Nairobi. Baada ya wiki moja ya maandamano na mijadala nchini Kenya kufuatia kifo cha mwalimu na mwandishi wa habari, Albert Ojwang’, hatimaye Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi, Eliud Lagat amejiondoa kwa muda kupisha uchunguzi unoendelea kuhusiana na sakata hilo.
Tovuti ya Taifa Leo imeripoti leo Jumatatu, Juni 16, 2025, kuwa Lagat amesema amechukua hatua hiyo kwa kutambua wajibu wake kama Naibu Inspekta Jenerali katika Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) na sababu uchunguzi unaoendelea kuhusu kifo cha kusikitisha cha Albert Ojwang’.
“Leo nimeamua kujiondoa kutoka ofisi ya Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi hadi uchunguzi unaoendelea utakapokamilika. Majukumu ya ofisi yangu kuanzia sasa yatatekelezwa na msaidizi wangu hadi uchunguzi utakapokamilika,” amesema Lagat.
Lagat ambaye anatakwa kuhusika kwenye mchakato wa kukamatwa kwa Ojwang’ ameahidi ushirikiano wa aina yoyote utakapohitajika kwa maofisa wanaochunguza tukio la kifo cha mwandishi huyo.
“Natoa salamu za pole kwa familia ya Albert Ojwang’ kwa kupoteza mpendwa wao,” amesema Lagat.
Ojwang’ alifariki dunia Juni 8, 2025 baada ya kupigwa na kuteswa mikononi mwa polisi katika Kituo Kikuu cha Polisi Nairobi, nchini Kenya.
Mwanablogu huyo, ambaye pia alikuwa mwalimu, alikamatwa nyumbani kwao Homa Bay, siku chache tangu Lagat awasilishe malalamiko yake kwenye Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kwamba mwandishi huyo alichapisha tarifa zinazomchfua mitandaoni.
Kifo cha Ojwang’ kimesababisha hasira kwa umma hususan baada ya ripoti ya Mtaalam wa Patholojia wa Serikali kufichua kuwa Ojwang’ alifariki dunia kwa madai ya kuteswa, kuteswa kikatili kunyongwa akiwa katika mahabusu ya polisi.
Tangu wakati huo, watetezi wa haki za kibinadamu, wanasiasa na raia wa kawaida wamekuwa wakiandamana kushinikiza Lagat ajiuzulu kwa madai kuwa amehusika kwenye mauaji ya mwanablogu huyo ambaye ni baba wa mtoto mmoja.