Selfie’ ya mwisho familia watu watano kabla ajali

Ahmedabad, India. Akitabasamu mbele ya kamera, hii ndiyo ‘selfiE’ ya mwisho aliyopiga Daktari Prateek Joshi akiwa na mkewe na watoto wao muda mfupi kabla ya wote kufariki dunia kwenye ajali  ya ndege ya Air India.

Dk Joshi, mtaalamu wa mionzi (radiologist) aliyekuwa akifanya kazi katika Hospitali ya Royal Derby nchini Uingereza, alikuwa amesafiri kwenda India siku mbili tu kabla ya ajali hiyo ya Alhamisi, kwa ajili ya kuungana na familia yake mke wake Dk Komi Vyas, pacha wao wa miaka mitano Nakul na Pradyut, pamoja na binti yao wa miaka minane, Miraya.

Familia hiyo ilikuwa hatimaye tayari kuanza maisha mapya kwa pamoja nchini Uingereza baada ya muda mrefu wa kuwa mbali. Picha waliopiga wakiwa ndani ya ndege iliibua taswira ya furaha na matumaini.

Wakiwa wameketi ndani ya ndege katika uwanja wa Ahmedabad, Dk Joshi alitabasamu kwa furaha mbele ya kamera akiwa karibu na mke wake wa ndoa ya miaka kumi, ambaye hivi karibuni alikuwa ameacha kazi yake katika Hospitali ya Pacific huko Udaipur ili kuungana na familia nchini Uingereza.

Watoto wao watatu, waliokuwa wameketi upande wa pili wa njia ya kupita ndani ya ndege, walitabasamu lakini kumbe walikuwa katika furaha ya mwisho.

Hakuna aliyeweza kutarajia kilichokuwa kikiwasubiri sekunde chache baadaye ndege hiyo ilipoanguka ghafla baada ya kupaa, ikisababisha vifo vya abiria wote waliokuwa ndani, huku mtu mmoja tu akinusurika.

Hekalu la Kihindu la Derby, mahali ambapo Dk Joshi alikuwa mshiriki wa kawaida wa ibada, lilithibitisha kwa huzuni kupitia ujumbe wa mtandaoni kwamba familia hiyo ya watu watano ilikuwa miongoni mwa raia 169 wa India waliopoteza maisha kwenye ajali hiyo.

Rafiki wa karibu na mwanafunzi mwenzake wa zamani, Dk Deepak Kaladagi, alishiriki picha ya familia hiyo wakiwa likizoni na kuandika ujumbe wa majonzi: “Roho zao zipumzike kwa amani na Mungu awape nguvu familia na wapendwa wao kuvumilia msiba huu mzito.”

Kwa mujibu wa taarifa rasmi, jumla ya watu 229 walifariki katika ajali hiyo, wakiwemo Waingereza 52, Wahindi 169, Wareno 7 na raia mmoja wa Canada.

Related Posts