Uhaba wa wataalamu Uzi, wajawazito wajifungulia kwenye boti

Unguja. Wanawake wa kisiwa cha Uzi, Mkoa wa Kusini Unguja wameendelea kuiangukia Serikali kuhakikisha kituo cha afya kilichojengwa katika eneo hilo kinapata wataalamu wa afya, ili kuwaondolea mateso ya kujifungulia katika mazingira hatarishi, ikiwamo kwenye boti wakati wakisafirishwa kwenda maeneo mengine kupata huduma hiyo.

Licha ya kuwepo kwa kituo hicho cha afya kilichojengwa mwaka 2023 kwa msaada wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), wajawazito kutoka visiwa vya Uzi na Ng’ambwa bado wanakabiliwa na adha kubwa kutokana na ukosefu wa madaktari na wauguzi.

Akizungumza na Mwananchi iliyofika kisiwani huko jana Jumamosi Juni 14, 2025, Furaha Yassin, mkazi wa Uzi, amesema baada ya kituo kujengwa walitegemea kuwa changamoto iliyokuwa inawakabili wanaotaka +kujifungua na watoto itapungua, lakini hali imeendelea kuwa mbaya.

Amesema kuna wajawazito wanaolazimika kujifungulia kwenye boti kutokana na ukosefu wa huduma za haraka.

“Kituo kilijengwa kwa matumaini, lakini sasa ni kama pambo tu. Hatuna wataalamu na wanawake tunaendelea kuteseka,” amesema.


Mwananchi mwingine, Mwantaga Ramadhani, amesema licha ya jengo kuwa kubwa na la kisasa, bado linaonekana kutokuwa na maana kwao kwa sababu hakuna huduma muhimu. Mwantaga amedai kuwa mara kadhaa wanawake huzalia njiani wakisafirishwa kwenda hospitali nyingine, jambo analolitaja kuwa ni hatari na unyanyasaji wa kijinsia.

Mwanaamisi Khamis Yahya, mkazi mwingine wa eneo hilo, ameiambia Mwananchi kuwa hivi karibuni kuna mjamzito alimpoteza mtoto wake baada ya kukosa msaada wa haraka wakati wa kujifungua.

“Yule mama mtoto wake alifia tumboni kwa sababu alikosa usafiri wa boti usiku na hata hakukuwa pia na muuguzi wala mganga, basi akashindwa kuzaa mtoto akafia tumboni,” amedai Mwanaamisi.

Mkazi mwingine kisiwani humo Omar Mohamed Haji amesema licha ya mabadiliko ya miundombinu ya kituo hicho yaliyofanyika mara kadhaa, huduma bado hazijaimarika kutokana na ukosefu wa vifaa na wataalamu.

“Hali inatufanya tuwapeleke wake zetu kufuata huduma kule Kitogani, ni mbali kutoka hapa,” amesema.

Sheha wa Shehia ya Uzi, Othman Mwinyi Haji, amekiri kuwapo kwa changamoto hizo.

Amesema kito hicho kinahitaji huduma za afya kwa saa 24 pamoja na upatikanaji wa maji, ambao nao ni changamoto baada ya miundombinu ya maji kuondolewa wakati wa ujenzi wa barabara.

Amesema kwa sasa wapo katika mpango wa kuchimba kisima ili kukabiliana na tatizo hilo.

Akizungumzia kero hiyo, Mkurugenzi wa Kinga kutoka Wizara ya Afya, Dk Salim Slim pia amekiri kwamba wana uhaba wa wataalamu lakini akabainisha kuwa Serikali inafanya juhudi za kuhakikisha upatikanaji wa watumishi katika vituo mbalimbali, kikiwemo cha Uzi unatekelezwa kwa haraka.

Mkurugenzi Kinga wizara ya afya, Dk Slim Salim akizungumza kuhusu changamoto za ukosefu wa wataalamu kituo cha afya Uzi na Mipango ya Serikali wizarani hapo. Picha na Jesse Mikofu



Amesema tayari kibali cha ajira kimetolewa na kituo hicho ni miongoni mwa vitakavyopewa kipaumbele.

Kuhusu maji, Dk Slim amesema kampuni ya Direct Aid imekubali kushirikiana na Serikali kujenga miundombinu ya maji kuanzia mwezi ujao.

Aidha, Waziri wa Afya, Nassor Ahmed Mazrui, akizungumza kwenye Baraza la Wawakilishi wiki iliyopita, alisema uhaba wa wataalamu ni changamoto kubwa na juhudi zinafanyika waongeza kupitia ajira za Serikali na sekta binafsi.

Amesema kwa mwaka 2025/26, wizara imeidhinishiwa bajeti ya Sh368.150 bilioni, sehemu ya fedha hizo zitatumika kuboresha huduma katika vituo mbalimbali kikiwamo cha Uzi.

Kituo hicho kinahudumia watu 4,233 kati yao, wanawake ni 2,081.

Related Posts