Dar es Salaam. Familia ya wanandoa waliokutwa wamefariki dunia chumbani kwao eneo la Tabata Bonyokwa Gk, wilayani Ilala jijini Dar es Salaam wameruhusiwa na Jeshi la Polisi kuchukua miili ya marehemu hao kwa ajili ya kuendelea na taratibu zingine.
Vifo vya wanandoa hao Antony Ngaboli (46) na Anna Amiri (39) vimetokea usiku wa kuamkia Juni 12, 2025 katika makazi yao.
Akizungumza na Mwananchi leo Juni 14,2025 msemaji wa familia hiyo, Nuhu Msangi amesema wanatarajia kuchukua miili ya marehemu hao Jumatatu kwa ajili ya kuendelea na taratibu nyingine za maziko.
“Hatujakabidhiwa rasmi miili hiyo ila tumeruhusiwa kuichukua na kuendelea na taratibu zingine.”
Awali, Msangi alisema wanatarajia kuipumzisha miili ya wanandoa hao katika makazi yao ya milele kwenye Kijiji cha Ngulu Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro siku ya Jumatano Juni 18,2025.
“Ibada ya kuwaaga marehemu hawa inatarajiwa kufanyika siku ya Jumanne na kisha kuanza safari ya kwenda Kilimanjaro,” amesema.
Amesema marehemu hao watazikwa eneo moja kwa kuwa walikuwa wanandoa.
“Kwa mujibu wa mila zetu mwanamke akiolewa anakuwa wa kwetu, hivyo Ally na mkewe watazikwa katika eneo moja,”ameeleza.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Juni 12,2025 na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro ameeleza kuwa miili ya wanandoa hao imekutwa ndani ya chumba chao ikiwa na majeraha.
Akizungumza na Mwananchi leo Juni 14,2025 kwa njia ya simu Muliro amesema kuwa uchunguzi wa tukio hilo unaendelea. “Upelelezi kuhusu vifo vya wanandoa hao bado unaendelea.”