Sh216 bilioni kutumika chanjo, utambuzi wa mifugo kidijitali

Simiyu. Rais Samia Suluhu Hassan leo Jumatatu Juni 16, 2025, amezindua rasmi kampeni ya kitaifa ya chanjo na utambuzi wa mifugo, itakayotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka huu hadi 2029.

Uzinduzi huo umefanyika mkoani Simiyu, ambako Rais Samia ameongoza shughuli hiyo inayolenga kuboresha afya ya mifugo, kuongeza tija na kufanikisha upatikanaji wa masoko ya nje kwa mazao ya mifugo.

Akitoa taarifa ya kampeni hiyo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk Ashantu Kijaji amesema Serikali imetenga Sh216 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa programu hiyo kwa kipindi cha miaka mitano.

Amesema Serikali imetoa Sh19.2 bilioni kwa  mwaka huu wa kwanza wa utekelezaji awamu ya kwanza ya chanjo na utambuzi.

“Viwanda vyote vya ndani vimepewa jukumu la kuzalisha na kusambaza chanjo. Tutaanza kwa kuchanja kuku wa asili milioni 40 nchi nzima na chanjo hiyo itatolewa bure kabisa bila mchango kutoka kwa wafugaji,” amesema Dk Kijaji.


Ameongeza kuwa Serikali pia itatoa chanjo ya ugonjwa wa sotoka kwa mbuzi na kondoo milioni 17. Gharama ya chanjo hiyo ni Sh600 kwa kila mnyama na Serikali itatoa ruzuku ya Sh300 na mfugaji atachangia kiasi kilichobaki.

Katika hatua nyingine, Dk Kijaji amesema zaidi ya ng’ombe milioni 19 watapatiwa chanjo, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Shirika la Afya ya Wanyama Duniani linalotaka angalau asilimia 70 ya ng’ombe nchini kuchanjwa ili kupata ithibati ya kuuza mifugo na mazao yake kimataifa.

“Wafugaji wamekubali sasa kuondoka kwenye ufugaji wa asili, tunakwenda kufuga kibiashara ili taarifa za mifugo itakapochanjwa zote ziwe za kidijitali, popote unaweza kuona mifugo mingapi imechanjwa,”amesema Dk Kijaji.

Katika kuonesha usalama wa chanjo hiyo, ng’ombe wawili wa Rais Samia wamechanjwa hadharani wakati wa uzinduzi, kama ishara ya kuwahakikishia wafugaji kuwa chanjo hiyo ni salama.

Akitambulisha baadhi ya viongozi waliohudhuria kwenye mkutano wa Rais Samia na wananchi katika viwanja vya Nyakabindi mjini Bariadi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Riziki Shemdoe amesema  hiyo ni mara ya pili tangu nchi ipate uhuru kufanya kampeni ya chanjo kitaifa.

“Toka nchi hii imepata uhuru hii ni mara ya pili kufanya kampeni ya chanjo kitaifa, kwa mara ya kwanza lilifanyika awamu ya kwanza ya uongozi wa Taifa hili,”amesema Profesa Shemdoe.

Amesema, pia hiyo ni mara ya kwanza kufanyika utambuzi wa mifugo nchini, uzinduzi unaofanyika kwa kuzingatia teknolojia ya kisasa.


Naye, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Kenan Kihongosi amesema hali ya usalama mkoani humo ni shwari na shughuli zote za maendeleo zinaendelea vizuri, huku akibainisha kuwa Serikali imepeleka zaidi ya Sh1.4  trilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo, ikiwemo sekta ya afya, elimu, maji, na kilimo katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa awamu ya sita.

“Tumejenga Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu na kuipatia vifaa tiba vya kisasa, hali iliyofanya wananchi wetu kutoenda tena Bugando kufuata huduma za kibingwa,” amesema.

Wakati huohuo, Rais Samia amekabidhi pikipiki 700 kwa maofisa mifugo nchini, huku 120 kati ya hizo, zikitolewa mkoani Simiyu.

Mbali ya pikipiki, Rais pia amekabidhi vishikwambi 4,500 vitakavyotumika kuhifadhi taarifa za chanjo kwa njia ya kidijitali huku akiwataka waliokabidhiwa vitendea kazi hivyo kuvitumiwa kama ilivyokusudiwa.

Related Posts