Dar es Salaam. Watanzania wamehamasishwa kuwa na moyo pamoja na utamaduni wa kujitolea damu bila kusubiri siku rasmi za kitaifa ama kimataifa, Ili kuokoa maisha ya Watanzania wenzao wenye uhitaji wa damu hospitalini.
Hayo yamesemwa mwishoni mwa wiki na Mkuu wa Kitengo cha Maabara katika Hospitali ya Aga Khan, Dk Caroline Ngimba katika tukio la uchangiaji damu lililoandaliwa na hospitali hiyo kwa kushirikiana na Benki ya DCB, kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wachangia Damu Duniani, hospitalini hapo, Dar es Salaam.
“Uzuri ukichangia damu kama afya inaruhusu kila baada ya miezi mitatu unaweza kuchangia tena, tungeomba tabia hii iwe endelevu kwani hakuna kiwanda cha kutengeneza damu, damu inayopewa mwanadamu inatoka kwa mwanadamu.
“Kuna uhitaji mkubwa wa damu hospitalini, sisi watu wa hospitali tunajua jinsi tunavyopata shida ya damu katika mahitaji tofauti, mfano wanaojifungua, watu waliopata ajali na wagonjwa mbalimbali,” amesema Dk Caroline akitoa shukurani kwa wafanyakazi hao pamoja na wadau wengine waliofika hospitalini hapo kuchangia damu.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa DCB, Sabasaba Moshingi alisema benki yao itaendelea kufanya jitihada tofauti katika kusaidia afya za Watanzania wenye uhitaji wa kupata damu kutokana na kukabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo magonjwa na ajali.
“Leo tumeamua kushirikiana na Aga Khan na kuja kujitolea damu kwani licha ya kuwa benki yetu hujishughulisha na utoaji wa huduma za kifedha, lakini pia tunaona kuna umuhimu wa kuhakikisha Watanzania wanaohitaji damu salama hospitalini wanazipata bila kuwa na haja ya kusubiria ndugu waje kujitolea.”
“Leo tupo hapa pamoja na washirika wenzetu hospitali ya Aga Khan kwa lengo la kuchangia damu, tutaendelea kushiriki matukio mengine kama haya na mengineyo yenye lengo la kusaidia kuokoa maisha ya Watanzania wenzetu wenye uhitaji wa damu na mahitaji mengine ya kibinadamu,” amesema Moshingi.

Naye mtaalamu wa utoaji damu kutoka Mpango wa Taifa wa Damu Salama, Peter Chami ameishukuru benki hiyo huku akizitaka taasisi nyingine kuiga mfano huo ili kuokoa maisha ya Watanzania wenye shida ya damu, kwani mahitaji ni makubwa sana.
Katika hafla hiyo jumla ya uniti 44 zilipatikana kutoka kwa wafanyakazi hao pamoja na watu wengi waliojitokeza kushiriki hatua hiyo.
Amani Mbwambo, mkazi wa Dar es Salaam akizungumzia hilo amesema ni jambo la muhimu kuchangia damu hata kama si siku mahususi bali ukifanya hivyo kwa hiari yako unaokoa maisha ya wengi.
“Mimi binafsi nilizoea kuchangia damu shuleni kipindi nasoma na nimekuwa nikiendelea na utaratibu huo hadi leo hii. Nawashauri na wenzangu hasa vijana kuwa na mazoea ya namna hii,” ameshauri.