Maeneo ya kipaumbele ya programu ya kizazi chenye usawa yatajwa

Dodoma. Wakati Programu ya Kizazi chenye Usawa (GEF), ikiendelea kutekelezwa nchini, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Malumu  imetaja maeneo manne yaliyopewa kipaumbele ikiwamo kazi zenye staha kwa wanawake katika sekta isiyo rasmi.

Maeneo mengine ni uwezeshaji wa kijinsia kwenye sekta binafsi, upatikanaji wa rasilimali za uzalishaji kwa wanawake na ubunifu na utekelezaji wa miradi ya kiuchumi kwa wanawake.

Katika kufuatilia na kushauri kuhusu maendeleo ya utekelezaji wa jukwaa hilo, Desemba 2021 Rais Samia Suluhu Hassan alianzisha Kamati ya Kitaifa ya Ushauri (GEF).

Akizungumza katika kikao cha kuwajengea uwezo maofisa habari kuhusu utekekelezaji wa programu hiyo Juni 14,2025, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum,  Merkion Ndofi, amesema Serikali inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika utekelezaji wa maeneo manne hayo ya  kipaumbele.

Amesema maofisa hao ni wadau muhimu wa katika maeneo yao kwa kuwa ni wasemaji wa miradi mbalimbali ya Serikali.

Ndogi amesema anaamini kupitia wao, taarifa na maendeleo ya utekelezaji wa  Programu ya Kizazi Chenye Usawa zitasambaa, kufahamika zaidi kwa jamii na kusaidia utekelezaji wa haki na usawa wa kiuchumi nchini.

“Programu hii imekuwepo kwa muda mrefu na sasa inatimiza miaka mitano. Rais Samia Suluhu Hassan, alishiriki Mkutano wa Kizazi cha Usawa uliofanyika Paris (nchini Ufaransa) na akaahidi kuwa kinara katika kutekeleza haki na usawa wa kiuchumi,” amesema  Ndofi.

Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jinsia, Badru Abdnoor, amewataka maofisa habari kupaza sauti kuhusu program hiyo ili jamii ifahamu fursa zilizopo na kuweza kushiriki kikamilifu.

Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Juliana Kibonde amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango wa maofisa habari na ndiyo sababu imeamua kuwakutanisha ili kujadiliana kwa pamoja kuhusu namna bora ya kuitangaza programu hiyo kwa ufanisi.

Related Posts