WAKATI kikosi cha Tabora United kikijiandaa na mechi ya keshokutwa Jumatano ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam FC, wachezaji wa timu hiyo wanadaiwa kuweka mgomo baridi hadi pale ambapo watakapolipwa mishahara ya miezi miwili.
Timu hiyo imebakisha mechi mbili za kuhitimisha msimu huu ikianza ugenini kesho dhidi ya Azam, huku kikosi hicho cha Nyuki wa Tabora, kikiwa na kumbukumbu nzuri ya kushinda mabao 2-1 katika mechi ya duru la kwanza iliyopigwa Desemba 13, 2024.
Baada ya hapo, Tabora itaufunga msimu kwa kucheza na Coastal Union pia ugenini kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga Juni 22, huku timu hizo zikiwa na kumbukumbu ya kutoka sare ya 1-1 zilipokutana mechi ya mkondo wa kwanza mjini Tabra Desemba 17, 2024.
Baadhi ya wachezaji kutoka ndani ya timu hiyo ambao wameomba kuhifadhiwa majina yao, wameliambia Mwanaspoti wameamua kuchukua uamuzi wa kugoma kutokana na madai ya mishahara yao ambayo hawajalipwa kuanzia mwezi wa tano na huu wa sita.
“Tumekuwa tukipiga kelele sana juu ya hili lakini viongozi hawaonyeshi ushirikiano wowote jambo ambalo limetufanya kwa umoja wetu kugomea hadi watakapolipa au kusikiliza mahitaji yetu muhimu tunayoyahitaji,” alisema mmoja wa wachezaji hao.
Mchezaji huyo alisema suala la kucheza halina shida kwa sababu ndio kazi yao, japo wanachohitaji ni kuona viongozi wanachukulia kwa uzito mahitaji yao, kwani wana familia na watu mbalimbali wanaowategemea katika kuendesha maisha yao.
“Suala hili limeanza kwa baadhi ya benchi la ufundi tangu mwanzoni ambao pia wamekuwa wakiondoka kwa sababu za aina hii na uongozi hauchukulii kwa usiriasi mkubwa, sasa tumeona na sisi wachezaji tufanye uamuzi huu,” alisema mchezaji huyo.
Akizungumza na Mwanaspoti kuhusiana na suala hilo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Tabora United, Charles Obiny alisema hawezi kuzungumza mambo ya mtandaoni kwa sababu kwa sasa malengo yao ni kuhakikisha wanamaliza mechi mbili vizuri zilizobakia katika Ligi Kuu Bara.
“Kama kuna suala la kutolipwa ambalo linaelezwa hilo halijafika bado mezani kwangu na likiwepo sisi kama uongozi tutatoa taarifa. Pia inapotokea mtu anadai hawezi kutumia kigezo cha kugoma bali anapaswa kufuata utaratibu,” alisema Charles.
Hadi gazeti hili linakwenda mitamboni jana Jumatatu msimamo wa wachezaji hao ulikuwa haujabadilika.
Tabora iliyopanda daraja msimu uliopita ikifahamika kama Kitayosce kabla ya kubadilisha jina kwa sasa ipo katika nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi ikimiliki pointi 37 zilizotokana na mechi 28, ikishinda 10 kutoka sare saba na kupoteza 11, ikifunga mabao 27 na kufungwa 39.
Msimu uliopita timu hiyo iliponea katika tundu la sindano kushuka daraja ikacheza mechi za mtoano, kwani katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ilimaliza ikiwa nafasi ya 14 ikiwa na pointi 27, ikishinda mechi tano, sare 12 na vipigo 13 ikifunga mabao 20 na kufungwa 41 katika mechi 30 ilizocheza.