Samia amteua Masaju Jaji Mkuu, wadau wataja yanayomsubiri

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amemteua Jaji wa Mahakama ya Rufani, George Masaju kuwa Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania huku wadau wa masuala ya sheria wakizungumzia umahiri wake na mambo yanayomsubiri

Uteuzi huo umetangazwa leo Ijumaa, Juni 13, 2025 kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa na Ofisi ya Rais, Ikulu Chamwino, Dodoma.

Masaju anachukua nafasi ya Profesa Ibrahim Juma ambaye amestaafu rasmi nafasi hiyo ya juu ya uongozi wa Mahakama.

Taarifa hiyo iliyosainiwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Moses Kusiluka imesema Jaji Masaju ataapishwa Jumapili Juni 15, 2025 saa 10 jioni katika Ikulu ya Chamwino, Dodoma.

Kutokana na uteuzi huo, wadau na wabobezi wa sheria nchini wamesema ni mzoefu katika utekelezaji wa masuala ya kisheria na utoaji haki, wakimtaka kujenga mazingira mazuri kuhakikisha mhimili huo unakuwa huru na kimbilio la wananchi wanyonge.

Aprili 5, 2025 jijini Dodoma, Rais Samia alisema hana dhamira ya kugombana na majaji, hivyo amedhamiria kumuacha Jaji Mkuu, Profesa Juma aliyekuwa amebakiza miezi michache, aende kupumzika.

Alisema hayo alipozindua majengo matatu ya makao makuu ya Mahakama Tanzania, Tume ya Utumishi wa Mahakama na nyumba za majaji zilizojengwa katika eneo la Iyumbu, jijini Dodoma.

“Natambua kuwa umebakisha miezi michache kusataafu, na mimi sina tena dhamira ya kugombana na majaji wale, nina dhamira ya kukuacha ukapumzike. Kwa hiyo, majaji jipangeni, jaji huyu anakwenda kupumzika.

“Jaji Mkuu niseme umefanya mageuzi makubwa ya Mahakama yetu. Pamoja na msukumo wa Serikali, lakini mageuzi ya fikra, kusimamia na kuleta mageuzi tunayoyaona leo ni mabadiliko makubwa ndani ya mhimili huu,” alisema.

Juni, 2023 ulizuka mjadala kuhusu kuongezwa muda wa utumishi wa Jaji Mkuu, Profesa Juma ukiibua dosari katika Katiba kuwa vifungu vilivyopo katika Katiba ya sasa ya mwaka 1977 vinaleta mkanganyiko wa kisheria.

Jjambo hilo lilipingwa na wadau wa sheria, akiwemo Jaji wa Mahakama ya Rufani, Stella Mugasha aliyemwandikia barua Mtendaji Mkuu wa Mahakama akieleza kuwa kilichofanywa ni uvunjaji wa Katiba na kutozingatia misingi ya sheria.

Hoja ya Jaji Stella msingi wake ni matakwa ya Katiba ya Tanzania, Ibara ya 120 (1) inayosema: “Kila Jaji wa Mahakama ya Rufani atalazimika kuacha kazi yake atakapotimiza umri wa miaka 65, lakini masharti ya ibara hii ndogo yatatumika bila kuathiri masharti yafuatayo katika ibara hii.

Hata hivyo, uamuzi wa Rais Samia ni kwa mujibu wa Ibara ya 120 (3) ya Katiba ya Tanzania, inayompa mamlaka mkuu wa nchi kumwongezea muda Jaji wa Mahakama ya Rufani hata akifikisha kipindi cha kustaafu, iwapo ataona kuna manufaa ya umma.

Kulingana na Ibara hiyo, “Iwapo Rais ataona aliyetimiza umri wa miaka 65 aendelee kufanya kazi na mhusika akakubali kwa maandishi kuendelea kufanya kazi, Rais anaweza kuagiza aendelee kwa muda wowote atakaoutaja.

Profesa Juma alitimiza miaka 65, Juni 15, 2023 hivyo aliongezea miaka miwili na Rais Samia. Aliteuliwa katika wadhifa huo Septemba 10, 2017 na aliyekuwa Rais wa wakati huo, Dk John Magufuli, baada ya Jaji Mkuu, Mohamed Chande kustaafu akianza kwa kukaimu nafasi hiyo.

Masaju amezaliwa Aprili 7, 1965 katika Kijiji cha Bwai wilayani Musoma mkoani Mara. Baada ya kuhitimu masomo katika ngazi mbalimbali za elimu ikiwamo Chuo Kikuu, aliajiriwa kuwa wakili wa Serikali kuanzia Aprili 1994 na kuendelea kufanya kazi hiyo hadi Oktoba 2006.

Mwaka 2006 hadi 2009 aliteuliwa kuwa Mshauri wa Rais wa Masuala ya Sheria na Oktoba, 2009 aliteuliwa kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, nafasi aliyohudumu hadi Januari 2015 alipoteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Februari mosi 2018, aliteuliwa na hayati Rais John Magufuli kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania. Kabla ya wadhifa huo, Dk Magufuli alimteua kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Aprili 20, 2023, aliteuliwa na Rais Samia kuwa Mshauri wa Rais wa masuala ya sheria hadi Januari 10, mwaka huu alipomteua kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania.

Makamu wa Rais wa Chama cha Mawakili wa Serikali (TPBA), Debora Mcharo amesema Masaju ni kiongozi aliyeshika nyadhifa mbalimbali nchini na mbobevu wa sheria, hivyo wanaamini kazi hiyo ataifanya vizuri na kwa weledi kulingana na miongozo ya kisheria.

“Tupo tayari kushirikiana naye katika kufanikisha utawala wa sheria nchini na kusimamia utoaji haki,” amesema huku akimpongeza.

Mkurugenzi Msaidizi, Madai ya Ndani na Wakili wa Serikali Mkuu, kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Deodatus Nyoni amesema wana imani kubwa na Jaji Masaju kutokana na kuhudumia sekta ya sheria tangu akiwa wakili wa Serikali.

Amesema ni mchapakazi, hivyo Mahakama imepata mtu sahihi wa kuongoza mhimili huo wa utoaji haki.

Wakili Nyoni amesema Jaji Masaju anafahamu mifumo ya mahakama, changamoto na maendeleo ya kidijitali yaliyofikiwa, hivyo ataendeleza yaliyofanywa na mtangulizi wake na kuhakikisha mahakama zote zinafanya vizuri kiutendaji.

Sifa hizo zinaungwa mkono na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi kuwa wanafahamu uzoefu wa kutosha wa Jaji Masaju katika utendaji serikalini.

Mwabukusi amesema kutokana na ubobevu wake katika masuala ya sheria, inampa fursa ya kuongeza uhuru wa mahakama, wa majaji na mahakimu katika kufanya kazi zao kwa namna ambavyo haki itaonekana ikitendeka.

Amesema Mahakama ya Tanzania inasifika na imekuwa chachu ya mabadiliko ya sheria kwa nchi nyingine kutokana na uamuzi uliotolewa wakati Masaju akiwa mwanasheria mkuu wa Serikali, hivyo anaamini wanatambua kiu na hamu ya Watanzania ya kupigania haki zao.

“Tunaomba kwa sasa awekeze nguvu katika utoaji haki, hususani kwenye masuala ya kesi za kikatiba ili imani ya wananchi kwa Mahakama irudi kwa kiwango kikubwa zaidi.

“Sisi kama TLS, tunaahidi kushirikiana kuboresha mifumo ya utoaji haki, kuendeleza mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) iliyowekwa wakati wa uongozi uliopita,” amesema.

Vivyo hivyo, Wakili wa kujitegemea, Stella Rweikiza amesema hana wasiwasi na utendaji kazi wa Jaji Masaju kwa sababu amefanya kazi naye kwa miaka 17, akimwelezea ni mpenda haki na mchapakazi.

Amesema Jaji Masaju ni kiongozi mwenye maono, anayefanya kazi na kila mtu.

“Ni uchaguzi sahihi, tunampongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumuona. Tunaamini ataendeleza yale mazuri yote yaliyoanzishwa na Jaji Mkuu Ibrahim Juma, aliyeanzisha mifumo inayowezesha kesi kuanza na kumalizika kwa muda mfupi,” amesema.

Amesema ubobevu wake katika masuala ya sheria, uongozi na utawala katika usimamizi wa haki jinai na madai, atayaweka sawa kuhakikisha mahakama inaendelea kuaminika.

Kwa upande wake Onesmo Ole Ngurumwa, mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) amesema wanashukuru kupata jaji mkuu mpya ingawa walipaswa kuwa naye miaka miwili iliyopita.

Amesema kwa uzoefu wake wa kuwa kiongozi, wanaamini anaweza kutoa uongozi mzuri katika muhimili huo wa dola.

“Tunategemea kuona mahusiano yakiendelea kuboreka kwa maana ya wadau wote wa mnyororo wa haki nchini. Ili haki iweze kukamilika lazima kuwe na ushirikiano katika mnyororo wa wadau kama asasi za haki za binadamu, wasaidizi wa kisheria, wanasheria na mawakili,” amesema.

Amemtaka ajitahidi kujenga mazingira mazuri ya kuhakikisha mhimili huo unabakia kuwa huru na kuendelea kujenga nchi inayoheshimu mgawanyo wa madaraka kati ya Serikali, Mahakama na Bunge.  

Ameshauri haki kutolewa kwa wakati kwa watu wanyonge na wenye uwezo wowote.

“Mahakama ionekane ndiyo sehemu pekee mtu anaweza kupata haki ya mwisho,” amesema.

Related Posts