.

Bajeti hiyo inaeleza kuwa, sekta ya elimu ndiyo itakayokuwa katika nafasi ya pili kwa kutumia fedha nyingi, ikitengewa Sh7.39 trilioni, ikifuatiwa na ulinzi, utawala wa sheria na usalama iliyopewa Sh6.3 trilioni.

Inayofuata ni sekta ya ujenzi, usafirishaji na mawasiliano, ikipewa Sh5.52 trilioni, kisha hifadhi ya jamii Sh3.1 trilioni na afya Sh3 trilioni.

Sekta nyingine ni nishati iliyotengewa Sh1.96 trilioni, ikifuatiwa na kilimo Sh1.92 trilioni.

Zinazofuata ni sekta ya maji Sh897.1 bilioni, habari, michezo na utamaduni Sh519.6 bilioni, maliasili, utalii na mazingira Sh317.4 bilioni, viwanda na biashara Sh239.5 bilioni, madini Sh225 bilioni na maendeleo ya jamii Sh196.5 bilioni.

Pia, imo sekta ya ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi, iliyotengewa Sh166.9 bilioni.

Katika mgawanyo wa bajet hiyo, vijana ndilo kundi lililotengewa fedha kiduchu zaidi kiasi cha Sh38.4 bilioni, ikiwa ni kiwango kidogo zaidi cha fedha kilichotengwa kwa mujibu wa mgawanyo wa bajeti katika sekta.

Hata hivyo, kiwango hicho kilichotengwa ni ongezeko la asilimia 12.9 kutoka Sh34 bilioni zilizotengwa kwa ajili ya kundi hilo, kazi na maendeleo ya kukuza ujuzi mwaka uliopita.

Asilimia 71 ya bajeti yote ya Serikali ya mwaka 2025/26 inategemea mapato ya ndani, huku kiwango kinachosalia, asilimia 29 kikitegemea mikopo.

Wakati hali ikiwa hivyo kwenye vyanzo vya bajeti hiyo ya Sh56.49 trilioni, asilimia 29.4 ya bajeti yote imeelekezwa katika mfuko mkuu, huku asilimia 24.8 ikielekezwa katika kulipa madeni.

Wakati huo huo, kila mwezi Serikali itatumia Sh1.09 trilioni kulipa mishahara ya watumishi wa umma ndani ya mwaka huo wa fedha.

Mgawanyo wa bajeti kisekta

Katika bajeti hiyo, vijana ndilo kundi lililotengewa fedha kiduchu zaidi kiasi cha Sh38.4 bilioni, ikiwa ni kiwango kidogo zaidi cha fedha kilichotengwa kwa mujibu wa mgawanyo wa bajeti katika sekta.

Hata hivyo, kiwango hicho kilichotengwa ni ongezeko la asilimia 12.9 kutoka Sh34 bilioni zilizotengwa kwa ajili ya vijana, kazi na maendeleo ya kukuza ujuzi mwaka uliopita.

Related Posts