Pombe ya ulanzi yagundulika kusaidia utunzaji viumbe maabara

Dar es Salaam. Ulanzi ni kinywaji cha asili kinachopatikana zaidi katika maeneo ya nyanda za juu kusini mwa Tanzania, hasa miongoni mwa jamii za Wabena, Wakinga na Wanyakyusa.

Kinywaji hicho hugemwa kutoka katika mianzi na kuachwa kwa saa kadhaa kabla ya kuanza kutumika.

Kwa muda mrefu ulanzi umejizoelea umaarufu zaidi kwa matumizi ya kijamii na kiutamaduni, lakini tafiti za hivi karibuni zinaonyesha kuwa kinywaji hiki kina uwezo mkubwa wa kutumika kama malighafi ya kutengeneza bidhaa mbalimbali ikiwemo nishati.


Moja ya tafiti kuhusu kinywaji hicho imefanywa katika Chuo Kishiriki cha Elimu Mkwawa cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (MUCE).

Katika tafiti yao waliyoifanya kwa zaidi ya mwaka mmoja, wamegundua kuwa kupitia ulanzi unaweza kutengenezwa nishati aina ya bioethanol kemikali muhimu kwa ajili ya kuhifadhia viumbe katika maabara za kibaiolojia.

Pia wamegundua ulanzi unaweza kuwa malighafi ya kutengenezea vitakasa mikono ‘sanitizer’, spiriti, mifuko ya plastiki ambayo ni rafiki kwa mazingira, mvinyo wa asili na bidhaa nyinginezo.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi, mmoja wa waliofanya utafiti huo ambaye pia ni Mhadhiri Mwandamizi wa Idara ya Kemia kutoka Muce, Dk  Jovin Emmanuel amesema ulanzi ni kinywaji cha asili ambacho mara nyingi kimekuwa kikitumiwa na watu wenye kipato kidogo kutokana na kuuzwa kwa gharama ndogo.

Dk Emmanuel anasema hilo ni moja kati ya jambo lilimsukuma yeye na wenzake kuumiza kichwa na kufanya utafiti kuhusu pombe hiyo ili kuiongezea thamani.

Pia, kuiongezea matumizi yake kwa kutengeneza bidhaa mbalimbali ambazo ni rafiki kwa mazingira.

“Kwa zaidi ya mwaka mmoja nikiwa pamoja na Dk Lewis Mtashobia na mwanafunzi wetu Osia Mwanaesi, tulifanya utafiti ambao uliweza kuiongezea thamani na kubadilisha ulanzi kuwa bidhaa mbalimbali zenye matumizi mapana katika sekta ya afya, viwanda na hata nishati mbadala,” anasema.

Ulanzi kutengeneza nishati

Anaeleza kuwa kutokana na kuongezeka kwa uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi nchini, walipata wazo la kutafiti iwapo ulanzi ungeweza kutumika kutengeneza nishati.

Pombe ya ulanzi ikiwa kwenye chombo tayari kwa ajili ya kunywa. Picha na Mtandao



Anasema baada ya kufanya utafiti walibaini kuwa kupitia ulanzi unaweza kutengeneza nishati ya nishati aina ya bioethanol.

Nishati aina ya bioethanol ni aina ya nishati mbadala (renewable energy) inayotokana na mchakato wa kuchakata sukari au wanga kutoka kwenye mimea.

“Nishati hiyo ni rafiki kwa mazingira na inaweza kutumika kupikia, koroboi zinazotumia nishati safi pamoja na mafuta kwa ajili ya magari yanayotumia nishati ya bioethanol,” amesema.

Bidhaa zinazotumika hospitalini, maabara

Dk Emmanuel ameeleza kuwa utafiti huo ulibaini Ulanzi unaweza kutumika kama kemikali maalum ambayo inatumika kuhifadhia baadhi ya viumbe visioze kama vile mijusi, chura, jongoo katika maabara kwa ajili ya kujifunza.

“Kiminika hiki ni cha asili hivyo ni salama zaidi kiafya pia ni gharama nafuu,” ameeleza mtafiti huyo.

Ameeleza kuwa ulanzi unaweza pia kutengenezea vitakasa mkono ‘sanitizer’, spiriti, mvinyo, mifuko ya plastiki ambayo ni rafiki kwa mazingira, mvinyo wa asili na bidhaa nyinginezo.

“Tuko katika hatua ya awali ya kutengeneza bioplastics zinazotokana na ulanzi, lengo likiwa ni kuja na mifuko ya plastiki inayooza, Hii itakuwa mbadala mzuri wa mifuko ya plastiki inayochafua mazingira,” ameeleza.

Hata hivyo amesema kuwa pamoja na ugunduzi ambao wameufanya bado bidhaa hizo hazijaingia rasmi sokoni zikiwa katika hatua mbalimbali ya kuidhinishwa na mamlaka husika na kupewa kibali.

Dk Emmanuel amesema anaamini kupitia utafiti na ugunduzi huo walioufanya utafanya ulanzi kuongezeka thamani na kutambulika zaidi kimataifa.

“Naamini ugunduzi huu ukiendelezwa unaweza kusaidia kuongeza kipato cha wananchi wa vijijini kwa kuwawezesha kuuza ulanzi kwa bei ya juu zaidi, kuzalisha ajira, kuimarisha uchumi wa viwanda, na kuongeza mapato kwa chuo na serikali kupitia kodi,” amesema.

Related Posts