Arusha. Kwa mara ya kwanza, Uwanja wa Ndege wa Arusha umeanza kupokea ndege kutoka nje ya nchi moja kwa moja tofauti na ilivyokuwa awali ambapo walikuwa wakilazimika kwenda katika viwanja vingine kufanya ‘clearance’ (kupata vibali) kabla ya kutua uwanjani hapo.
Hiyo inatajwa kuwa fursa kwa wafanyabiashara, watalii kutoka nje ya nchi kupunguza gharama na kupoteza muda mwingi ambapo safari hizo hizo zimeanzia kwa ndege ndogo ambapo uwanja huo unaendelea kupanuliwa.
Hayo yamebainishwa leo Jumatatu Juni 16, 2025 na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda wakati akizungumza uwanjani hapo baada ya safari hizo kuanza rasmi jana Jumapili Juni 15, 2025.
Amesema hatua ambazo Serikali imepiga ni pamoja na kuhakikisha mazingira bora ya kukuza uchumi na kuwa uwanja huo sasa utaruhusu watu kutoka nje ya nchi kutua uwanjani hapo moja kwa moja.
“Uwanja wetu ulikuwa unatumika kama uwanja wa ndani, maana yake ulikuwa hauruhusu mtu yoyote kutoka nje ya nchi kutua hapa, siyo mpaka, aanzie viwanja vingine vya ndege, agongewe mihuri kama ya Uhamiaji, TRA na zingine. Na hiyo ni moja ya changamoto ambayo iliwasumbua wafanyabiashara wengi na watalii katika mkoa wetu, wengine wakitumia saa nyingi barabarani wakati walitamani kutumia ndege zao kupunguza muda na waweze kufanya mambo yao.
“Tulimuomba Rais Samia Suluhu Hassan, tuanze kupokea wageni wa kimataifa moja kwa moja katika uwanja huu japo kwa ndege ndogo na fursa ziko nyingi ikiwemo kukomboa muda na inaokoa gharama ambazo wafanyabiashara au watalii walikuwa wanalazimika kutumia ili kufika Arusha. Kwa lugha nyepesi, Arusha imefunguka na leo tumeshuhudia ndege zimeanza kuingia,” amesema.
Mkuu huyo wa mkoa amesema hatua hiyo itakuwa fursa hata kwa wamiliki wa ndege ndogo wa nchi jirani ambao watakuwa na mikutano iwapo wana ndege binafsi, zitawarahisishia kufanya mikutano yao na kurejea nchini mwao kwa haraka.
Amesema maboresho mbalimbali yanaendelea uwanjani hapo ikiwemo kuweka taa na kuwa Desemba 2025, uwanja huo utaanza kufanya kazi kwa saa 24.
“Tunaomba wenye kampuni za ndege, kwa unyenyekevu mkubwa, yako mambo tunafanya ili kutumia uwanja huu vizuri. Ombi langu, muanze safari kutoka Arusha kwenda Dodoma, kuna abiria wengi sana, kama Rais amefungua mazingira haya fungueni milango tukifanya hivyo tutatimiza ndoto za Arusha kufikika kirahisi zaidi na kila mtu aokoe muda na atengeneze fedha,” ameongeza.
Meneja wa uwanja huo, Edgar Mwankuga amesema wanaipongeza Serikali ambayo imewekeza kwenye kiwanja hicho na kumekuwa na miradi mingi kuanzia ujenzi wa jengo la abiria, maegesho ya ndege yameboreshwa.
“Sisi kazi yetu ni kuhakikisha huduma ambazo tunazitoa hapa ni za kiwango cha juu ili tuweze kuwaridhisha wateja wetu wanaotumia kiwanja cha ndege cha Arusha. Hatua hii ya leo ni kubwa kwetu kwa sababu tunaongeza movement (safari) za ndege,” amesema.
“Itaongeza mapato na kuimarisha utalii, uwekezaji na biashara ambayo sasa mamlaka tutafaidika na wananchi kwa ujumla,” amesema.

Meneja huyo amesema maboresho uwanjani hapo yalianza mwaka 2021 ambapo walikuwa na uwezo wa kuhudumia abiria 130,000 kwa mwaka, lakini kwa sasa wanahudumia abiria zaidi ya 400,000 kwa mwaka.
Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Arusha, Fakih Nyakunga amesema watashirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuhakikisha wageni wanaoingia nchini kupitia uwanja huo wanafuata sheria na taratibu za nchi.
“Mkoa tumepewa watendaji, mifumo na vifaa vingine ambavyo kwa namna moja ama nyingine vitasaidia kuwasaidia wageni wanaoingia nchini na sisi kama uhamiaji tuko katika uwanja huu tumeanza kutoa huduma,” amesema.
Ameongeza: “Na tutazitoa kwa mujibu wa taratibu zilizopo, uhamiaji ni usalama na maendeleo tutahakikisha kwa kushriikiana na vyombo vingine vya usalama, wageni wote wanaoingia uwanja huu kama sehemu ya mpaka wanafuata taratibu za nchi.”