Mbunge ahoji sababu uchumi wa wananchi Kagera uko chini, Serikali yajibu

Dodoma. Mbunge wa Viti Maalum Bernadetha Mushashu ameshangaa kwa nini Mkoa wa Kagera kila wakati unatajwa kuwa ni masikini.

Bernadetha ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Juni 13, 2025 kwenye mdahalo wa uchambuzi wa Bajeti 2025 uliowakutanisha wabunge na wataalamu wa Mipango na Uchumi.

Mdahalo huo umekuja kwa mara ya kwanza katika mfumo wa kibunge ambapo wabunge mbali na kujadili Bajeti, lakini wamehoji kwa nini uchumi wa watu haukui kama inavyotajwa.

“Kagera kuna maghorofa makubwa, maisha mazuri na jinsi watu walivyojipanga lakini nashangaa kusiki eti kila wakati iko chini kwenye masuala ya uchumi,” amehoji Mushashu.

Mbunge huyo ametaka kujua vigezo ambavyo hutumiwa na wataalamu katika kuainisha umasikini wa Watanzania bila kufanya utafiti.

Kwa mujibu wa Mbunge huyo, huenda iko Mikoa ambayo inaonekana wazi kwamba ipo chini zaidi ya Kagera lakini kwenye mpangilio inaonekana kuwa juu.

Ametaja utafiti ukafanyike upya ili kubaini kinachoelezwa kama kuna uhalisia au imekuwa ni utaratibu wa kuandika tu.

Katika hatua nyingine Mbunge huyo amehoji kwa nini Serikali inashindwa kudhibiti riba kubwa zinazotozwa na Taasisi za fedha kwa kuwa ni chanzo Kikuu cha kuwafanya wawe masikini.

Mushashu amesema kama riba zitapungua na kutozwa kwa utaratibu wa Benki Kuu, watu wa kipato cha chini wataibuka kuwa na uwezo mzuri kwani watazalisha na kupata faida.

Akijibu kuhusu umasikini wa Kagera, Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Dk Fred Msemwa ametaja kinachoishusha Kagera katika kipimo cha umasikini ni Wilaya ya Biharamulo ambayo ilikuwa na kiwango kikubwa cha umasikini.

Dk Msemwa amesema hali ya sasa ni tofauti kwa kuwa Wilaya hiyo imekuwa kiuchumi na hivyo wanaamini taarifa za sasa zitakuwa tofauti.

Related Posts