Mwanza. Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando imesema kumekuwa na ongezeko la wagonjwa wa saratani wanaohitaji matibabu lakini wanashindwa kumudu gharama.
Hali hiyo imeweka hospitali katika mazingira ya kutoa misamaha mara kwa mara kwa wagonjwa hao, ili kuhakikisha wanapata huduma stahiki.
Katika jitihada za kutafuta suluhisho la kudumu la changamoto hiyo, Hospitali ya Bugando imeanzisha mbio za hisani za ‘Bugando Health Marathon Season 2’, zenye lengo la kukusanya Sh1 bilioni, ili kugharamia matibabu ya wagonjwa wa saratani wasiojiweza kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Mbio hizo za kilometa 2.5, 5, 10, na 21 zitakazofanyika zimezinduliwa rasmi leo Jumamosi, Juni 14, 2025, huku kilele cha tukio hicho kikitarajiwa kuwa Agosti 3, mwaka huu katika viwanja vya Bugando, mgani rasmi akiwa Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete.
Mbio hizo zenye kaulimbiu ya “Kimbia, Changia Matibabu ya Saratani” zimezinduliwa rasmi leo na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda.
Katika hafla hiyo, washiriki zaidi ya 300 wamekimbia kilometa tano na kufanikisha mazoezi mepesi kama sehemu ya maandalizi ya mbio hizo.
Akizungumza leo Juni 14, 2025, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa hospitali hiyo, Dk Bahati Wajanga, amesema mwaka 2024 hospitali hiyo ilisamehe Sh1.2 bilioni kwa wagonjwa wenye ugonjwa wa saratani, jambo ambalo limekuwa mzigo mkubwa kwa taasisi.
Amesema msimu wa kwanza walikusanya zaidi ya Sh222.4 milioni zilizotumika kusaidia matibabu ya saratani kwa watoto 153 kutoka familia duni na kupata vifaa vyenye thamani ya Sh77 milioni vilivyotumika kwenye matibabu hayo.
Dk Wajanga amesema kiasi hicho kitapatikana kupitia ada ya usajili Sh35, 000 kwa kila mshiriki na michango ya wadau wakilenga kusajili washiriki zaidi ya 2,500.
“Wazo la kusajili mbio hizi lilianza baada ya kubaini ongezeko kubwa la misamaha ya wagonjwa wanaotibiwa na kushindwa kumudu gharama za matibabu” amesema Dk Wajanga.
Mtanda amesema ongezeko hilo la wagonjwa wa Saratani limekuwa kubwa tangu hospitali hiyo ilivyoanza matibabu ya ugonjwa huo mwaka 2019, ambapo amewataka wananchi kuungana kusaidia wagonjwa ili watibiwe warudi kusaidia maendeleo ya taifa.
Mtanda ameahidi kuchangia Sh5 milioni kuunga mkono jitihada za hospitali hiyo kurejesha tabasamu kwa Watanzania ambao wamegundulika kuwa na tatizo hilo.
Shujaa wa Saratani, Said Mandingo ‘Babuu wa Kitaa’, amewashauri wananchi kuacha kasumba ya kukimbilia kwenye tiba za kienyeji ambako wanapoteza maisha na badala yake wajenge utamaduni wa kupima afya zao kila mara ili kuwahi matibabu.
“Kama kijana niliyepambana nikapokea hali ya saratani nikaanza matibabu na kupona, nawasihi wagonjwa unapojigundua kuwa na maambukizi haya, usikate tamaa kubali hali hiyo na uanze matibabu mapema,” amesema.
Mmoja wa washiriki wa mbio hizo kutoka Bugando Fitness, Christina Urio amesema: “Watu wengi wanasumbuliwa na ugonjwa huu, hivyo hamasa kama hii inavuta jamii kushiriki moja kwa moja kugusa jamii na wagonjwa kupata matibabu ambayo ni gharama sana.”