Dar es Salaam. Taka bado ni mwiba inaoitesa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo mkoani Dar es Salaam, huku mambo matatu yakitajwa kuwa vikwazo vya kuzitokomeza.
Akizungumza leo Jumamosi Juni 14, 2025, kwenye maadhimisho ya siku ya mazingira yaliyofanyika kimkoa katika Shule ya Msingi Makuburi, Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti Taka na Usafishaji Manispaa ya Ubungo, Lawi Bernard amesema manispaa ya Ubungo inakusanya tani 890 za taka kwa siku huku tani 453 sawa na asilimia 51 pekee ndizo hufikishwa dampo la Pugu Kinyamwezi huku nyingine zikisalia mitaani.
Ametaja dhana potofu ya jamii kuhusu taka, gharama kubwa ya ukusanyaji na uchakataji wake na miundombinu hafifu kuwa vikwazo vinavyokwamisha ukusanyaji na uchakataji wa taka katika manispaa hiyo.
“Taka ni kitu kisichofaa, mtu akishaona ni takataka anazisukuma tu mitaani huko lakini wangeitambua thamani ya taka na kujua kuzitenganisha, wangetusaidia kuzikabili na kunufaika nazo.”
Amesema kiwango kikubwa cha taka (zaidi ya tani 470) kinachozalishwa Ubungo kila mwezi kinaweza kudhibitiwa kwa kuongezewa thamani, hata hivyo, kutokana na jamii kukosa elimu inashindwa hata kubadili taka rejeshi kuwa mbolea na chakula cha mifugo.

Amesema miongoni mwa jitihada zinazofanyika kutokomeza taka ni pamoja na ujenzi wa vituo vitatu vya ukusanyaji wa taka na uchakataji wake kikiwemo cha eneo la Simu 2000, Kibamba na Goba ambavyo vinatarajiwa kuanza kufanya kazi rasmi Agosti, mwaka huu.
“Tumeanza kutoa elimu ya namna ya kutenganisha na kuhifadhi taka kwa jamii na kisha kuziuza kwa kampuni zinazozikusanya na kuzichakata. Hata hatua ya upanuzi wa barabara sasa unaweza kutusaidia kufika hadi maeneo yasiyofikika kwa urahisi,” amesema Bernard.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha Mazingira Mkoa wa Manispaa ya Ubungo, Nice Vahaye, uwepo wa taka katika mazingira unahatarisha afya ya jamii, kuchafua vyanzo vya maji na kuchochea mabadiliko ya tabianchi.
“Kama taka zisipokusanywa na kushughulikiwa ipasavyo athari zake zinaenda kwenye vyanzo vya maji, zinachafua mazingira na ni chanzo cha magonjwa ya mlipuko na kuchochea mabadiliko ya tabianchi. Jamii isipozikabili taka, kizazi cha kesho kitakosa mahala salama pa kuishi,” amesema Vahaye.
Akizungumzia uchakataji wa taka, Ofisa Afya wa Kampuni ya Kajenjele Trading Company, Dk Patrick Chibwana amesema taka zikikusanywa na kuchakatwa ipasavyo zinaweza kugeuka lulu na chanzo cha kipato kwa jamii.
Akitolea mfano taka rejeshi, Chibwana amesema mabaki ya mbogamboga na matunda yasiyo na asidi yanaweza kutumika kuzalisha nzi chuma (Black Soldier Fly) ambao ni chakula cha mifugo kama nguruwe, samaki, mbuzi, kuku na mbwa huku mabaki yake yakitengeneza mbolea.
“Taka nyingine zinaweza kutumika kutengeneza biogas (gesi asilia) ambapo kama mtu ana mtambo wa kuzalisha biogesi, kilo 40 inapika chakula siku 14 bila kukata. Wakati unaendelea kupika unaendelea kuchakata taka ama kusindika gesi yako,” amesema Chibwana.
Kuhusu taka za plastiki, Chibwana amesema zinaweza kuchakatwa kwenye vipande vidogo vitakavyouzwa kwenye viwanda vinavyozalisha bidhaa za plastiki na mifupa kuzalisha bidhaa nyingine na kuipatia jamii fedha.
Akitoa maelekezo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando ameziagiza kampuni zinazokusanya taka kuzikusanya kwa wakati na kuzishughulikia kama mkataba unavyoelekeza.
Amesema Dar es Salaam inakusanya wastani wa tani 5,000 za taka kwa siku huku uwezo wa kuchakata wa mkoa huo ukiwa hauzidi asilimia 50, yaani tani 2,500.
“Naziagiza mamlaka na idara zinazohusika kutoa elimu kwa umma kuhusu namna sahihi ya kuhifadhi na kutenganisha taka ili iweze kutumika kama chanzo cha kipato lakini pia kulinda mazingira yetu,” amesema Msando.