Wanasheria, madaktari wataja hatari punguzo tozo ya ‘energy drink’

Dar es Salaam. Wanasheria na wataalamu wa afya wameitaka Serikali kufuta pendekezo la punguzo la kiwango cha ushuru wa bidhaa kwenye vinywaji vya kuongeza nguvu ‘energy drink’ wakisema ni kinyume cha Katiba ya nchi katika kulinda afya ya jamii.

Badala yake wameitaka Serikali kuja na sera zitakazodhibiti uingizaji, uzalishaji na matumizi ya vinjwaji hivyo ili kupambana na unywaji holela unaoambatana na athari katika ogani za figo, moyo na ini.

Maoni hayo yametolewa siku moja baada ya kusomwa mapendekezo ya bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2025/2026 bungeni Juni 12, 2025 na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba.

Serikali imepunguza kiwango cha ushuru wa bidhaa ya vinywaji hivyo vinavyozalishwa ndani ya nchi kutoka Sh561 kwa kila lita hadi Sh134.2 kwa kila lita.

Dk Mwigulu alisema lengo ni kuweka unafuu kwa wazalishaji wa ndani wa energy drink, kuongeza ushindani na kuchochea uwekezaji nchini, hatua aliyosema itapunguza mapato ya Serikali kwa Sh1.7 bilioni.

Wakili na mwanasheria, Jebra Kambole amesema wananchi wana haki ya kupata usalama ikiwa ni pamoja na kula na kutumia vinywaji bora na vyenye viwango.

“Hii haiko sawa, Serikali inapaswa kutohamasisha matumizi ya energy drinks kwa sababu ina wajibu wa kulinda na kusimamia afya za Watanzania. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 26 ibara ndogo ya kwanza, inatoa wajibu wa kuheshimu sheria na Katiba ya nchi. Tafiti zinaonyesha matumizi ya energy drinks ambayo yamezidi viwango yana athari kubwa kwa afya,” amesema.

Ameshauri bidhaa hiyo kuongezwa kodi ili Watanzania wengi washindwe kuitumia akieleza: “Kupunguza tozo itazalishwa kwa wingi zaidi na itashuka bei na wengi wataitumia.”

Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), kimezungumzia tozo hiyo kikirejea utafiti uliochapishwa na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) miaka miwili iliyopita juu ya matumizi ya energy drinks.

Rais wa MAT, Dk Mugisha Nkoronko amesema utafiti ulionyesha matumizi yanaongezeka kwa kasi, vijana wakikitumia kufanya kazi huwapa hamasa ya kuendelea na majukumu yao.

“Unapotumia isivyotakiwa nje ya taratibu za mtengenezaji unaweza kuongeza mapigo ya moyo na kuhatarisha maisha yako, kuongeza kiwango cha sukari kuwa kikubwa, hivyo matumizi ya insulini ni mengi, utamaliza uliyonayo mwilini mapema kabla ya muda uliokusudiwa,” amesema.

Mugisha ambaye ni daktari bingwa wa upasuaji, amesema ukiona mazingira ya kikodi yanawekwa kwenye mfumo yanaweza yakahamasisha utengenezaji na kisha kuongeza matumizi miongoni mwa jamii.

“Ushauri wetu MAT, energy drinks ni sawa na vinywaji vingine isipotumika vile inavyotakiwa huleta madhara, hivyo pamoja na faida wanayopata wazalishaji na watengenezaji nchini, tunawaomba waangalie na athari zake na watoe elimu kwa jamii,” amesema.

Mtaalamu wa lishe kutoka Shirika la Word Vision, Dk Daudi Gambo amesema kwa kupungua tozo, bei itapungua pia na watu watatumia kirahisi na madhara kiafya yataongezeka.

“Maoni yetu, tunashauri watunga sera waliangalie hili wajadili nini itakuwa athari hasi kupunguza tozo hii. Hili jambo pia limeenda kinyume cha sera ya chakula kwa sababu sera watu wanatakiwa kubanwa wasitumie vinywaji hivyo, kuna madhara mengi kuliko faida,” amesema.

Dk Gambo amesema taasisi za masuala ya uchumi na biashara wataona faida ipo lakini wataalamu wa afya jicho lao linaona tofauti.

Ripoti ya Tanzania Energy Drinks Market 2023 ulionyesha biashara ya vinywaji hivyo nchini inatazamiwa kukua kwa kiwango cha Dola milioni 13.3 za Marekani kati ya mwaka 2023 na 2028.

Ingawa watumiaji hao ni wa rika na sababu mbalimbali, wakuu ni walio na umri wa kati ya miaka 24 na 40. Katika ripoti ya gazeti la Mwananchi mwaka 2023 walitajwa kuwa vijana wanne kati ya tisa hufika Hospitali ya Benjamin Mkapa kila wiki figo zikishindwa kufanya kazi.

Utafiti huo wa mwaka 2023 ulipendekeza matumizi ya energy drink yanaweza kuleta madhara ya mishipa ya moyo kuziba ghafla na hata vifo vya ghafla.

Walionya kuwa mtu asizidishe kikopo kimoja (250mls) cha kinywaji hicho kwa saa 24, wakisisitiza itapendeza zaidi mtu asipokunywa vinywaji hivyo maana matokeo yake hasi hayatabiriki.

Related Posts