Dar es Salaam. Raia wa Watanzania waliopata mafunzo ya ulinzi wa amani yaliyotolewa na Chuo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani Tanzania (TPTC) kwa muda wa wiki moja wamesema mafunzo hayo yamewajenga darasani na kivitendo katika mchakato mzima wa ulinzi wa amani.
Lengo la mafunzo hayo ilikuwa ni kuwaandaa na kuwawezesha raia kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na weledi wanapokuwa kwenye jukumu la ulinzi wa amani ndani na nje ya nchi.
Kozi ya mafunzo hayo yaliyotolewa na Jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ), imetolewa katika Chuo hicho cha Mafunzo kilichopo Kunduchi Dar es Salaam kuanzia Juni 9 hadi leo 13, 2025.
Akizungumza baada ya kupokea cheti wakati wa ufungaji wa kozi hiyo hafla iliyofanyika chuoni hapa, Ofisa Mambo ya Nje Mkuu kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Nice Munissy amesema sasa mafunzo yana tija ukizingatiwa kuwa Wizara hiyo inafanya kazi kwa karibu na JWTZ na jumuiya ya mambo ya nje.
Akifafanua zaidi amesema moja ya majukumu yao ni kuhakikisha wanatekeleza sera ya mambo ya nje ikiwemo kuimarisha ulinzi wa amani ikiwa ni sehemu inayogusa masilahi ya kila mtu.
“Kozi hii imeniimarisha na kunifundisha kwamba sisi raia ambao hatuko kwenye vyombo vya ulinzi na usalama tunaweza kushirikiana pindi linapokuja zoezi la ulinzi wa amani hasa tunapokuwa nje ya nchi.
“Mfano tunapokuwa kwenye misheni namna gani mnaweza kushirikiana. Tumefanyiwa mazoezi. Tumezaliwa Tanzania na kukulia hapa hatujawahi kushuhudia vita tumekuwa tukisikia kwa wenzetu,” amesema Ofisa huyo.
Amesema Tanzania imekuwa ikishiriki michakato ya kusaidia nchi nyingine kupata uhuru, kusuluhisha migogoro na upatanishi, kusaidia nchi zisizo na amani kwa hiyo kozi hiyo ni muhimu kulingana na muktadha huo.
George Ndata, Ofisa Mwandamizi Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki amesema bila amani hakuna siasa wala maendeleo hivyo suala la amani limechukuliwa kuwa la kila raia na si vyombo vya ulinzi pekee.
“Endapo raia anaenda nje kulinda amani anakua anajua hali halisi. Suala hili linaenzi hata waasisi wa nchi yetu ya kusema kwamba kuna umuhimu wa kulinda amani wakiweko raia,” amesema Ndata.
Amesema wote waliopata mafunzo hayo wanaenda kuwa mabalozi wa ulinzi wa amani ndani na nje ya nchi.
Kozi hiyo imefadhiliwa na Serikali ya Japan na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).
Akizungumza mgeni rasmi wa hafla hiyo, Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la Anga, Meja Jenerali Shaban Mani, ameweka bayana mipango ya Chuo cha TPTC kuwa kituo kikubwa cha kikanda katika kufundisha watu wote wanaohitajika kulinda amani.
“Kwenye kulinda amani raia wananafasi yao, kozi hii ya ushirikishwaji wa raia inatupatia uwezo JWTZ na Tanzania kwa ujumla kila tunapoenda kwenye misheni ya ulinzi wa amani tunakua tumekamilika idara zote,” amesema.
Naibu Mwakilishi Mkaazi wa UNDP, John Rutere amesema shirika hilo litaendelea kufanya kazi na Serikali ya Tanzania katika kuhakikisha raia wanapata mafunzo hayo huku akisema hii siyo ya mwisho bali zitaendelea.
“Kozi hii itafanya Tanzania kuwa na walinda amani wengi kwakuwa ni nchi inayokuwa na tunataka iongoze katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini,” amebainisha.
Naye, mwakilishi wa ubalozi wa Japan, Nomura Hiroyuki amesema mafunzo hayo yanatakiwa kuwa endelevu na ndiyo mipango iliyopo.
Mkuu wa Chuo cha TPTC, Brigedia Jenerali George Itang’are amewapongeza wahitimu wote wa mafunzo hayo huku akisisitiza kwenda kuyatumia kwa ufanisi.