Miili waliofariki dunia ajali ya basi na lori yatambuliwa Moro

Morogoro. Miili yote 10 ya waliofariki kwenye ajali ya basi la kampuni ya Hai Express iliyogongana na lori jana Juni 12 mwaka huu, imetambuliwa na tayari baadhi ya miili hiyo imeshachukuliwa na ndugu kwa ajili ya taratibu za mazishi.

Akizungumza na Mwananchi, Ofisa Uhusiano wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro, Scholastica Ndunga amesema mpaka kufikia asubuhi ya leo Ijumaa Juni 13, 2025 miili miwili ya marehemu hao ilishatambuliwa na kuchukuliwa na ndugu zao huku mingine ikiendelea kuhifadhiwa wakati ndugu wakifuata taratibu za kuichukua.

Kuhusu majeruhi Ndunga amesema kati ya majeruhi 44 waliofikishwa hospitali hapo watatu wamepewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya kupatiwa huduma za kibingwa na wengine 24 wameruhusiwa kurudi nyumbani baada ya kuonekana afya zao zinaendelea vizuri.

“Kwa sasa majeruhi waliobaki hapa hospitali ni 17, wanaume ni 10 na wanawake ni saba wanaendelea kupatiwa vipimo na matibabu mbalimbali tunaamini Mwenyezi Mungu atawaponya kwa haraka, ” amesema Ndunga.

Related Posts