Dar es Salaam. Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imewatunuku vyeti wahitimu 48 na walimu 8 waliofanya vizuri zaidi kwenye masomo ya sayansi kidato cha nne 2023 na kidato cha sita 2024 kwa kutambua bidii na kujituma kwao katika masomo hayo.
Zawadi hizo zimehusisha mshindi wa kwanza hadi wa tatu kwa wasichana na wavulana kwa kila somo kwa kidato cha nne na kidato cha sita.
Akizungumza Juni 12, 2025 jijini Dar es Salaam katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Kinga kutoka Wizara ya Afya, Dk Hamad Nyembea amesema Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imeendelea na utaratibu wa kila mwaka wa kuwazawadia wanafunzi wanaofanya vizuri zaidi katika masomo hayo kitaifa katika mitihani yao ya kidato cha sita na nne.
“Kwa kuwa wingi wa ufaulu katika masomo hayo, ni ufanisi mkubwa katika maendeleo ya watoto wenyewe, shule wanazotoka, wazazi pamoja na taifa katika kuhimili matokeo ya ukuaji wa sayansi na teknolojia,” amesema Nyembea, akimuwakilisha Waziri wa Afya, Jenista Mhagama.
Amesema Serikali inaendelea kufanya jitihada mbalimbali zenye kuwezesha na kutoa msukumo kwa wanafunzi kupenda masomo sayansi ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya baadaye kwa vijana kukabiliana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia, na mchango wake kwa maendeleo endelevu.
Mkurugenzi huyo amesema Serikali imewapa nafasi sawa watoto wa Kitanzania kupata elimu kwa kuondoa ada kwa elimu ya msingi na sekondari, kuajiri walimu wa sayansi, kuboresha maabara na maktaba za kujifunzia, kuweka miundombinu mbalimbali kama vile vifaa na mifumo ya Tehama pamoja na kuongeza vyumba vya madarasa na madawati.
“Mheshimiwa Rais hakuwasahau wanafunzi wenye changamoto mbalimbali kwa kuwawekea miundombinu rafiki katika shule wanazosoma ili kuhakikisha hawabaki nyuma katika kujipatia elimu,” amesema.
Kwa upande wa sekta ya afya, amesema Serikali imefanya uwekezaji mkubwa wa miundombinu hasa katika ujenzi wa majengo yenye kukidhi mahitaji na ununuzi wa mitambo na vifaa mbalimbali vya kisasa ili kuboresha utoaji wa huduma katika sekta ya afya.
Amesema Mamlaka ya Maabara ya Mkemia wa Serikali, pia, ni mnufaika mkubwa wa masomo ya sayansi ikihitaji watalaamu wa kemia, vinasaba vya binadamu, sayansi ya chakula, mazingira, tiba asili na watalaamu wa mitambo ya uchunguzi wa kimaabara ambao wote kwa pamoja wanahitaji kujengwa kupitia masomo ya Kemia, Biolojia, Hisabati na Fizikia.
Kwa upande wake, Mkemia Mkuu wa Serikali, Dk Fidelice Mafumiko amesema tangu kuanza kwa utaratibu wa kutoa zawadi mwaka 2007 hadi sasa, Mamlaka itakuwa imetoa tuzo na zawadi kwa jumla ya wahitimu 432 na walimu 56.
“Tangu kuanzishwa kwake, utaratibu huu umepata mafanikio mengi ikiwemo kuongeza hamasa kwa wanafunzi na kuongeza nguvu kazi ya wataalamu katika sekta ya afya na sekta nyinginezo zinazohitaji taaluma ya sayansi,” amesema Dk Mafumiko.
Amesema takwimu zinaonesha tangu kuanza kwa utaratibu huo, zaidi ya asilimia 75 ya wanafunzi wanaozawadiwa, hususani kwa kidato cha sita, wanajiunga vyuo vinavyotoa taaluma ya afya ikiwemo Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), Chuo Kikuu cha Afya Bugando, Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) na Chuo Kikuu cha Kumbukumbu cha Hubert Kairuki.