Tabora. Jeshi la Polisi Mkoa wa Tabora limeanzisha uchunguzi wa kina kubaini chanzo na wahusika waliokurekodi na kusambaza taarifa na video inayomtambulisha Daudi Delimu kuwa ni Mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi (OCS) Wilaya ya Igunga.
Akizungumza na Mwananchi ofisini kwake jana Juni 12, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao alisema uamuzi huo unatokana na sababu kuu tatu, ikiwemo dalili za uwepo wa nia ovu nyuma ya kurerekodiwa na kusambaza video hiyo.
“Sitaki kutoa maelezo yanayoweza kuingilia hatua ya uchunguzi, lakini ni dhahiri kulikuwa na nia ovu nyuma ya tukio lile kwa sababu Delimu si askari wala OCS wa Kituo cha Polisi Igunga,” alisema Kamanda Abwao
Alisema ni jambo la kufikirisha kuona mazungumzo ya mzee huyo na viongozi wa Chadema yamerekodiwa na kurushwa yakiambatana na maelezo yanayomtambulisha kuwa ni mkuu wa kituo cha polisi wakati si kweli.
Kamanda Abwao alisema uongo wa maelezo ya utambulisho wa Delimu umeibua taharuki katika jamii na kusababisha usumbufu kwa makundi mengi likiwemo Jeshi la Polisi lenyewe.
Alisema matokeo ya uchunguzi ndio utabaini wahusika, nia yao ya kurekodi na kusambaza video yenye maelezo na utambulisho wa uongo wa Mzee Delimu.
“Sitaki kuingia kwa undani wa suala hili, lakini naamini baada ya uchunguzi tutajua wahusika na hatua ya kuchukua. Lakini kwa sasa itoshe tu kusema tunaendelea kumhoji Mzee Delimu kujua mazingira ya yeye kuhojiwa na kurekodiwa akiwa eneo la kituo cha polisi na kupewa utambulisho wa uongo,” alisema Kamanda Abwao.
Maelezo ya Kamanda huyo wa Polisi yanatokana na video iliyosambaa kupitia mitandao ya kijamii ikimwonyesha Delimu, mkazi wa Kijiji cha Mbagala A, Wilaya ya Igunga mkoani Tabora akimwomba radhi Heche kwa kitendo cha kijana wake, kudaiwa kufanya vurugu kwenye mkutano wake wa hadhara.
Tukio la vurugu lilitokea wakati viongozi wa Chadema wakihutubia mkutano katika uwanja wa Sokoine mjini Igunga baada ya vijana waliojichomeka katikati ya umati kuanza kipiga kelele, kabla ya kuanza kushambulia watu kwa mawe na kujeruhi watu kadhaa.
Kutokana na vurugu hizo, Jeshi la Polisi Wilaya ya Igunga ilimtia mbaroni Lufigo Bundala, mkazi wa Kijiji cha Ibuta wilayani Igunga kwa tuhuma za kuhusika kwenye vurugu hizo.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Polisi Wilaya ya Igunga, Meshack Sumuni, Bundala pamoja na wenzake wawili waliofanikiwa kutoroka ndio waliongoza wenzao kufanya vurugu hizo.
Video iliyoibua sintofahamu
Baada ya kuhitimisha mkutano wake, Heche akiongozana na viongozi kadhaa wa Chadema walienda Kituo Kikuu cha Polisi Wilaya ya Igunga ambapo walikutana na OCD na wakati wanatoka kituoni, ndipo wakakutana na Mzee Delimu aliyejitambulisha kuwa ni mjomba wa Bundala na kuomba radhi kwa vurugu za mkutanoni kwa niaba ya mpwa wake, ambaye wakati huo alikuwa mikononi mwa polisi.
Wakati mzee huyo akizungumza, watu walirekodi maelezo na kuisambaza video mitandaoni na maelezo kuwa mhusika ni Mkuu wa Kituo cha Polisi Igunga akimwomba radhi Heche.
Akizungumzia sakata hilo, Heche alieleza kusikitishwa na kitendo cha Mzee Delimu kushikiliwa na polisi kwa tuhuma kuwa alijitambulisha ni Mkuu wa Kituo cha Polisi.
“Kwanza mzee yule (Delimu) alijitambulisha kwangu ni mjomba wa kijana aliyekamatwa kwa kufanya fujo… Nimesikitishwa kuona video yake ya kuomba radhi inasambaa ikiwa na utambulisho eti ni OCS wa Igunga,” alisema Heche.
Alisema isingekuwa rahisi kwa Mzee Delimu kujitambulisha kwake ni OCS wa Igunga kwa sababu muda anakutana naye nje ya kituo cha polisi, yeye na viongozi wenzake wa Chadema tayari alishakutana na kuzungumza na OCS husika ofisini kwake kabla ya kuwapeleka kwa Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD).
“Kwanza OCS wa Igunga ni mwanamke; hivyo, kitendo cha video ya mwanaume kusambaa mitandao ikimtambulisha ni OCS ni jambo lenye nia ovu ama kwa Chadema au kwa mzee wa watu. Nawasihi polisi wamwachie huru kwa sababu yeye ni mwathirika wa nia ovu hiyo,” alisema Heche.
Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Magharibi, Dickson Matata ameungana na Heche kuliomba Jeshi la Polisi kumwachia huru Mzee Delimu akisema ni ama aliyerekodi na kusambaza video ikimtambulisha kuwa OCS wa Igunga hakupata taarifa sahihi au amefanya makusudi kwa nia ovu.
“Tayari nimerekodi video nikielezea tukio hilo na kuisambaza mitanadaoni tangu jana kuwezesha umma kupata ukweli wa kilichotokea,” amesema Matata.