Lusaka. Aliyekuwa Rais wa Zambia, Edgar Lungu ambaye alifariki dunia juma lililopita nchini Afrika Kusini, aliacha ujumbe kwamba mrithi wake ambaye ni Rais wa sasa Hakainde Hichilema asisogelee mwili wake.
Lungu alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 68, kwa ugonjwa ambao haukutajwa. Rais huyo wa zamani aliiongoza Zambia kwa miaka sita kuanzia mwaka 2015 na kushindwa katika uchaguzi ambao wananchi walimchagua rais wa sasa, Hakainde Hichilema kwa kura nyingi.
Baada ya kushindwa katika uchaguzi huo, alijiondoa kwenye siasa lakini baadaye akarejea na kuonekana kuwa na nia ya kugombea tena urais.
Kwa mujibu wa BBC na Africa News zikinukuu taarifa ya familia, Lungu aliacha maelekezo ya kwamba mrithi wake Hichilema hapaswi kuwa karibu na mwili wake huku akitaka maziko yake yawe ya faragha.
Hata hivyo, kumekuwepo sintofahamu juu ya mazishi ingawa Serikali ilikuwa imepanga kurudisha mwili wake nyumbani Jumatano iliyopita, lakini ilishindwa kufanya hivyo kutokana na mzozo na familia ya Lungu na chama chake cha kisiasa, Patriotic Front (PF), kuhusu maombolezo na mipango ya mazishi.
Viongozi hao wawili walikuwa wapinzani wa kisiasa kwa muda mrefu, kabla ya Hichilema kushinda wadhifa huo.
Katika hotuba kwa Wazambia Alhamisi jioni, Rais Hichilema hakurejelea moja kwa moja matakwa hayo, lakini alisisitiza wito wa amani, upendo na umoja katika wakati huu wa huzuni.
Katika hatua nyingine, Chama cha PF kilidai kuwa Lungu alipigwa marufuku kuondoka nchini kwa miaka kadhaa na kama angeruhusiwa kusafiri kutafuta matibabu mapema pengine angekuwa hai ingawa Serikali imekanusha madai hayo.
Msemaji wa familia ya Lungu, wakili Makebi Zulu, hapo awali aliiambia BBC kwamba familia haikupinga mazishi ya kitaifa, lakini ilitaka kushiriki kuamua nani ataongoza ibada.
Hata hivyo, familia imeazimia kutimiza matakwa ya Lungu ya kuzikwa faragha na Hichilema hapaswi kuwa popote karibu na mwili wa hayati Lungu.
Imeandikwa na Sute Kamwelwe kwa msaada wa mashirika ya habari.