Serikali kujenga shule maalumu ya wavulana Kanda ya Ziwa

Mwanza. Serikali inatarajia kujenga shule maalumu ya wavulana Kanda ya Ziwa, ambayo itajengwa mkoani Simiyu ikiwa ni mwendelezo wa mkakati wa kuzalisha wataalamu wa Tanzania kupitia elimu ya sayansi.

Akizungumza leo, Jumatatu Juni 16, 2025, mara baada ya kuzindua Shule ya Wasichana ya Mkoa wa Simiyu, Rais Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali haitabagua jinsia katika uwekezaji wa elimu ya sayansi.

“Siyo wa kike tu. Kwa hapa Simiyu, ukiacha shule hii ya wasichana, tunajenga shule maalumu ya wavulana ya Kanda hii ya Ziwa. Itajengwa hapa Simiyu, kwa madhumuni yale yale.

“Watoto wetu wenye akili za sayansi, wavulana na wasichana, wapate fursa ya kusoma kwenye shule maalumu ili tufikie lengo la kuzalisha wataalamu wa kitanzania,” amesema Rais Samia.

Ameongeza kuwa hapo zamani kulikuwa na shule chache tu zenye mazingira ya kuibua vipaji vya wanafunzi wa masomo ya sayansi, hasa zile zilizopo kwenye miji mikuu, lakini sasa Serikali inapanua wigo kwa kila mkoa kuwa na shule kama hizo.

“Mbali na shule hizi za vipaji, tunajenga pia shule za masomo ya amali na ufundi. Hapa Simiyu tunakuja kujenga moja. Watoto wetu wakitoka kwenye shule hizi na hawakupata sifa za kuingia vyuo vikuu, waende Veta kupata maarifa ya kuendesha maisha yao,” amesema Rais Samia.

Rais Samia amesema shule maalumu kwa watoto wa kike tayari zimejengwa katika kila mkoa nchini. Amesema baadhi zimekamilika na nyingine ziko katika hatua mbalimbali za ujenzi.

“Tunajenga shule hizi kwa sababu katika mkondo wa kawaida, watoto wa kike hasa mikoani, hata walipofaulu, walikuwa wakiachwa. Shule hizi zinawapa nafasi ya kipekee kusoma masomo ya sayansi na kuwa wataalamu wa baadaye,” amesema.


Amesisitiza kuwa mabweni na mazingira salama katika shule hizo yanawawezesha wanafunzi kusoma kwa utulivu bila usumbufu.

“Muwaachie watoto wa kike wenye akili nzuri wasome. Majengo haya yanajengwa kwa ajili yao. Mkiwazuia au mkiwaharibia katikati, maana yake tunapoteza fedha za Serikali na lengo halifikiwi,” amesema Rais Samia.

Awali, akitoa taarifa kwa Rais Samia, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa amesema wametekeleza maelekezo ya Rais kwa kujenga shule maalumu 26 za wasichana katika mikoa yote kwa gharama ya takriban Sh115.48 bilioni.

“Mpaka sasa, shule zote 26 zimekamilika na wasichana 9,810 wako darasani. Mkoa wa Simiyu umetumia Sh4.45 bilioni kujenga shule ya kisasa ambayo tayari ina wanafunzi. Katika shule hizi saba za awali, tayari wasichana 256 wamefanya mitihani ya kidato cha sita na matokeo yanatarajiwa kuwa mazuri,” amesema Mchengerwa.

Ameeleza kuwa shule hizo zinachukua wanafunzi waliopata alama za juu zaidi katika masomo ya sayansi.

Shule ya Wasichana ya Mkoa wa Simiyu imejengwa katika eneo la ekari 32.5 ikiwa na miundombinu ya mabweni, viwanja vya michezo, nyumba tano za walimu, madarasa 22, maabara nne, jengo la utawala, bwalo, jiko, jengo la Tehama, jengo la wagonjwa, maktaba na vyoo vya matundu 16.

Mkuu wa shule hiyo, Huruma Mtindya, amesema pia kuna fensi yenye urefu wa mita 350, nguzo za matenki mawili ya maji, na kisima kirefu.

Amesema katika ujenzi wa shule hiyo, mpaka Mei 30, 2025, fedha iliyotumika ni zaidi ya Sh4.159 bilioni, salio likiwa ni zaidi ya Sh290 milioni huku, shule ikiwa imewezeshwa nishati safi ya kupikia, hivyo mazingira ya kuandaa chakula ni rafiki.

Hata hivyo, amesema changamoto zilizopo ni ukosefu wa samani kwenye bwalo la chakula, ukosefu wa jenereta na gari la shule.

“Tunapenda kukushukuru wewe binafsi na Serikali kwa kutupatia fedha hizi ambazo zimewezesha kujenga miundombinu bora kwa ajili ya watoto wa kike. Hii itaboresha kiwango cha taaluma, hususan katika masomo ya sayansi,” amesema Mtindya.

Related Posts