Sungusungu Shinyanga waja na kanuni 33 kudhibiti uhalifu

Shinyanga. Jeshi la Jadi Sungusungu Wilaya ya Shinyanga limeweka kanuni 33 zitakazotumika kudhibiti uhalifu kwenye maeneo yao ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku watoto kucheza michezo ya kamali kwa sababu ni chanzo cha wizi.

Hayo yamebainishwa na Katibu wa Sungusungu Wilaya ya Shinyanga, Daudi Ludelengeja leo Juni 13, 2025 wakati wa maadhimisho ya miaka 43 tangu kuanzishwa kwa Sungusungu mwaka 1982 ili kudhibiti vitendo vya uhalifu ukiwemo wizi wa mifugo.

Akisoma kanuni hizo, Ludelengeja amesema zinatakiwa kuzingatiwa ili kukomesha matukio ambayo yanaweza kuwa chanzo cha uhalifu pamoja na kuwadhibiti wanawake ambao hawajaolewa kutokana na baadhi yao kuwa chanzo cha kuleta wahalifu kwenye vijiji.

Amesema watoto watakaobainika wanacheza kamali wataadhibiwa huku wakiwataka wazazi na walezi kutowapatia fedha ambazo zinafanya kuingia kwenye michezo hiyo ambayo inafanya waingie kwevye vitendo vya udogozi na kuwaibia watu.

Mwenyekiti wa Jeshi la Jadi sungusungu Wilaya ya Shinyanga Mabeja Halawa amesema adhabu wanazotoa zinatokana na kanuni na miiko waliyojiwekea kama jeshi la jadi ambapo wamekuwa wakishirikisha Jeshi la polisi pindi wanapokamata wahalifu.

“Tumeshapewa miongozo na Jeshi la Polisi na sasa sungusungu wanazingatia sheria na taratibu na hata vijana, tumewapa elimu juu ya adhabu zinazopaswa kutolewa tofauti na kipindi cha nyuma kwa sasa tunazingatia kanuni,” amesema Halawa.

Kwa upande wake mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Amos Chacha amelitaka jeshi la jadi sungusungu kufanya kazi zao kwa kuzingatia sheria na taratibu na kuepuka kujichukulia sheria mkononi, jambo ambalo ni kinyume na sheria.

Ametumia fursa hiyo pia kuwatahadharisha kujiepusha kutumiwa na wanasiasa ambao badala yake wasimamie miiko yao katika kufanya kazi zao za kuzuia uhalifu na kulinda raia na mali zao kwa kuhakikisha vijiji vyao vinakuwa na utulivu.


Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Iselamagazi, Rosemary Kasabi amesema Sungusungu wamekuwa mstari wa mbele kusimamia miradi ya maendeleo ukiwemo ujenzi wa Kituo cha Polisi Iselamagazi mambo ambayo yanapaswa kuigwa watu wengine.

Related Posts