Musoma. Mwanafunzi wa kidato cha tatu ambaye bado hajafahamika amemtelekeza mtoto wake mwenye umri wa wiki moja na siku nne katika eneo la stendi ya mabasi Bweri Manispaa ya Musoma kwa madai ya ugumu wa maisha, huku akiomba serikali na wadau kumsaidia katika malezi ya mtoto huyo.
Mbali na ugumu wa maisha pia mwanafunzi huyo ambaye ameeleza kuwa anasomea nchini Kenya amesema ameamua kufanya hivyo ili aweze kurudi shule na kuendelea na masomo yake, huku akiahidi kurejea na kumchukua mwanaye huyo baadaye atakapohitimu masomo yake mwakani.
Akizungumza na Mwananchi leo Juni 13, 2025 Mkazi wa Mtaa wa Morembe katika Manispaa ya Musoma, Happiness Chacha ameeleza namna alivyomuokota mtoto huyo mwenye jinsi ya kiume ambapo amesema siku hiyo akiwa anaeleka nyumbani kwake alisikia mtoto akilia pembezoni mwa barabara jambo ambalo lilimpa hofu.
“Ilikuwa juni 9, 2025 muda wa saa tisa mchana nikiwa naelekea nyumbani nilipofika jirani na kanisa la Kanisa la Kiinjili la Kilitheri Tanzania (KKKT) nikasikia mtoto akilia nikajiuliza iweje mtoto alie maeneo yale wakati siyo makazi ya watu ndipo nikaelekea sehemu ilipokuwa ikitokea sauti ili niweze kujua kulikoni,” amesema.
Amesema baada ya kufika eneo hilo alibaini uwepo wa mtoto mchanga aliyefunikwa na kanga, huku pembeni pakiwa na mfuko mdogo wenye nguo.
“Nilimfunua haraka haraka kwakweli alikuwa na hali mbaya inaonekana alilia kwa muda mrefu kwani alikuwa amejisaidia na inaonekana alikuwa njaa huku akikosa pumzi nadhani wakati anahangika akwa anajikaba na ile kanga na kusababisha akose pumzi,” ameeleza.
Amesema baadaye walimpeleka mtoto huyo katika ofisi ya Mtaa wa Morembe mita chache kutoka eneo la tukio kabla ya mtoto kupelekwa kituo cha polisi na ustawi wa jamii kwa hatua zingine.
Katika eneo la tukio pia kulikuwa na barua inayosadikiwa kuwa iliandikwa na mama wa mtoto huyo na kuwekwa ndani ya mfuko wa nguo uliokuwa pembeni.
Barua hiyo yenye kurasa mbili huku mwandishi wake akiwa ametumia kalamu nyekundu kuandika ujumbe aliokusudiwa kufika kwa jamii na umma kwa ujumla.
Kwa mujibu wa barua hiyo, mwandishi wake ndiye mama wa mtoto na ameeleza kuwa yeye ni mwanafunzi wa kidato cha tatu huko nchini Kenya ambapo awali ya yote ameomba radhi kwa uamuzi huo alioufanya kwani amelazimka kufanya hivyo kutokana na kutokuwa na namna yoyote ile.
Katika barua hiyo ameomba mtoto wake huyo atunzwe vizuri bila kunyanyaswa huku akitoa na pendekezo la jina kuwa aitwe Sabato Elija ambapo pia ameeleza kuwa mbali na mtoto huyo kuwa na umri wa wiki moja na siku nne tayari amepata chanjo ya bega maarufu chanjo ya ndui.
“Nimelazimika kufanya hivi sio kwa kupenda kwangu, mimi ni mwanafunzi ila kwa ujinga wangu nilipata ujauzito baada ya kushawishiwa na marafiki zangu, sina cha kumpa huyu mtoto,naomba msaada wenu,najua mtauliza kuhusu wazazi wangu ukweli ni kuwa mama amekataa kunisamehe yeye anachotaka ni mimi kurudi shule,” inasomeka sehemu ya barua hiyo.
Amesema yeye sio muuaji na ndio maana ameamua kumuacha mtoto huyo katika eneo hilo ili aweze kupata msaada huku akieleza tangu amejifungua mlo kwake ni changamoto kutokana na mama yake kushindwa kukubaliana na hali aliyokuwa nayo ya ujauzito hivyo kukosa maziwa ya kumyonyesha mwanae na kwamba anaamini njia hiyo ni sahihi kwaajili ya kumnusuru mtoto.
“Nimefanya maamuzi haya lakini nina maumivu makali na uchungu mwingi pia naomba mjue sijamtupa mwanamgu ila naomba mwenye uwezo anisaidie,nitarudi kumchukua,”
Ofisa Mtendaji wa Mtaa wa Morembe, Johnson Mwenura amesema hadi sasa bado hawajapata taarifa juu ya mzazi wa mtoto huo kwani hakuna taarifa juu ya uwepo wa mzazi katika mtaa wake ambaye amejifungua karibuni na mtoto wake haonekani.
“Wanasema siku ya tukio huyo binti alionekana akivuka ule mto karibu na stendi na kuna mtu alimshika mkono kumsaidia kuvuka kwasababu pale pana mawe na yeye alikuwa amebeba mtoto na huo mfuko na alipovuka alipanda bodaboda na kusema anaelekea kanisa la Wasabato kule juu sasa haijulikani kwanini safari ilishia hapa hapa,” amesema
Meneja Msaidizi wa Kituo cha kulea watoto yatima cha Musoma, Consolatha Maduhu amesema mtoto huyo hivi sasa anatunzwa katika kituo hicho huku akitoa wito kwa wadau kujitokeza kusaida katika mahitaji ya mtoto hasa maziwa na mavazi.
“Tumeona maziwa ya kopo ni bora zaidi hasa kwa umri wake lakini maziwa haya ni aghali hivyo tunaomba wadau wajitokeze kutuunga mkono sambamba na nguo kwani hayo ndiyo mahitaji ya mtoto kwa sasa,” amesema
Amesema hadi sasa hakuna changamoto yoyote ya kiafya waliyobaini kwa mtoto huyo, huku akieleza kuwa malezi yake si magumu kwani halii mara kwa mara.
Ofisa Ustawi wa Jamii wa Manispaa ya Musoma, Atupele Chilambo amesema mtoto amekabidhiwa katika kituo cha kulelea watoto kwaajili ya uangalizi wakati polisi wakiendelea na uchunguzi.
Amesema tukio la aina hiyo lilitokea Machi mwaka huu ambapo mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja alitelekezwa na mzazi wake katika kituo cha daladala katikati ya mji wa Musoma ambapo mzazi huyo aliacha kadi ya kliniki ya mtoto huo pamoja na ujumbe uliodai kuwa amefanya hivyo kutokana na ugumu wa maisha.
“Kumekuwa na ongezeko la watoto kutelekezwa ingawa kwasasa sina takwimu,wengine kwenye nyumba za kulala wageni wengine kwenye vichaka na vituo vya usafiri na maeneo mengine mengi, na baadhi ya watoto wanakuwa katika hali mbaya sana kiafya” amesema
Amesema zipo sababu kadhaa zinazosababisha kuwepo kwa hali hiyo ikiwepo suala la ugumu wa maisha na kwamba ofisi yake imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa malezi ya wazazi kwa mtoto.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Pius Lutumo amethibitisha kutokea tukio hilo na kuongeza kuwa tayari wameanza uchunguzi ili kubaini mzazi wa mtoto huyo na hatimaye hatua ziweze kuchukuliwa.