Arusha. Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Namelok Sokoine, amewataka viongozi na wanachama wa CCM mkoani Arusha kuwa mstari wa mbele kujibu kwa hoja maudhui ya kejeli dhidi ya Rais Samia Suluhu Hassan yanayosambazwa kwenye mitandao ya kijamii.
Namelok amesema hayo leo Juni 14, 2025, jijini Arusha, wakati wa mapokezi ya kumkaribisha nyumbani kwa cheo kipya, baada ya kuteuliwa Mei 28, 2025 na Rais Samia kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa.
“Halafu nawauliza, hivi hamuoni jinsi Rais wetu anavyotukanwa kwenye mitandao ya kijamii na baadhi ya watu? Nataka Mkoa wa Arusha uwe wa kwanza kukemea. Anzeni sasa kuwaambia watu mambo makubwa na mazuri anayoyafanya mama yetu.”
Pia, Namelok amewataka wajumbe wa kamati za maamuzi kutumia uwezo wao kikamilifu katika kuchuja wagombea wa nafasi mbalimbali watakaokata rufaa katika uchaguzi ujao.
Amesema kuwa fursa ya wajumbe kuamua wagombea ni dhamana kubwa, hivyo haipaswi kutumika vibaya kwa kuumizana au kulipizana kisasi.
“Badala yake, wajumbe wanapaswa kuwapitisha wagombea wenye uwezo wa kushinda na kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, wakihudumia wananchi na kutatua kero zao kwa wakati unaofaa,” amesema.
Akiwashukuru viongozi na wanachama wa CCM waliojitokeza kumpokea na kumpongeza, Namelok amesema ataitumia nafasi hiyo kwa uaminifu na bidii katika kukijenga na kukiimarisha chama, kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo.
“Tunapoelekea katika uchaguzi huu, naomba tuwe na mwelekeo mmoja. Wajumbe wenzangu katika ngazi mbalimbali za maamuzi, tukatende haki, tusiutumie wadhifa huu kwa ajili ya kuumizana au kuwakandamiza wasio sehemu ya vikao hivi. Tuwe waadilifu, tuepuke upendeleo, na tuwazingatie wagombea wenye uwezo wa kushinda na kutumikia wananchi kwa ufanisi,” amesema.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amewataka wana-CCM kuwa wamoja na kushikamana nchi inapoelekea kwenye uchaguzi ili kukibakisha chama salama kwa ajili ya kizazi kijacho.
Awali, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Thomas Ole Sabaya amesema wana kila sababu ya kumpongeza Namelok kupata nafasi hiyo ya kuwa kwenye timu ya watu 28 wa kutoa mapemdekezo na mwelekeo wa kimaamuzi ndani ya CCM na Serikali kwa ujumla.
“Hii ni ‘surprise’ kubwa Rais ametufanyia, tuna kila sababu ya kumshukuru sana kwani imeonesha hatukufanya maamuzi mabaya ya kumchagua kuwa mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM Mkoa mwaka 2023,” amesema.
Amemtaka Namelok kuhakikisha anafanya kazi ndani ya matarajio ya Rais kumpatia nafasi hiyo akianza na uchaguzi wa mwaka huu unaotarajia kufanyika Oktoba, 2025.