VIDEO: Lissu asimulia anayopitia gerezani, Hakimu asema…

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu ametumia zaidi ya dakika 40 kizimbani kusimulia madhira anayokutana nayo katika Gezera za Ukonga, jijini Dar es Salaam.

Lissu anayekabiliwa na kesi mbili ya uhaini pamoja na ya kuchapisha taarifa za uongo mitandaoni, zinasikilizwa na mahakimu wawili tofauti zote na zote zimeendelea leo Jumatatu, Juni 16, 2025 katika hatua tofauti tofauti.

Kesi ya uhaini inasikilizwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Franco Kiswaga. Upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Nassoro Katuga umeomba kesi kuahirishwa.



Lissu aibua mazito mahakani, asimulia magumu

Wakili Katuga amesema upelelezi wa kesi hiyo umekamilika, jalada lipo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ambaye analisoma na ataamua kama alipeleke Mahakama Kuu au la. Hakimu Kiswaga ameiahirisha hadi Julai 1, 2025.

Kabla ya kufikia ahirisho, Lissu alinyoosha mkono baada ya Wakili Kiongozi wa Jopo linalomtetea, Mpale Mpoke kumaliza kuwatambulisha mawakili wake (Lissu) zaidi ya 30 akiwemo kaka yake, Alute Mughwai.

Baada ya Hakimu Mfadhiwi, Kiswaga kumruhusu, Lissu amewashukuru mawakili wake jinsi ambavyo wamepambana kwa hatua mbalimbali ndani na nje ya Mahakama kwenye kesi hizo na kuwaomba wamachie awakabili mawakili wa Serikali.

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu akizungumza leo Jumatatu, Juni 16, 2025 wakati kesi yake ikiendelea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisuru.



“Nawashukuru mawakili wangu. Mmepigana kwa ujasiri, kwa weledi, mlitimiza wajibu wenu na mlifanya vizuri sana. Sasa ni wakati wa kupisha ili kuanzia sasa mimi ndiye nitakayejibizana na hawa mawakili wa Serikali,” amesema Lissu.

Rais huyo wa zamani wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) amedai kwa siku 68 alizokaa Gereza la Keko kwa wiki moja kisha kuhamishiwa Gereza Kuu la Ukonga, mawakili wake wamekuwa wakifika gerezani ili kushauriana juu ya kesi yake.

“Katika siku hizi 68 nilizokaa gerezani, hawajaruhusiwa kuniona na kuwasiliana na mimi na kuzungumza na mimi kwa faragha,” amedai Lissu.

Amedai Gereza Kuu la Ukonga kuna chumba ambacho kuna mapokezi na mbele kuna chumba ambacho kina kioo, wanasimama upande wa pili na anaanza kuwasiliana nao kwa simu.

“Hakuna fursa ya kubadilishana nyaraka na mimi nina nyaraka nyingi kidogo, hakuna fursa ya kuandika kwani hakuna kiti, yaani tunazungumza kwa simu. Sasa mheshimiwa hakimu, nimedai sana, nina haki ya kuonana na mawakili, siyo mapenzi ya bwana jela na bwana jela amenikatalia,” amedai Lissu.

Amedai kuna wakili alikwenda kuonana naye: “Nilipopiga sana kelele, bwana jela akasema nizungumze naye mbele ya maofisa wa magereza. Lakini hizo simu wanazotaka nitumie kuzungumza nani anazisikiliza.

Nani anayejua kwamba kuna mtu mwingine anayesikiliza, nani anajua kwenye control room hakuna vinasa sauti ili kunasa mazungumzo yangu na mawakili. Mheshimiwa hakimu hii ni kinyume kabisa na kanuni.”

Lissu ambaye kitaaluma ni mwanasheria amedai kwa mujibu wa kanuni: “Anayeamua usionane na wakili ni Mahakama tu na wala si bwana jela.”

Jambo jingine, Lissu amedai kwa siku 68 amekuwa akiomba aende kusali: “Lakini bwana jela amekataa kila Jumapili ikiwemo Jumapili ya jana. Wafungwa na mahabusu wote wanakwenda isipokuwa mimi.”

Lissu akirejea kanuni mbalimbali amesema: ”Kiongozi wa kiroho ataruhusiwa kutembelea magerezani kwa muda unaofaa, siyo kwenda kuwaambia habari gani, kwenda kuwapa huduma ya kiroho, Waislamu kila Ijumaa, sisi Wakristo kila Jumapili, wote wanakwenda isipokuwa huyu mhaini ambaye hatakiwi hata kuomba Mungu.”

Aidha amesema, ikiwa mfungwa au mahabusu hajabatizwa au kupata kipaimara anaruhusiwa kupata mafundisho: ”Na siyo lazima, unakwenda ukitaka, sasa mimi nimekata lakini nimezuiliwa kwa siku 68, kwa hiyo haki yangu ya kuabudu imekiukwa vibaya sana, haki yangu ya kisheria.”

“Na nimewaambia mawakili wangu muda wote, wamenipambania sana, imeshindikana,” amedai.

Mahakama ikiwa kimya ikimsikiliza Lissu, ameeleza jambo la tatu ambalo amedai: “Hivi nina kaa wapi gerezani Ukonga?.”

Amedai Gereza la Ukonga lina sehemu mbili ambazo kuna sehemu ambayo wafungwa wote ambao wamehukumiwa maisha, miaka 30, miaka mitano na mahabusu wanakaa na kuna sehemu moja inaitwa eneo maalumu ambalo wanakaa wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kifo kwa kunyongwa.

“Mimi nakaa kwenye hiyo sehemu wanayokaa wanaosubiri kunyongwa. Ukikaa hili eneo kama ninalokaa mimi, ambaye sijahukumiwa bado labda tutafika huko, wanapaswa kutenganishwa na wafungwa wengine wote.

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu akijadiliana jambo na mawakili wake leo Jumatatu, Juni 16, 2025 wakati kesi yake ikiendelea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisuru.



“Mimi ninakaa eneo hili tangu Ijumaa Kuu na nikitoka kwenda kuonana na mawakili au ndugu zangu, nafuata na maaskari wawili kama wanavyotakiwa kufanya kwa waliohukumiwa kunyongwa, mimi sijahukumiwa kunyongwa,” amedai Lissu.

Amedai pamoja na kuwekwa eneo hilo bado anakuwa na haki ya kuabudu, kufanya mazoezi: “Lakini kwenye chumba ninachokaa, kuna uwanja mkubwa, wanaotaka kutembea wanaotembea, wanaotaka kukimbia wanakimbia isipokuwa wanaoshia eneo hili.”

Lissu amedai anapaswa kufanya mazoezi na kutokana na mazingira, anafanya mazoezi katika mifereji ya maji machafu licha ya mguu wake kutokuwa imara ulioshambuliwa na watu wasojulikana kwa risasi Septemba 7, 2017.

Amesema Sheria ya Magereza kifungo cha 72 kinaeleza mfungwa aliyehukumiwa kunyongwa asichanganywe na wafungwa wengine: “Nimewaambia hili mawakili wangu, siku 68, wamepambana lakini wameshindwa.”

“Mheshimiwa Hakimu, mawakili wangu wameniambia wamewasilisha haya mbele yao juu ya ukiukwaji huu wa haki mfungwa, jibu walilonieleza wameambiwa Mahakama haiingilii mambo ya magereza,” amedai.

Lissu amedai kuwa amewambia kuwa Hakimu Kisanga alitembelea Mahakama na kwa mujibu wa sheria Mahakama ndiyo inafuatilia mambo ya wafungwa na mahabusu na wala si bwana jela (Mkuu wa Gereza).

Baada ya maelezo marefu ya Lissu, Hakimu Mfawidhi, Kiswaga amekubaliana na hoja ya Lissu ya mawikili wake wajitoea na kwamba yeye (Lissu) atakuwa ajikitetea.

“Kwa sasa mshtakiwa atajitetea mwenyewe kama alivyoomba na kuanzia sasa ni mawakili wa Serikali dhidi ya mshtakiwa,” amesema Kiswaga.

Kuhusu hoja zingine, Hakimu Mfawidhi, Kiswaga amesema: “Nimezichukua hoja zako na nitazifanyia kazi kiutawala na siyo kimahakama. Na mimi kama mfadhiwi nimekuwa natembelea (Magereza) na zitafanyiwa kazi kiutawala sawa sawa.”

Related Posts