Dodoma. Jina la Edward Lowasa limetajwa bungeni kutokana na msimamo wake wa uwekezaji katika sekta ya elimu huku Tanzania ikitakiwa kusimamia jambo hilo.
Kauli hiyo imetolewa bungeni leo Jumatatu Juni 16, 2025 na Mbunge wa kuteuliwa Shamsi Vuai Nahodha ambaye amesema bila kuwekeza katika elimu maendeleo ya nchi yatakuwa ndoto.
Nahodha ametoa kauli hiyo wakati akichangia Bajeti Kuu ya Serikali kuhusu hali ya uchumi wa taifa kwa Mwaka 2024, mpango wa maendeleo wa taifa kwa Mwaka wa Fedha 2025/26 na Makadilio ya mapato na matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/26.
Nahodha ambaye ni Waziri Kiongozi mstaafu wa Zanzibar amesema Edward Lowasa akiwa Waziri Mkuu alitaja vipaumbele vitatu ambayo ni elimu, elimu na elimu.
Lowassa alikuwa waziri mkuu kuanzia Desemba 30, 2005 hadi Februari 7, 2008 katika utawala wa wamu ya nne wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete. Alifariki dunia Februari 10, 2024.
Aidha, katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, Lowassa alikuwa mgombea urais wa Chadema akiungwa mkono na vyama vilivyoshirikiana vya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), vya CUF, NCCR-Mageuzi na NLD ambapo sera ya elimu, elimu, elimu alisisitiza na kuahidi angeingia madarakani angeifanyia kazi.
Katika mchango wake bungeni, Nahodha amesema Mzee Lowassa katika sekta ya elimu na teknolojia aliweka nguvu nyingi katika kuhakikisha sekta hiyo inasonga mbele kwa kasi nchini Tanzania.
Akiwa Waziri Mkuu katika awamu ya kwanza ya Serikali ya awamu ya nne, Lowasa alisimamia ujenzi wa shule za sekondari kila kata shule ambazo zimetajwa kuwa mkombozi wa elimu kwa nchi nzima.
“Lowassa alisema akipewa nafasi ya kutaja vipaumbele vikuu vitatu vya mipango ya maendeleo ya taifa basi atataja kipaumbele cha kwanza elimu, cha pili elimu na cha tatu kitakuwa elimu kwani elimu inapaswa kuwa kipaumbele cha kwanza kwa mustakabali wa Taifa letu,” amesema Nahodha.
Amesema Taifa lolote linalotaka kujikomboa na kuondokana na umasikini halina budi kuwekeza katika elimu ili wananchi wake waweze kuelimika.
Kwa upande mwingine ameitaka Serikali kuwekeza katika Chuo Kikuu cha Nelson Mandela kwenye ujenzi wa mabweni na maabara kwani kimekuwa na sifa nzuri ya kuzalisha wataalamu lakini miundombinu yake imechoka.