Vijana Moshi wachangamkia supu ya pweza, daktari aeleza faida

Moshi. Supu ya pweza inayotumika sana mikoa ya pwani, sasa imefika bara katika mji wa Moshi mkoani Kilimanjaro na kujipatia watumiaji wengi huku ikihusishwa na kuongeza nguvu za kiume.

Vijana wa kiume wamekuwa watumiaji wakubwa wa supu ya pweza ambao baadhi yao wanatumia kwa lengo la kuongeza nguvu za kiume na baadhi yao wamethibitisha imewasaidia.

Kwa mujibu wa mtaalamu wa lishe, pweza ana virutubisho mbalimbali vinavyoweza kuchangia afya ya uzazi kwa wanaume, jambo linalotajwa kuwa mojawapo ya sababu ya kupendwa kwa supu yake.

Hata hivyo, Mwananchi imepita eneo la stendi kuu ya mabasi Moshi Mjini na kushuhudia idadi kubwa ya vijana wakiwa katika vibanda vinavyouza supu hiyo kwa Sh1,000 huku vipande wa pweza vikiuzwa kwa Sh300hadi Sh200 kutegemea kwa ukubwa wa kipande.

Mteja akichukua kipande cha pweza kwa kutumia kijiti kwenye kopo  maalum la kuwekea pweza hao.



Kwa mujibu wa baadhi ya wauzaji wa supu hiyo, idadi ya wateja hasa wa kiume, imeongezeka kwa kasi, wengi wao wakiamini ina faida za kiafya, hususani katika kuongeza hamasa na uwezo wa tendo la ndoa.

Mmoja wa watumiaji wa bidhaa hiyo, Leonard Tesha amasema supu ya pweza ni nzuri mwilini hasa kwa mwanamume kwa kuwa inaufanya mwili kujisikia vizuri wakati wote.

“Napenda kunywa supu ya pweza kwa sababu kama mwanamume inaufanya mwili wangu kuwa sawa hata nikiwa na mama watoto wangu, siwezi kudhalilika maana muda wote nipo timamu,” amesema Tesha.

Wakizungumza na Mwananchi, baadhi ya wananchi wa Moshi mjini wamesema sasa hivi imefika mahali kila kijana anatamani kujaribu kile anachoelezwa kinasaidia kuimarisha nguvu za kiume kutokana na mtindo wa maisha.

Francis Peter amesema vijana wa sasa kutokana na mtindo wa maisha wanaoishi wamekuwa wakiishi kwa majaribio wakiamini kila kitu wanachojaribu kitawasaidia na kwamba ndio sababu kubwa ya kukimbilia kwenye pweza.

“Vijana wengi wanashindwa kumudu tendo la ndoa, hivyo wanalazimika kutumia mbinu mbadala kujiweka sawa wakiamini watapata nguvu,” amesema Peter.

Kwa upande wake, Joseph Sillas amesema: “Vijana wengi wanatumia supu ya pweza wakiamini ni suluhisho kwenye tendo la ndoa, kwa hiyo matatizo yanapowakuta na wanaposikia tetesi kwamba ukinywa supu ya pweza unaongeza hiki na hiki na mambo yanakuwa mazuri.

 “Vijana wengi siku hizi wanakula chips au tambi unafikiri watapata wapi nguvu za kiume, vijana wa zamani ndio walikuwa na nguvu kuliko vijana wa sasa hivi kwasababu wao walijitunza kwa kula vyakula vyenye lishe bora.”

Mmoja wa wafanyabiashara wa pweza akimimina supu ya pweza kwa mteja eneo la pembezoni mwa stendi kuu ya mabasi mjini Moshi.Picha na Janeth Joseph



Miongoni mwa wafanyabiashara wanaouza supu hiyo, Mariam Salim amesema biashara yake imekuwa ikikua kwa kasi kutokana na mahitaji makubwa kutoka kwa vijana.

“Kila jioni vijana wanajaa hapa kunywa supu, wanasema inawapa nguvu na inawafanya wajisikie vizuri, mimi mwenyewe nafurahia kuona biashara inakuwa na vijana wanakuwa na afya njema,” amesema Mariam.

Pia, amesema supu hiyo huuza Sh1,000 na vipande vya pweza huuza kati ya Sh200 hadi Sh 300 kulingana na mahitaji ya mteja.

Akizungumzia kuhusu faida za pweza, daktari wa tiba ya chakula kutoka hospitali ya KCMC, Japhari Mwijae amesema pweza ni moja ya viumbe wa baharini ambavyo vina protini nyingi inayoitwa ‘arginine.’

Amesema protini hiyo huwa ina kichocheo mwilini na huwa inatoa kemikali inayoitwa ‘nitric oxide’ inayosaidia kupanua mishipa ya damu, kuboresha mtiririko wa damu na kuimarisha nguvu za kiume kupitia mzunguko wa damu.

Dk Mwijae amesema unywaji wa supu ya pweza mara kwa mara, pia unasaidia mzunguko wa damu kuwa mzuri na kwenda kwenye ubungo na sehemu nyingine za moyo.

“Pweza ana madini ya zinki yanayoingia kwenye mwili na inachochea utengenezwaji wa homoni ya ‘testosterone’ ambayo ndio inamfanya mwanamume kuwa na nguvu na hamu ya tendo la ndoa,” amesema Dk Mwijae.

Pia, amesema madini ya zinki yanasaidia kulinda mbegu za mwanamume na kuimarisha nguvu za kiume kwa hali ya ubora, kiasi cha ujazo wake hadi kulifikia yai la kike.

Dk Mwijae amesema pweza anaweza kuwa na mchango mzuri katika afya ya mwanamume kwa jumla kutokana na virutubisho alivyonavyo, lakini si tiba ya moja kwa moja ya kuongeza nguvu za kiume.

Related Posts