Ufuta waingizia Tanzania mapato ya Sh300 bilioni mwaka 2024

Morogoro. Tanzania imeingiza kiasi cha Sh300 bilioni baada ya kuuza tani 150,000 za ufuta nje ya nchi kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala kwa mwaka 2024, hatua inayodhihirisha mafanikio ya mfumo huo katika kuongeza mapato ya wakulima na taifa kwa ujumla.

Akizungumza na Mwananchileo Juni 13, 2025 mjini Morogoro, Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Usimamizi wa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala, Asangye Bangu amesema maandalizi ya msimu mpya wa mauzo ya zao hilo yameshaanza kwa kuandaa vikao vya wadau katika mikoa na wilaya zinazolima ufuta ili kujiandaa kwa mauzo ya mwaka 2025.

“Katika msimu wa mwaka 2024, tuliuza tani 150,000 za ufuta nje ya nchi na kuingiza Sh300 bilioni. Mwaka huu tunatarajia kuvuka lengo hilo kwa kuuza kati ya tani 180,000 hadi 200,000, tukilenga kuongeza fedha za kigeni na kuchochea uchumi wa nchi,” amesema Bangu.

Amefafanua kuwa maandalizi ya msimu huu yamehusisha vikao vya wadau kutoka idara za kilimo, vyama vya ushirika, na halmashauri za wilaya mbalimbali kama Morogoro Vijijini, Mvomero, Ifakara, Kilosa, Mlimba, Ulanga na Gairo. Lengo ni kuwaelimisha wakulima kuhusu ubora na usafi wa ufuta kabla ya kuuza kupitia mfumo wa stakabadhi za ghala.

Kwa mujibu wa Bangu, bei ya ufuta msimu uliopita ilikuwa kati ya Sh2,700 hadi Sh3,800 kwa kilo, hali iliyowanufaisha wakulima wengi. Hata hivyo, alionya kuwa mwaka huu bei zinaweza kushuka hadi kati ya Sh2,400 hadi Sh2,500 kwa kilo kutokana na ongezeko la uzalishaji katika soko la dunia.

“Nchi zinazoshindana nasi kwenye soko la kimataifa ni pamoja na Sudan, Nigeria na Pakistan. Hata hivyo, ufuta wa Tanzania una ubora wa hali ya juu unaopendwa kwenye masoko ya China, Japan, Marekani na India,” amesema Bangu.

Mfumo wa stakabadhi za ghala unatekelezwa kwa ushirikiano wa karibu kati ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC), Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB), na Bodi ya Mfumo wa Stakabadhi za Ghala na Soko la Bidhaa Tanzania (TMX).

Mfumo huu huwezesha mazao ya wakulima kukusanywa kupitia vyama vya msingi, kuhifadhiwa kwenye maghala rasmi, na kuuzwa kwa njia ya mnada ambapo wanunuzi hupata taarifa za bei kwa uwazi.

Kwa upande wake, mkulima Asha Abasi kutoka Kijiji cha Mbuga, Wilaya ya Mahenge amesema kuwa ingawa mfumo huu unasaidia kupunguza unyonyaji kutoka kwa madalali, bei ya mwaka huu ni ya chini ikilinganishwa na miaka iliyopita.

“Ningependa mfumo huu uendelee, lakini bei ipande hadi kati ya Sh2,800 na Sh3,000 kwa kilo ili mkulima apate faida na alipwe kwa wakati,” alisema Asha.

Meneja Mkuu wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Wakulima Mkoa wa Morogoro (MOFACU), Andrewa Mabellah amesema mfumo wa stakabadhi za ghala umeleta mabadiliko makubwa katika maisha ya wakulima. Alieleza kuwa mkoa wa Morogoro una zaidi ya wakulima 4,000 wa ufuta waliounganishwa kupitia vyama vya ushirika 32, ambavyo pia vinajishughulisha na uzalishaji wa kakao na mbaazi.

“Tangu mwaka 2021, wakulima wameanza kuona faida ya kilimo. Serikali ilipoanzisha mfumo huu, madalali waliondolewa na sasa wakulima wanauza moja kwa moja kwa wanunuzi wakubwa,” amesema Mabellah.

Ametoa mifano ya bei zilizoongezeka kupitia mfumo huo: mwaka 2021, kilo moja ya kakao iliuza kwa Sh39,000, tofauti na zamani ambapo ilikuwa Sh4,000. Mwaka 2022, kilo ya ufuta iliuza kwa Sh3,500 badala ya Sh1,000 hadi Sh1,500 kabla ya mfumo huo. Kwa upande wa mbaazi, mwaka 2023, kilo moja iliuza kati ya Sh3,500 hadi Sh4,000 ikilinganishwa na Sh500 hadi Sh1,000 hapo awali.

Mabellah amesema mfumo huu si tu umeongeza kipato kwa wakulima, bali pia umeongeza uwazi, ufanisi wa masoko, na usalama wa mali ya mkulima hadi muda wa malipo.

Wadau mbalimbali wameshauri Serikali kuendeleza mfumo huu kwa mazao mengine muhimu ya kimkakati ili kuongeza mapato kwa wakulima na taifa kwa ujumla, hasa katika kipindi hiki ambacho nchi inaendelea kusaka fedha za kigeni na kuimarisha uchumi wa ndani.

Related Posts