“Hakuna sehemu ya kukaa, hakuna meza, hakuna kiti. Tunazungumza tukiwa tumesimama na kwa njia ya simu, mbele ya maaskari na wengine. Hii sio faragha,” anadai Lissu.
Lissu anabainisha kuwa zaidi ya mara moja, Mkuu wa Gereza anakataa kumruhusu kuonana na mawakili wake kwa faragha, licha ya kuwa ni haki yake ya kikatiba na kwa mujibu wa Kanuni za Usimamizi wa Magereza pamoja na ‘Mandela Rules’ (Kanuni za Kimataifa za Haki za Wafungwa).
Aidha, anadai kuwa mawakili wake walijitahidi sana kutafuta haki hiyo bila mafanikio, hadi kufikia hatua ya yeye kuamua kujitetea mwenyewe ili wasije kulaumiwa baadaye endapo kutatokea dosari yoyote katika kesi hiyo.
“Hii ni kesi yangu, na kwa kuwa adhabu ya uhaini ni kifo kwa kunyongwa, sitaki mawakili wangu waje kulaumiwa. Kuanzia leo, nitajitetea mwenyewe,” alidai
Lissu pia alilalamikia kukiukwa kwa haki yake ya kuabudu akiwa gerezani, akidai kunyimwa ruhusa ya kushiriki ibada za Kikristo tangu alipohamishiwa Gereza la Ukonga, hata katika sikukuu muhimu kama Ijumaa Kuu na Pasaka. Alidai hali hiyo inakiuka haki za binadamu na kanuni za magereza, zinazotambua haki ya mfungwa kuabudu.
Mbali na hilo, Lissu alifichua kuwa amekuwa akishikiliwa katika sehemu ya gereza inayohifadhi wafungwa waliokwishahukumiwa kunyongwa, licha ya kwamba yeye bado hajahukumiwa. Anadai anafuatiliwa na askari wawili kila anapotoka kwenda kuonana na mawakili au wageni, kama ilivyo kwa wafungwa waliokwishahukumiwa adhabu ya kifo.
“Naishi kwenye eneo la kusubiri kunyongwa, ninatembea katikati ya mifereji ya maji machafu. Hii ni hatari kwa afya yangu na usalama wangu,” alidai.
Akijibu hoja hizo, Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga, alidai Mahakama ilishatoa uamuzi kuhusu ombi la Lissu la kujitetea mwenyewe, na kwamba upande wa Jamhuri haukuwa na pingamizi. Aliongeza kuwa baadhi ya malalamiko yaliyotolewa yanahusu uongozi wa gereza na hayapaswi kujadiliwa mahakamani pasipo kufuata taratibu rasmi za kisheria, kama vile kuwasilisha maombi maalum ya mandamus.
Katika hatua nyingine ya kesi hiyo, Katuga alidai kuwa jalada la kesi bado lipo ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kwa ajili ya kulipitia na kutoa maelekezo ya kama kesi hiyo itahamishiwa Mahakama Kuu au la.